Baada ya kumalizika kwa vita ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe huko Liberia, mwanasoka mstaafu, George Opong Weah, alitangaza kuwania urais wa nchi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, kisha akaanzisha chama kinachoitwa Congress for Democratic Change (CDC).
Lakini licha ya kuwa kwake maarufu nchini humo, Weah alikuwa akibezwa kwamba asingeweza kuliongoza taifa kwa vile hakusoma, tena akichuana na mhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani, Ellen Johnson-Sirleaf, na pia alidaiwa kutokuwa na uzoefu wa uongozi katika ngazi yoyote.
Sambamba na kuwa msomi kutoka chuo kikuu kinachoheshimika duniani, mama huyo pia alikuwa Waziri wa Fedha wa Serikali ya Rais William Tolbert katika miaka ya 1970. Alipoondoka Liberia baada ya Rais Tolbert kuangushwa kijeshi na Sajenti Samwel Doe mwaka 1980, Sirleaf alikwenda Marekani alikofanya kazi katika taasisi tofauti.
Alianzia kazi katika Benki ya Citibank, kisha Benki ya Dunia (WB) na baadaye akajiunga na Umoja wa Mataifa Makao Makuu jijini New York. Kana kwamba hiyo haitoshi, wapinzani wa Weah pia walizusha kuwa alichukua uraia wa Ufaransa wakati akicheza soka katika klabu ya Paris Saint Germain (PSG) kati ya mwaka 1992-1995, madai yaliyotupiliwa mbali na mahakama.
Pamoja na vikwazo hivyo vyote, mchezaji huyo wa zamani wa kandanda alifanya vizuri katika uchaguzi huo mkuu baada ya wagombea wote kukosa ushindi wa moja kwa moja, hivyo wakaingia mzunguko wa pili.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 11, 2005, Weah alipata asilimia 28.3, lakini duru ya pili iliyofanyika wiki nne baadaye hapo Novemba 8 akashindwa. Aliambulia asilimia 40.6 kati ya kura zote huku Sirleaf akijikusanyia asilimia 59.4 zilizobaki na kuwa rais mpya Liberia.
Akiwa ameonyesha upinzani mkali pamoja na kuanza kwa kudharauliwa, Weah aliposhindwa alidai kuwa uchaguzi huo haukuwa wa haki. Alilalamikia wizi wa kura, kubadilishwa kwa masanduku ya kupigia kura huku wafuasi wake wakiandamana kwa wingi hasa katika jiji la Monrovia kupinga matokeo.
Lakini yalipothibitishwa rasmi na mamlaka zinazohusika, baadhi ya viongozi barani Afrika waliomba wafuasi hao wa Weah wayaamini. Walifanya hivyo baada ya timu ya Umoja wa Afrika kusema “uchaguzi huo ulifanyika kwa amani, uwazi na kwa haki”.
Hapo ndipo Ellen Johnson-Sirleaf akatangazwa rasmi kuwa rais mpya wa Liberia na kuwa mwanamke wa kwanza barani Afrika aliyechaguliwa kidemokrasia kushika nafasi hiyo. Hata hivyo, kushindwa kwa Weah kulitokana kwa kiasi kikubwa zaidi na turufu ya elimu kuwa hakusoma, madai aliyoyajibu kwa utulivu na ujumbe mzito.
“Pamoja na uzoefu na elimu yao yote, wakaiongoza nchi yetu kwa miongo mingi, bado hakuna cha maana walichoifanyia hadi sasa,” alisema mara kadhaa akijibu tuhuma hizo dhidi yake.
Wakati huo huo, Weah pia alikuwa akisema ana Shahada ya Kwanza ya Utawala wa Michezo kutoka Chuo Kikuu cha Parkwood, London nchini Uingereza, lakini ikadaiwa kuwa hakuipatia darasani na wala haitambuliki popote duniani.
Kumalizika kwa uchaguzi huo mkuu na kuandamwa kwamba hakusoma kulimfanya aende Marekani, akajiunga na Chuo Kikuu cha DeVry, Miami alikosoma na kuhitimu Shahada ya Uongozi wa Biashara.
Katika kipindi hicho chote, mwanasoka huyo wa zamani kamwe hakuacha shughuli za siasa. Aliporejea Liberia mwaka 2009 aligombea Ujumbe wa Baraza la Seneti kupitia uchaguzi mdogo katika jimbo la Montserrado, hatua iliyochukuliwa na wengi kuwa maandalizi ya kugombea tena urais mwaka 2011.
