Tetesi zimesambaa huko Kenya kuwa nyota wa muziki nchini hapa, Nandy, ni Mkenya. Tetesi hizo zinaeleza kuwa Nandy alizaliwa na kukulia Mombasa nchini Kenya, ingawa hazielezi wazazi wake ni kina nani. Tetesi hizo zinadai pia kuwa hadi hivi sasa mrembo huyo mwenye sauti nyororo ana maskani yake jijini Mombasa.

“Nandy ni msichana wa Mombasa na alikulia hapa,” amenukuliwa jamaa anayeishi eneo la Kisauni, anayedai kuwa mjengo wa mrembo huyo upo meta chache kutoka ilipo nyumba yake.

Jamaa huyo analonga zaidi: “Ninapafahamu anapoishi na connection ya Bongo ni kwa sababu yuko na familia huko.”

Hizi zinaweza kuwa habari za kushtua kwa wengi, hasa ikizingatiwa kuwa siku zote watu wanaamini kuwa mwanamuziki huyo ana damu ya Tanzania isiyo na mawaa.

Wakati Wakenya hao ‘wakijifaragua’ kuwa Nandy ni raia wa nchi yao, taarifa rasmi zinaonyesha kuwa Nandy, ambaye jina lake halisi ni Faustina Charles Mfinanga, alizaliwa Moshi, Novemba 9, 1992.

Nandy amewahi kushinda kama mwanamuziki bora wa kike kutoka Afrika Mashariki katika kinyang’anyiro cha All Africa Music Awards mwaka 2017.

Wazazi wa Nandy ni Mary Charles, ambaye anatajwa kuwa ni fundi wa nguo na Charles Mfinanga, fundi wa magari.

Jina Nandy ni kifupisho cha jina lake halisi, Nandera.

Alianza kazi ya muziki akiwa na umri mdogo. Akiwa na miaka mitano, alikuwa mmoja wa waimbaji wa kwaya ya watoto ya Kanisa la KKKT Moshi. Alisoma Shule ya Msingi Mawenzi kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Lomwe ambako alikuwa kiongozi wa kwaya.

Baada ya kumaliza kidato cha sita alijiunga na Chuo cha Biashara, CBE, jijini Dar es Salaam.

Alianza kujulikana kwenye muziki baada ya rafiki yake mmoja kumtambulisha kwa marehemu Ruge Mutahaba, ambaye alimwingiza Tanzania House of Talent (THT). Hapo ndipo alipokutana na Emma the Boy, ambaye alimsaidia kutoa wimbo wake wa kwanza, ‘Nagusagusa’.