Katika sehemu ya nne tuliishia katika aya isemayo: Kama serikali ingelikubali azimio hilo lililobadilishwa, Dar es Salaam pasingekuwa na uchaguzi mwaka 1958. Ndiyo kusema Mwalimu Nyerere angeendelea kukaa katika Baraza la Kutunga Sheria kwa kuteuliwa na gavana ingawa baraza hilo mwaka 1958 lingekuwa na wajumbe 15 waliochaguliwa na raia. Kwa upande wake hili lingekuwa jambo la fedheha kidogo; lakini alikuwa tayari kukubali fedheha hiyo ili kusaidia kuondoa kero ya kura ya lazima. Sasa endelea…
Mwezi Septemba, 1957 alipinga sheria mpya iliyokusudia kuipa serikali uwezo wa kuanzisha mabaraza ya wilaya yaliyogeuka mabaraza ya utawala wa wenyeji. Sababu zake za kupinga sheria hiyo zilikuwa kubwa na alizieleza barazani kama alivyokwisha kuzieleza katika sauti ya TANU namba 15; serikali ilipotaka sheria hii ipitishwe angeweza kutoa azimio kwamba isipitishwe.
Kama angefanya hivyo, serikali isingepata hata nafasi angalau ya kuwavika machifu na raia wao kilemba cha ukoka. Lakini hakufanya hivyo. Aliomba serikali iahirishe jambo hilo mpaka baada ya miezi sita.
Alifurahi kwamba Bayldon, Rais wa Chama cha U.T.P., alimuunga mkono akaomba sheria hiyo izungumzwe mara ya mwisho katika mkutano wa Baraza la Kutunga Sheria uliokuwa ukifuata baada ya mkutano wa mwezi Februari.
Ombi hilo liliipa serikali nafasi ya kuendelea kuzungumza na machifu habari za sheria hiyo. Baadhi ya machifu walikuwa Mzumbe. Aliikumbusha serikali habari hiyo. Ilikuwa wajibu wa serikali kuheshimu kidogo manung’uniko ya machifu na kukubali kuahirisha sheria hiyo mpaka kupata maoni yao ya mwisho.
Hii isingezuia sheria hiyo kupitishwa, lakini ingeonyesha kwamba serikali ilikuwa tayari angalau kusikia, hata kama haikufuata maoni ya machifu na watu wao. Kama sheria ingekubali shauri hilo, sheria hiyo ingepitishwa mwezi Aprili au Mei, 1958.
Mabaraza yangeanzishwa yanayokiuka machifu ambao ndio ulikuwa msingi mkubwa wa kuimarisha serikali za mitaa na msingi ambao haukuwa na kifani katika serikali kuu. Hili halikuwa jambo rahisi kuachia lifanyike. Aidha, nia moja ya serikali katika kuanzisha mabaraza hayo ilikuwa ni kuwapatia nafasi Wazungu na Wahindi kushiriki katika serikali za mitaa.
Mwalimu Nyerere alisema tena katika Baraza la Kutunga Sheria kwamba alikuwa hapingai jambo hili. Lakini kama nia ilikuwa ni hiyo tu, palikuwa hapana haja kukiuka mabaraza ya utawala wa wenyeji na kuanzisha mabaraza mapya kabisa. Serikali yenyewe ilikuwa imekwisha kusema zamani na waziri wa utawala alikuwa amerudia kusema tena katika Baraza la Kutunga Sheria, kwamba katika mabaraza ya wilaya 56 ya utawala wa wenyeji, 36 yalikuwa yamewakaribisha Wazungu na Wahindi kwa hiari yao wenyewe.
Hii ilikuwa ni alama ya wazi wazi ya nia ya utawala wa wenyeji kufungua mlango wa mabaraza yao kwa Wazungu na Wahindi. Basi, palikuwa na haja gani kwa serikali kuwatia machifu mashaka ambayo yangeweza kuleta chuki baina ya mataifa bila sababu?
Serikali ilipokuwa ikifanya mambo ambayo yangeweza kuleta chuki katika nchi yetu, na wakati huo Serikali ya Tanganyika ikifanya mambo ambayo kama raia wote, Wazungu, Wahindi na Waafrika isingeambiwa iyaache yangeleta chuki mbaya sana kati ya mataifa.
Mashauri yote hayo, Mwalimu Nyerere aliyoipa serikali yalikataliwa. Kwa hiyo aliona kwamba ataidanganya nchi na TANU akiendelea kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, na kupokea mshahara wa baraza hilo, na kwenda katika makaribisho mbalimbali; na kuwadanganya watu kwamba anafanya jambo la maana katika baraza hilo, kumbe yeye mwenyewe alijua kwamba kazi yake ilikwisha. Kwa hiyo alikuwa hana budi ajiuzulu.
