Wiki mbili zilizopita niliandika juu ya Kitabu alichoandika Rais (mstaafu), Benjamin Mkapa kiitwacho “Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais Mtanzania Akumbuka.”
Nilijadili mada ya ununuzi wa nyumba/jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia. Niligusia maelezo ya Rais Mkapa aliyekwenda mahakamani kutoa ushahidi kumtetea Balozi Prof. Costa Mahalu kwa uamuzi huu alioufanya wa kulipia nyumba kwa njia ya kukwepa kodi. Mkapa akasema bayana mahakamani kuwa aliufahamu mpango huo, hivyo kesi ikaisha kwa sababu Prof. Mahalu alifanya ununuzi huo kwa njia ya kukwepa kodi kwa baraka za rais aliyekuwa madarakani, Benjamin Mkapa.
Sitanii, kwa tafsiri isiyo rasmi, Mkapa katika kitabu chake Uk. wa 204 na 205 anasema: “Hivyo, ununuzi ulifanywa kwa malipo mara mbili tofauti, ingawa ushahidi uko wazi kuwa kiasi chote kilitoka Hazina ya Tanzania, kiasi chote kikalipwa katika akaunti ya Ubalozi (wa Tanzania nchini Italia), ambako ziligawanywa na kulipwa katika akaunti ya benki Italia na Monaco (Ufaransa).” Alisisitiza kuwa alifahamu kila kitu na aliruhusu.
Binafsi sina tatizo na Prof. Mahalu. Nafahamu ni mwanasheria mzuri tu, lakini wakati anafanya ununuzi huu, alikuwa amevaa joho la siasa. Alikuwa Balozi, hivyo alipokea maelekezo kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje (wakati huo), Jakaya Kikwete, hapana shaka Kikwete naye alikuwa amepokea maelekezo ya Mkapa (kama alivyokiri yeye), hivyo serikali yetu ikafanya ununuzi wa nyumba hiyo kwa kukwepa kodi.
Sitanii, ni bahati mbaya kuwa katika kitabu hiki, Mkapa amejisifia kwa kiwango kikubwa utadhani ni binadamu aliyetokea mwezini. Anaona viongozi wa sasa wanakosea katika kufanya uteuzi, anaona wanasiasa wanahemea posho bungeni, anasema waandishi wa habari wa Tanzania hataki kuzungumza nao kwani hawana maarifa ya kutosha na mengine mengi ya kujikweza. Mimi ninasema kwa uhakika kabisa, ninaelewa kwa nini Mkapa anawapenda waandishi wa nje. Hawa waandishi wa nje wanamuuliza maswali yanayotokana na ripoti za Benki ya Dunia, na si kilichopo ardhini. Tim Sebastian wa BBC (Hard Talk) alijaribu kumuuliza maswali halisi, akakiri kuwa amechukua!
Vyombo vya habari vya ndani anavichukia kwa kuhoji Kampuni ya ANBEN ilivyopata Kiwira, vya nje haviyajui haya. Tena anatumia maneno makali kwenye kitabu chake kuwa ni “upuuzi mtupu”. Kwa bahati mbaya, sisi waandishi wa Tanzania anaosema hatuna uelewa tunabaini kuwa katika ukurasa wa 201 wa kitabu hiki, amekiri kuwa baba mkwe wake alibinafsishiwa Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira. Anasema aliuliza iwapo alikuwapo mshindani mwingine aliyetaka kubinafsishiwa mgodi huo, akaelezwa kuwa hakuwapo, kisha akajiambia: “Sitazuia ubinafsishaji (wa Mgodi wa Kiwira) kwa sababu ‘mnunuzi’ ni baba mkwe wangu; hili si tatizo langu. Ikiwa haya ndiyo mapendekezo ya kiuchumi, ambayo serikali itapata (faida), basi ni sahihi.”
Mzee Mkapa anataja tukio jingine lililomuumiza kuwa ni kuambiwa shemeji yake alihusika kuwaleta NetGroup Solutions nchini. Katika Uk. 202, anasema: “Jambo jingine lenye kuumiza ni tuhuma zisizo za haki zilizotolewa wakati shemeji yangu alipohusika katika utafutaji wa kampuni ya kuendesha TANESCO… alikuwa anajihusisha na Kampuni ya NetGroup Solutions Ltd, jambo ambalo sikulifahamu wakati huo, na wala hata sasa sijui alipata nini kutokana na kazi yake kwao.” Kama rais wa nchi, ninasema alipaswa kufahamu kila jambo katika tukio kubwa kama hili.
Sitanii, matukio haya mawili yanaacha maswali mengi. Mzee Mkapa alipaswa kuwa mkweli zaidi. Hili la Kiwira anafahamu na kueleza jinsi baba mkwe wake alivyokwenda hadi India na China kutafuta teknolojia ya kuukarabati mgodi huo kuzalisha megawati 200. Shemeji yake hajui alilipwa nini. Inasikitisha!
Kimsingi, nimeandika makala hii kueleza kuwa viongozi wetu wanapokuwa madarakani, wazisome sheria sawa sawa. Kwamba matukio ya kununua nyumba, Kiwira na TANESCO, yakichunguzwa na ikabainika uzembe, rais aliyefanya uamuzi huu anaweza kushitakiwa kwa mujibu wa sheria. Tanzania inafuata mfumo wa sheria wa Waingereza (Common Law Legal System). Mfumo huu umeweka misingi na njia tatu za kutafsiri sheria, ambazo ni tafsiri ya moja kwa moja (literal interpretation rule), tafsiri ya kutafuta maana (golden interpretation rule) na tafsiri ya nia ya watunga sheria (mischief interpretation rule).
Kwamba Ibara ya 46 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema mtu akiwa Rais hatashitakiwa kwa jambo lolote la madai au jinai alilolifanya akiwa madarakani, ni sahihi katika literal translation. Hata hivyo, tunapaswa kuiangalia iwapo nia ya watunga sheria walilenga kumkinga Rais na jinai za makusudi kama ukwepaji kodi, upendeleo kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki… sitaki kuamini hivyo. Mahakama ikitafsiri Katiba kwa kutumia mischief interpretation rule, tutapata majibu tofauti katika hili. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania. Heri ya Mwaka Mpya 2020.