Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, ameiomba Wizara ya Kilimo kuhakikisha inawalipa deni la Sh bilioni 5 wakulima wa korosho mkoani Pwani ambao hawajalipwa baada ya kuuza korosho zao msimu uliopita.

Ulega amesema hayo wakati wa mkutano wa wakulima wa zao hilo katika Wilaya ya Mkuranga hivi karibuni alipokwenda kuwasikiliza wakulima hao.

Ulega, ambaye alisikiliza kero hizo kama mbunge wa jimbo hilo, anasema baadhi ya wakulima wamekata tamaa ya kulipwa fedha za mauzo ya korosho ya msimu uliopita.

Akizungumzia mavuno ya msimu huu, Ulega, ambaye aliambatana na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, anasema mvua kubwa zilizonyesha na kukosekana kwa magunia ni kati ya sababu kuu zilizoathiri zao hilo jimboni mwake msimu huu.

Anasema mvua hizo zimeshusha ubora wa korosho, hivyo kuzifanya zisiweze kushindana kwenye soko la dunia.

Anaiomba wizara husika kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima kwa kuwatafutia mnunuzi mwenye kujali masilahi ya mkulima ili waweze kuuza korosho hizo kwa haraka.

Kwa upande wake, Mgumba, ameahidi kuyashughulikia matatizo hayo haraka iwezekanavyo ili wakulima wanufaike na jasho lao.

Mgumba anasema amefanya ukaguzi katika vyama vya ushirika vya msingi kupima ubora wa korosho na amegundua kwamba korosho nyingi zinastahili kuwa daraja la tatu baada ya kuathiriwa na mvua.

Anasema kwa kawaida korosho daraja la tatu zinabakia katika vyama vya ushirika vya msingi na zile za madaraja ya kwanza na pili zinapelekwa katika maghala makuu. Anaongeza kuwa korosho za Tanzania zinafahamika katika soko la kimataifa, hivyo kuzipeleka hizo za daraja la tatu kutaharibu sifa hiyo.

Lakini anaonyesha kushangazwa na wakulima hao kuendelea kudai Sh bilioni 5 kutoka msimu uliopita, akieleza kuwa tayari serikali ilikwisha kutoa fedha zote za malipo ya wakulima.

Anasema amebaini kuwa kuna watu wachache ambao walijilipa fedha hizo wao wenyewe badala ya kuwalipa wakulima waliokuwa wamepeleka korosho zao.

“Tumeligundua hilo na tutawashughulikia ipasavyo. Rekodi zetu zinaonyesha kuwa serikali ilikwisha kutoa fedha zote kulingana na kiasi cha korosho zilizokuwa zimekusanywa. Hao waliokula fedha hizo ni sawa na wamekula sumu,” anasema.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, anawataka wakulima hao kutokuwa na wasiwasi kwani korosho hizo zitauzwa kwa kuzingatia masilahi ya mkulima kwa njia ya stakabadhi ghalani.

Ndikilo anasema serikali itahakikisha inamlinda mkulima kwa kuwaleta wanunuzi katika AMCOS zao ili kununua kwa bei yenye masilahi kwa mkulima.

Mjumbe wa Chama cha Ushirika cha Msingi wilayani humo, Abdallah Namanguku, anawalaumu maofisa ugani kwa kushindwa kufanya kazi zao sawasawa kiasi cha kusababisha korosho kuharibika.