Mwalimu Nyerere aliporudi kutoka Amerika alisema kwamba amerudi mikono mitupu. Maadui wa TANU walishangilia wakasema kwamba hiyo ilionyesha kuwa Umoja wa Mataifa (U.N.O) haukuwa na madaraka yoyote Tanganyika.
Katika muda mfupi aliokaa katika Baraza la Kutunga Sheria alifanya jitihada kubwa zaidi kuliko alivyofanya mara zote tatu alipokwenda Amerika. Lakini alitoka katika Baraza la Kutunga Sheria mikono mitupu. Alitumaini kwamba maadui wa TANU wangeshangilia tena na kusema kuwa hiyo ilionyesha kuwa Waingereza hawakuwa na madaraka yoyote katika Tanganyika.
Wajumbe hujisemea mambo kama walevi na baadaye wakikumbushwa maneno yao wenyewe hutamani kuyakana. Jitihada ya kudai haki haiwi kazi bure; na jitihada aliyofanya Mwalimu Nyerere na wenzake katika Baraza la Kutunga Sheria ilileta mazao yake baadaye, hata kama hayakuonekana wakati huo.
Mwalimu Nyerere alijiuzulu katika Baraza la Kutunga Sheria siku ya Ijumaa, tarehe 14/12/1957. Alisema kwamba wajibu wake na wenzake ulikuwa ni kuendelea na jitihada yao na kuzidi kuwapa nguvu wenzao waliokuwa katika Baraza la Kutunga Sheria.
Kuzima koleo si mwisho wa uhunzi. Uamuzi wa TANU kukubali uchaguzi wa kura tatu katika mkutano wa Tabora 1958
Akifungua Mkutano Mkuu wa TANU uliofanyika mjini Tabora, Mwalimu J.K. Nyerere, aliwaomba wajumbe wapatao 300 ambao walitoka Tanganyika nzima wamchague mwenyekiti wa muda. M. M. Kihere, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Tanga alichaguliwa kuendesha mkutano.
Mkutano ulianza siku ya Jumanne tarehe 21/1/1958, saa tatu asubuhi katika ukumbi wa Parokia ya Kanisa Katoliki, Tabora. Huu ulikuwa ni mkutano mkuu wa mwaka 1957, ingawa ulifanyika mwaka 1958.
Mwalimu Nyerere aliwaeleza wajumbe kwa kirefu kuhusu safari zake za UNO kwa ujumla na uongozi wa TANU, Tanganyika 1957. Pia aliwaomba wajumbe wafikirie sana na watoe maoni yao kwa busara na kuwaonya kwa kusema:-
“Mkutano huu ni mkubwa na wa maana, kwa hiyo yatakayojadiliwa na kupitishwa ndiyo yatakayobadilisha maendeleo makubwa ya Tanganyika.”
Itafaa kwanza, kuelewa hali iliyokuwapo katika nchi wakati huo ili kufahamu mashaka waliyokuwa nayo wajumbe wa mkutano huo.
Kwanza, miaka michache ya nyuma serikali ya kikoloni ilikuwa imeanzisha serikali za mitaa za mseto. TANU ilikuwa imeshakwisha kushambulia sana utaratibu huo wa serikali za mitaa mpaka ukachukiwa na wananchi kiasi cha kufanya serikali za kikoloni zishindwe kuziendesha vema serikali hizo.
Pili, ilikwisha kujulikana kuwa Kenya ilipangiwa katiba isiyoridhisha na wanasiasa walipinga na walikataa kushirikiana katika uchaguzi chini ya katiba hiyo. Viongozi hao walisifiwa na wananchi wengi wa Kenya na Tanganyika, lakini hawakuingia katika Baraza la Kutunga Sheria (Legico), wala hawakuwa katika serikali, wakabaki wanapinga nje tu.
Tatu, katiba mbaya ilikuwa imekataliwa na kupingwa na wanasiasa wa Rhodesia ya Kaskazini. Hivyo mtindo wa kukataa katiba mbaya ulikuwa umeshaingia katika sehemu hizi za Afrika.
Nne, kwakutumwa au kwa hiari, wakati huo huo wa mkutano, Dar es Salaam kulianzishwa Chama cha African National Congress ambacho kilidai kuwa Tanganyika ilikuwa ni nchi ya Waafrika pekee na kwamba TANU ilikuwa na siasa ya kuacha kuwatenga wasio Waafrika, hivyo ilikuwa haifai haki juu ya uananchi wa Kiafrika.
Mwisho, ni kuhusu siasa ya Chama cha Tanganyika United Party (U.T.P.).