Kama ilivyotarajiwa, Weah alitangaza kuwa angeingia katika mbio hizo kupambana kwa mara ya pili na Ellen Johnson-Sirleaf, huku akiwa hana tena tatizo la elimu aliyokuwa akiambiwa hana. Hata hivyo, kushindwa kwa chama chake cha CDChange kuungana na vyama vingine ili kusimamisha mgombea mmoja kulibadili kabisa harakati zake zote. Badala ya kuwania nafasi hiyo, CDC ilimteua kuwa mgombea mwenza wa urais huku jukumu hilo likiwekwa mikononi mwa Winston Tubman.
Alizaliwa Oktoba Mosi, 1966 katika eneo la Clara, Monrovia, mji mkuu wa Liberia na majina yake kamili ni George Tawlon Manneh Opong Ousman Weah. Alianza kabumbu na klabu ya Young Survivors Clareton mwaka 1981-1984 na kuhamia Bongrange Company aliyokaa nayo msimu mmoja, timu ambazo alizichezea katika soka la ujanani. Kama mwanasoka wa kulipwa aliichezea Mighty Barrolle mwaka 1985-1986, kisha akaenda Invisible Eleven mwaka 1986-1987 alipotoka nje ya Liberia.
Kwanza alijiunga na Africaine Sport ya Ivory Coast aliyoichezea mechi mbili tu na kuifungia bao moja, akaenda Tonnere de Yaoundé ya Cameroun. Alikaa nayo hadi mwaka 1988 alipokwenda Ulaya, na kuichezea Monaco ya Ufaransa kuanzia mwaka huo hadi 1992 aliponunuliwa na PSG.
Akiwa na timu hiyo, Weah aliiwezesha kutwaa ubingwa wa Ufaransa mwaka 1984. Alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Ligi ya Mabingwa ya Ulaya (UEFA) kwa msimu wa mwaka 1994/95, halafu akahamia AC Milan ya Italia aliyoichezea hadi mwaka 1999.
Kama mshambuliaji mahiri baada ya timu hiyo kuondokewa na mwanasoka maarufu kutoka Argentina, Diego Maradona, ambaye hivi sasa ni kocha wa Al Wasl ya Dubai, Falme za Kiarabu, Weah aliisaidia AC Milan kuwa Klabu Bingwa ya Soka ya Italia katika miaka ya 1996 na 1999.
Alikuwa Mwanasoka Bora wa Dunia wa Mwaka 1995, msimu ambao pia aliumaliza akiwa mfungaji wa kutegemewa zaidi wa timu hiyo, lakini akaihama mwaka 2000 na kupelekwa Chelsea ya England kwa mkopo. Alihamia Manchester City miezi michache baadaye na kuondoka tena mwaka uleule, akaenda Ufaransa kuichezea Olympique de Marseille.
Alihitimisha soka lake katika klabu ya Al-Jazra aliyoichezea kati ya mwaka 2001 na 2003 alipostaafu. Aliiwakilisha dimbani mara 60 timu ya taifa ya Liberia kuanzia mwaka 1988 na kuifungia mabao 22. Kama Mwanasoka Bora wa Dunia wa Mwaka 1995, Weah ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwa mchezaji pekee kutoka Afrika aliyetwaa taji hilo.
Waliomtangulia kuwa Wanasoka Bora wa Dunia tangu kuanzishwa kwa utaratibu huu mwaka 1991 ni Mathar Matthaus wa Ujerumani, Marco van Basten wa Uholanzi, Roberto Baggio wa Italia na Romario de Souza wa Brazil mwaka 1994.
Amewahi pia kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika katika miaka ya 1989, 1994 na 1995, lakini kubwa zaidi yeye ndiye Mwanasoka Bora wa Karne ya 20 wa Afrika. Uteuzi huo uliosimamiwa na Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (FIFA) na kuratibiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ulifanyika mwaka 1999 ukihusisha waandishi wa habari za michezo kutoka dunia nzima.
Wanasoka wengine wa karne ni Edson Arantes do Nascimento ambaye ni maarufu zaidi kama Pelé, wa Brazil kwa Amerika Kusini, Johan Cruyff wa Uholanzi kwa Bara la Ulaya, huku Diego Amando Maradona akiwa Mwanasoka Bora wa Muda Wote (All Time) Duniani.