DODOMA

NA GREYSON MWASE

Tume ya Madini imetangaza zabuni kwa watu wanaotaka kununua maeneo 10 yenye leseni hodhi za madini yenye
ukubwa wa kilometa za mraba 381.89 katika maeneo ya Ngara — Kagera, Kahama – Shinyanga, Chunya – Mbeya,
Bariadi na Busega — Simiyu; Morogoro na Nachingwea — Lindi. Leseni hodhi za maeneo hayo zilikuwa chini ya serikali.
Uamuzi huo umetangazwa wiki iliyopita jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari ambao pia ulihudhuriwa na Kamishna wa Tume ya Madini, Dk. Athanas Macheyeki; Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya pamoja na watendaji wengine wa Tume ya Madini.
Prof. Kikula anafafanua kuwa mwaka 2017 Bunge lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Madini Namba 123 na kanuni
zake ambapo pamoja na mambo mengine, zilizokuwa leseni hodhi za madini zilirudishwa serikalini.
Anasema baada ya marekebisho hayo maeneo yote 10 yenye ukubwa wa kilomita za mraba 381.89 yalirudishwa
serikalini na kuongeza kuwa wachimbaji wa madini wengi wamekuwa wakiulizia maeneo hayo mara kwa mara lengo
likiwa ni kuomba leseni za uchimbaji madini.
Anasema baada ya uchambuzi wa kina, serikali imeamua kuyatoa maeneo yote 10 kupitia zabuni na kukaribisha
kampuni za uchimbaji wa madini na watu binafsi wenye uwezo wa fedha na utaalamu katika miradi ya uchimbaji wa
madini na wenye nia ya kuendeleza miradi ya madini ya nickel, dhahabu na rare earth elements kuchangamkia zabuni hizo.
Anaongeza kuwa mwekezaji atakayeonyesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo atakuwa na jukumu la kufanya kazi zake, pia jukumu la kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo husika.
Wakati huo huo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Prof. Manya, anawataka wamiliki na waombaji wote wa leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini wenye upungufu kurekebisha upungufu uliopo ndani ya siku 30 kuanzia sasa.
Akifafanua, anataja baadhi ya upungufu kuwa ni leseni ambazo hazifanyiwi kazi, leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango la mwaka, maombi ambayo hayajalipiwa ada ya maombi na maombi yaliyokosa viambatisho muhimu kwa mujibu wa
sheria.
Prof. Manya anataja upungufu mwingine kuwa ni waombaji waliokidhi vigezo vya kupewa leseni lakini hawajalipa ada ya
maandalizi na wamiliki ambao leseni zao zimekwisha kutolewa lakini hazijachukuliwa.
Anasema hadi sasa zaidi ya leseni 134 za utafutaji na uchimbaji wa kati wa madini hazijachukuliwa na zaidi ya
maombi 450 ya leseni za utafutaji yana upungufu.
Akielezea hatua zitakazochukuliwa kwa kampuni au watu binafsi walioaminiwa na serikali na kupewa leseni lakini
wameshindwa kutekeleza masharti ya leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, anasema leseni ambazo hazijalipiwa ada ya pango kwa mwaka, leseni ambazo hazifanyiwi kazi na leseni ambazo zimekwisha kutolewa lakini hazijachukuliwa
zitaandikiwa hati ya makosa na yasiporekebishwa zitafutwa kwa mujibu wa sheria.