Deni la nje la taifa ambalo linahusisha deni la serikali na deni la sekta binafsi, lilikua na kufikia dola milioni 22,569.4 za Marekani ilipofika mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, Benki Kuu (BoT) imeeleza.
Taarifa ya Uchumi kwa Mwezi iliyotolewa na BoT mwezi uliopita inaeleza kuwa deni hilo liliongezeka kwa dola milioni 188.7 za Marekani na dola milioni 1,879.3 za Marekani kutoka katika deni lililorekodiwa mwezi uliotangulia na mwaka uliopita mtawalia.
Hali ya mwezi kwa mwezi ya deni hilo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya BoT, inatokana na madeni mapya na kushuka kwa thamani ya dola ya Marekani dhidi ya sarafu nyingine duniani ambazo zinatumika kukopa.
Kama ilivyo ada, deni la Serikali Kuu ndilo lilikuwa sehemu kubwa ya deni hilo la taifa, likiwa ni asilimia 77 ya deni lote, BoT imesema.
Kwa upande wake, sekta binafsi ilikuwa na deni lililofikia dola milioni 5,029.2 za Marekani, sawa na asilimia 22.3 ya deni lote huku mashirika yakiwa na deni la dola milioni 165.2 za Marekani sawa na asilimia 0.7 ya deni lote.
Wakopeshaji na wadai wakubwa waliendelea kuwa wale wale ambao ni mashirika ya kimataifa ambayo yalikuwa na asilimia 44.7 ya deni lote huku vyanzo vya kibiashara vikifuatia kwa kukopesha kiasi kikubwa kwa taifa.
Uchanganuzi wa wakopeshaji unaonyesha kuwa deni kutoka nchi nyingine ni kiasi cha dola milioni 1,960.6 za Marekani sawa na asilimia 8.7 huku deni kutoka vyanzo vya kibiashara likifikia dola milioni 8,129.2 za Marekani sawa na asilimia 36 huku mpango wa kuwakopesha waagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi ukiwa na deni la dola milioni 2,392.7 za Marekani.
Kwa upande mwingine, taarifa hiyo inaonyesha kuwa sekta za usafiri na mawasiliano ya simu zilipokea sehemu kubwa ya deni hilo kwa asilimia 26.8 zikifuatiwa na ustawi wa jamii na elimu, nishati na madini na mfuko mkuu wa serikali wa bajeti.
Kuhusu madeni mapya, taarifa ya BoT inasema kuwa mwezi Oktoba kiasi cha dola milioni 49.9 za Marekani zilipokewa na Serikali Kuu kama deni jipya.
Katika kipindi cha mwaka ulioishia Oktoba 2019, BoT inaeleza, deni jipya lilikuwa kiasi cha dola milioni 2,272.7 za Marekani, ambapo dola milioni 2,106.3 za Marekani zilikopwa na Serikali Kuu na kiasi kilichosalia kilikwenda kwa sekta binafsi.
Kwa upande wa malipo, BoT inaeleza kuwa mwezi Oktoba, kiasi cha dola milioni 37.4 za Marekani zilitumika kulipa deni la nje ambapo dola milioni 23.8 za Marekani zililipwa kama deni kuu huku kiasi kilichosalia kikiwa ni riba inayotokana na madeni hayo.
Katika mwaka ulioishia Oktoba 2019, malipo ya deni la nje yalifikia dola milioni 1,333.6 za Marekani ambapo dola milioni 1,026.2 za Marekani zilikuwa ni deni kuu.
Deni la ndani
Kwa upande wa deni la ndani, BoT inasema nalo liliongezeka kwa Sh bilioni 126.6 kutoka kiwango kilichokuwepo mwezi uliotangulia na Sh bilioni 71.3 na kufikia Sh bilioni 14,187.4 kulinganisha na deni lilivyokuwa mwezi Oktoba 2018.
Kwa mujibu wa BoT, ongezeko hilo lilitokana na kiwango cha mikopo mipya kuzidi kasi ya malipo ya deni hilo.
Hata hivyo, BoT inasema kuwa kukua huko kwa deni kunaendana na mkakati wa muda wa kati wa serikali wa kudhibiti madeni.
Madeni ya muda mrefu, ambayo yanahusisha dhamana za serikali yalikuwa ni asilimia 79.5 ya deni lote mwishoni mwa Oktoba, kwa mujibu wa BoT.
Benki ndizo zilikuwa mkopeshaji mkubwa kwa serikali, zikiwa na asilimia 37.6 ya deni lote, zikifuatiwa na mifuko ya pensheni ambayo deni lake lilikuwa ni asilimia 29.1 ya deni lote.