Ndugu Rais, leo tunaufunga mwaka 2019 kama unafungika. Na kesho tunaufungua mwaka 2020 kama utafunguka. Wanaosema ni mwaka mpya, watuonyeshe basi upya wake. Siku ni zilezile hazibadiliki. Wiki ni zilezile wala hazina maboresho. 





Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishuhudia uzinduzi wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mkoani Kilimanjaro mapema mwaka huu kama sehemu ya maandalizi ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwakani.

Miezi nayo inabaki ileile kumi na miwili lakini yenyewe imepewa majina. Tumeanza na Januari na kumaliza na Desemba tangu ujana wetu na hata sasa katika kuzeeka kwetu. Tunapoingia siku nyingine au wiki nyingine hata mwezi unaofuata, hawasemi tunaingia mwezi mpya. Tumekuwa na mzunguko huu tangu kuzaliwa kwetu, kukua kwetu na sasa mpaka kufa kwetu. Upya wa mwaka unatoka wapi wapendwa?

Baba, Rais wangu katika uelewa huu, naomba kwa unyenyekevu mkubwa, ikupendeze tu kujua kuwa sitakutakia heri ya mwaka mpya kwa kuwa haupo! Mwaka 2020 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu, hivyo tunahitaji busara zaidi kuliko nguvu za misuli yetu, iwe ya mikono au miguu yetu hata nyonga. 

Mazoezi ya akili yanajulikana. Chapisha machapisho. Andika vitabu au makala za kulifundisha taifa. Kukimbia au mazoezi ya ngumi ni sawa; lakini jiulize taifa linafaidika nini kwa mazoezi hayo?

Tunapoufunga mwaka wale ambao wanayatafuta madaraka hata kwa nguvu na wale ambao wanayatetea madaraka yao hata kwa nguvu, lazima waelewe kuwa wananchi wanaposema wanataka mabadiliko si mabwege wa kuwatoa waheshimiwa wa upande huu na kuwaweka waheshimiwa wa upande mwingine.

Ieleweke kuwa mwaka 2020 hakuna mheshimiwa atakayechaguliwa na timamu. Nani anamtaka mtu asiye na adabu kiasi cha kujiita mheshimiwa mbele ya mwajiri wake? Waheshimiwa ni wananchi na ndio waajiri. Wote wa pande zote, vueni fikra zenu chakavu za kujivika utukufu. Watakubalika walio tayari kuwa watumishi wao.

Mheshimiwa wa kweli hatumikii, anatumikiwa! Wakubwa wapo kwa sababu wadogo wapo. Hakuwezi kuwapo waheshimiwa bila kuwapo watwana. Hapa watwana ni nani kama si wananchi?

Katibu Mkuu aliyepita, Komredi Abdulrahman Kinana, katika utumishi wake wote aliwataka viongozi wenzake wajivue utukufu. Wasijiite waheshimiwa, kwa kuwa hawastahili. Lakini kwa wasaka tonge hili lilikuwa gumu kukubalika mpaka alipojiuzulu. Leo mtu muhimu huyu anadhalilishwa na kutukanwa na vijana wadogo wasio na thamani yoyote katika taifa hili. Tukumbuke kuwa kiongozi mnyofu kama Nyerere alikubali kuitwa ndugu, sisi tukikubali kuitwa hivyo tutababuka ngozi?

Mtakatifu wa kweli ni sawa na mzalendo wa kweli. Watu hawa huwa hawajijui katika jamii kuwa ni watakatifu au ni wazalendo. Wengine au jamii wanamoishi ndio wanawajua kuwa huyu ni mtakatifu au huyu ni mzalendo. Anayekujia mwenyewe akiwa na macho makavu na kukwambia kuwa yeye ni mzalendo, mhesabu katika kundi la watu chizi au wendawazimu!

Ndugu Julius Kambarage Nyerere hakuwa malaika, bali aliukataa uheshimiwa akawatumikia Watanzania na watu wengine wa mataifa kama mtumishi wao. Alikuwa mzalendo wa kwelikweli mtu yule, lakini hakuna popote alipojitangaza mwenyewe kuwa ni mzalendo. Lakini leo watu wema ndio wanahangaika atangazwe kuwa ni mtakatifu.

