Leo kupitia makala hii naomba tuwekane sawa katika mahusiano yetu. Dunia haiwezi kuwa salama bila msamaha. Familia yako haiwezi kuwa salama bila moyo wa msamaha. Lewis Smedes anasema: “Mtu wa kwanza, na mara nyingi ndiye ambaye huponywa na msamaha, ni yule ambaye anautoa msamaha huo. Tunaposamehe hali halisi ni kwamba tunakuwa tunamweka mfungwa fulani huru, na kisha tunagundua kwamba, mfungwa tuliyemweka huru alikuwa ni sisi.”
Kila mwanadamu anahitaji kuwa na furaha na amani katika maisha yake. Hakuna mwanadamu anayetamani kuwa na huzuni muda wote. Hakuna mwanadamu ambaye anapenda kuwa na msongo wa mawazo muda wote. Lakini unaweza kujiuliza maswali kadhaa; Kwa nini tunakutana na watu ambao maisha yao ni kujilaumu na kuwalaumu wengine?
Kwa nini tunakutana na wanadamu ambao wamejikatia tamaa ya kuishi duniani? Kwa nini tunakutana na watu ambao wana uchungu moyoni? “Hakuna mwanadamu aliyeshindwa kusamehe halafu akawa na maisha mazuri,” aliandika mtu fulani.
Kuna watu wengi wanaishi katika vifungo vya uchungu na kutokusamehe. Wengine wameapa kabisa na kusema: “Huyu sitamsamehe kamwe katika maisha yangu.” Mara nyingi tunafikiri kutokusamehe kunaleta madhara kwa yule asiyesamehewa lakini ukweli ni kuwa asiyesamehe ndiye anayeteseka zaidi.
Wengi tumejiapia viapo vya kutowasamehe waliotuumiza katika maisha yetu. Viapo hivi vimetufunga. Viapo hivi vinatutesa. Viapo hivi vinachochea hasira na maumivu makali kila kukicha. Tuko kifungoni. Hatujui tutatoka lini. Ni kweli, umeumizwa lakini leo fungua ukurasa mpya wa maisha yako.
Viachilie leo hivyo viapo vilivyokufunga. Msamehe mume wako aliyekuumiza. Msamehe mke wako aliyekuumiza. Msamehe mtoto wako aliyekuumiza. Msamehe kaka yako aliyekuumiza. Msamehe mama mkwe wako aliyekuumiza. Msamehe baba mkwe wako aliyekuumiza. Msamehe mzazi wako aliyekuumiza. Msamehe jirani yako aliyekuumiza. Msamehe shemeji yako aliyekuumiza. Msamehe rafiki yako aliyekuumiza. Msamehe bosi wako aliyekuumiza. Msamehe kila mtu aliyekuumiza katika maisha yako. Samehe! Samehe! Samehe!
Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, hayati Nelson Mandela anasema: “Kidonda kikubwa tunachosababishiwa hakiwezi kupona mpaka pale tunaposamehe.” Kutokusamehe kunaweza kukuangamiza wewe. Kucheua ubaya uliotendewa wewe, kulea uchungu, ni kudonoa kwenye donda lililo wazi na kukataa kuliruhusu lipone. Kuendelea kwetu kucheua, kukwazika, kubaki kwetu katika uchungu nafsini mwetu, mawazo yaliyojaa chuki, kutaka kwetu kulipa kisasi, hakumuumizi kabisa mtu mwingine aliyetutesa, na hakutuletei sisi jema lolote isipokuwa kunatufanya sisi tuharibikiwe tu.
Imebainika kwamba watu ambao hawasamehi wanaongoza kwa kujitabiria mambo mabaya katika maisha yao. Ni kweli. Kila kukicha matukio ya watu kujiua na kuwaua wenzao yanaongezeka. Kila siku kuna mtu mahali fulani akiamka asubuhi anawaza kujiua ama kuua. Kila siku kuna mtu mahali fulani akiamka asubuhi anahisi hawezi kufanya chochote chenye manufaa katika maisha yake.
Kila siku kuna mtu mahali fulani anaamka asubuhi akiwa amejawa woga wa kutofanikiwa kiroho, kimwili, kiuchumi na kifamilia. Kila siku kuna mtu mahali fulani akiamka asubuhi anawaza kufukuzwa kazi. Kila siku kuna mtu mahali fulani akiamka asubuhi anahisi kufilisika. Kila siku kuna mtu mahali fulani akiamka asubuhi anahisi hataolewa ama kuoa.
Mpendwa msomaji na rafiki yangu mwema, ‘Usiogope’. Usikate tamaa. Songa mbele. Imeandikwa: “Usiogope, kwa maana ‘Mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana Mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.’” [Isaya 4:6].
Maumivu ya kutokusamehe yanasababisha upweke. Watu wengi ni wapweke. Upweke ni gereza lisilo na ukuta. Upweke unatesa. Upweke unajeruhi sana. Kuna upweke wa aina nyingi. Upweke wa kiroho. Upweke wa kipato. Upweke wa kufiwa na mwenzi wa maisha. Upweke wa kukosa mtoto ndani ya ndoa. Upweke wa kuchelewa kuoa au kuolewa. Upweke wa kukosa malezi bora kutoka kwa wazazi. Upweke wa kukosa marafiki wazuri. Upweke wa kukosa kazi. Upweke umewafanya watu wengi wajione kama watu ambao hawastahi kuishi hapa duniani.
Upweke umewafanya baadhi ya watu wajione kama watu wasiostahili kupendwa. Kuna watu wamejinyonga kwa sababu ya upweke. Kuna watu wanajikataa kwa sababu ya upweke. Upweke umewafanya watu wengi kuwa na maumivu ndani ya mioyo yao.