Aliyeamuru bendera za Chadema zishushwe mimi simjui. Timamu wote waliofuatilia mkutano mkuu wa Chadema wanasema Mwenyezi Mungu anaweza akakuumba na kichwa kikubwa lakini akasahau kukuwekea vitendea kazi muhimu kama busara ndani yake. Busara ilikosekana.

Hawa ndio baadhi ya viongozi wetu ambao kwa mawazo yao ya kitoto wanazichafua busara njema za walio juu yao. Kama zilishushwa au hazikushushwa kulikuwa na faida gani au hasara gani kwa taifa?

Kutekeleza amri ile ilikuwa ni kufanya kazi ileile inayofanywa na mbwa wa polisi. Haulizi kuna kosa gani. Mwanadamu kufanya kazi kama mbwa ni kumkosea Mwenyezi Mungu aliyekupa akili na busara ili kabla ya kutenda ufikiri, uchambue na utafakari.

Urais aliouacha Julius Kambarage Nyerere, ni uleule aliouacha Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa, Jakaya Mrisho Kikwete na sasa uko kwetu. Urais na mtu ni vitu viwili tofauti. Mtu ndiye anayeweza kuwa rais bora au rais katili.

Mzee Malecela alisema kazi ya urais si kubeba zege. Wanaofikiri sawasawa nao wakasema, si urais peke yake, bali kazi yoyote unayoifanya, ukiiona ni ngumu sana tambua unaikosea. Unavyoifanya sivyo. Unamfukuza jogoo. Ukifaulu kumpata jogoo atakuwa nyakanyaka anachuruzika damu na wewe pia utakuwa nyakanyaka unachuruzika damu. Duniani hakuna kazi ngumu.

Kwa kuwa wapo waliokamia kuwa ni mwaka wa liwalo na liwe, wenye mamlaka wasipoitambua shari hii, wakafanya maridhiano kungali mapema watakapokuja kupata fahamu baadaye kuwa kumbe ilikuwa ni kwa hasara yao wenyewe watajikuta wamechelewa! Laiti ingekuwa ni amri ya mtu fulani tungeamua tusiufunge kwanza mwaka 2019 mpaka kwanza tufanye maridhiano. Mwisho wa walioshindwa huwa ni maumivu, lakini mwisho wa walioshinda huwa ni mchungu zaidi kuliko shubiri!

Watanzania hawakuwahi kufikishwa katika hali ya kukamiana wenyewe kwa wenyewe kiasi hiki! Hali hii ndiyo imefanya Awamu ya Tano iwe ngumu kuzoeleka.

Awamu ya Tano Watanzania wamejikuta katika hali ya ufukara zaidi kushinda walivyokuwa katika awamu zote zilizotangulia. Kinachowatatiza fukara wengi ni pale wanapohakikishiwa na baadhi ya viongozi wao kuwa nchi ni tajiri sana. Fedha za serikali ni fedha za wananchi wote, nazo hutolewa kwa utaratibu maalumu.

Baba, kabla hatujaufunga mwaka 2019 tuyatafakari mahubiri ya viongozi wetu wa dini waliyoyatoa wakati wa Noeli. Wanasema, haki ya kuishi inapoingiliwa kinakuwa ndicho chanzo cha vurugu katika nchi. Wanasema kwa sasa malalamiko ya kuumizana na dhuluma yamekuwa mengi. Furaha ya wananchi imepotea!

Baba Gulle akihubiri alisema: “Watu wamekandamizwa sana, wamekosa thamani na kuumizwa. Yesu anapokuja anataka kukaa ndani mwetu tuwe na amani na upendo.” Ujumbe wake ni kuwapenda wengine.

Baba Askofu Shoo akasema: “Na hapa kipekee napenda kutoa ujumbe kwa wenzangu wanaohusika katika kupeleleza kesi za watu, mahakimu na majaji, simamieni ukweli. Simamieni haki!”

Akisisitiza akasema: “Watanzania hawapaswi kuwatesa wala kufurahia kuwatesa wenzao wasio na hatia!”