DAR ES SALAAM

NA ANNA JULIA MWANSASU
 
Ninawashukuru wote walionipigia simu, walionitumia ujumbe mfupi na wengine kuongea nami ana kwa ana kuhusu makala yangu katika toleo lililopita la gazeti hili.
Awali ya yote, ninapenda kusema kwamba mimi si mwanasiasa, wala si mchambuzi wa mambo ya siasa, kwa kuwa uchambuzi unahitaji ujuzi na kusomea mambo ya siasa. Mimi ni mwananchi wa kawaida tu, ila nilifundishwa na Baba wa Taifa letu kuipenda nchi yetu.
Makala yangu ya kwanza kwenye Gazeti la Mzalendo Nalilia Ujamaa niliiandika mwaka 1989. Mwalimu Nyerere aliisoma na kunitia moyo niendelee kuandika.
Miongoni mwa walionitumia sms wapo walioniambia nimeandika upande mmoja tu, ilibidi niandike na upande wa pili wa shilingi. Wapo walioniambia ninakosea kumfananisha Mwalimu na Rais Magufuli na wapo waliokubaliana nami na kupongeza kazi nzuri anayofanya rais wetu.
Sms moja ilisema hivi: “Wasomaji wana maoni tofauti tofauti katika faida na hasara. Umeona faida tu. Kwa makusudi maalumu umeonyesha ni mpambe wa Rais. Wasomaji wa JAMHURI wangependa uchambuzi wa upande wa pili. Hayo uliyoandika ndivyo yalivyo. Hongera.”
Mwingine ameandika: “Salamu Mama Mwansasu. Katika kumuenzi hayati Baba wa Taifa (RIP) na kuyaishi maudhui mema alituasa, hususan eneo la maadili, utu na asili za binadamu wewe uliyekuwa karibu naye unanishangaza kwa kulinganisha na kinachoendelea katika taifa letu hivi sasa, kinyume kabisa na matunda ya Uhuru aliyoyapigania na wenzake. Mkakati mkuu wa ujenzi wa taifa lolote, msingi mkuu aliosimamia Nyerere ni utaifa, umoja, ushirikishwaji, amani na furaha… Tumepiga hatua kubwa sana kurudi nyuma kimaendeleo. Maendeleo si vitu, wala pesa si msingi kamwe. Legacy ya CCM baada ya Mwalimu kuondoka ni ya ufisadi na uporaji mkubwa wa rasilimali za umma… Mimi ni mmoja kati ya wagombea walioenguliwa eti sijui kusoma na kuandika! Au mtu kuwa chama tofauti na CCM ni uhaini?”
Natangulia kusema kwamba madhumuni ya makala yangu haikuhusu uchambuzi wa mazuri na mabaya ya rais wetu ama hasara na faida, bali kueleza juu ya mazuri aliyoyafanya ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, ambayo kwa namna moja ama nyingine yanafanana na yale aliyoyafanya Mwalimu Nyerere kwa manufaa ya taifa letu.
Kwa msingi huo, nilidiriki kufananisha utendaji wa Rais Magufuli na Mwalimu unaotokana na wote wawili kuguswa kwa dhati na matatizo ya wananchi wanyonge na kushughulika kujenga taifa letu kwa madhumuni ya kuliletea maendeleo.
Sikufananisha sura, wajihi ama muondoko, umaarufu nk — Mwalimu ni Mwalimu na Dk. John Magufuli atabakia kuwa ni yeye, Dk. Magufuli. Pia zama za uongozi wa Mwalimu ni tofauti na zama hizi za Rais Magufuli. Nawafananisha kwa utendaji wao ulioleta matokeo chanya.
Kuhusu “kuyaishi maudhui mema kwenye eneo la maadili, utu, na asili za kibinadamu.” Mimi pia ninashangaa, ambaye hana maadili na hana utu ni nani? Makala yangu ilikuwa ni juu ya rais wetu, kama maneno hayo yanamlenga rais, angekuwa hana maadili na hana utu angeliweza kufanya haya yote anayoyafanya kujenga nchi?
Yote haya anayofanya rais ya kutumbua, kukemea na kuwadhibiti wale wanaoiba rasilimali za nchi yetu na washirika wao yana lengo gani kama si kujenga maadili na uwajibikaji?
Kuwajali wanyonge wa nchi hii, kuwasaidia na kuhakikisha wana mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao ili wajitafutie maendeleo yao. Huo si utu?
Mtuma sms mwingine anasema: “Mkakati mkuu wa ujenzi wa taifa lolote, msingi mkuu aliosimamia Nyerere ni utaifa, umoja, ushirikishwaji, amani na furaha….” Ni utaifa upi, umoja upi, ushirikishwaji upi, amani ipi na furaha gani? 
Katika haya yote ni kipi kinachokosekana nchini mwetu? Kwa maoni yangu, Watanzania tunapaswa kuwa waangalifu sana katika kuzungumzia mambo yanayohusu mustakabali wa taifa letu. Wapo watu ambao wakati mwingine wanadiriki kusema kwamba “damu itamwagika”! Hawa wanajua kweli maana ya damu kumwagika nchini? Wanapoyasema hayo ni kwa sababu ya tofauti ndogo ndogo tu za kisiasa.
Pengine ifike mahali walio kwenye vyama vya upinzani waelewe kwamba wao wana mapungufu ambayo wanahitajika kuyafanyia kazi.
Upungufu mmoja ni kutotaka kuungana ili waweze kukikaribia Chama Cha Mapinduzi kwa ukubwa. Chama Cha Mapinduzi kina wanachama wengi na mtandao mkubwa uliojengeka kutokana na historia yake, kwa hiyo kuweza kukishinda chama hiki lazima vyama vya upinzani waungane. Wakibaki walivyo, wataendelea kutafuta mchawi kwa kushindwa kwao na kuwajengea wafuasi wao (ambao wengi wao hawana uelewa na upeo mkubwa wa mambo) mawazo kwamba wanahujumiwa!
Pili, tukichukulia Chadema, ambacho kinajipambanua kuwa ndicho mshindani mkuu wa CCM, umaarufu wake unashuka.
Kabla ya uchaguzi wa mwaka 2015 matumaini waliyoyapata kwamba wanaweza kuipiku CCM, yalitokana na makosa ya kiufundi yaliyofanywa na CCM, ya kukiuka misingi iliyojengwa na waasisi wa chama hicho chini ya uongozi wa hayati Mwalimu Nyerere na hayati mzee Abeid Amani Karume.
Halikadhalika, ongezeko la wabunge wa Chadema kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 lilitokana pia na makosa yaleyale ya kiufundi ya CCM ya kukumbatia mitandao mpaka Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa akatoka CCM na kujiunga na Chadema.
Alipofika huko wakaona wameokota almasi. Wakamchagua kuwa mgombea wao wa urais, akakiongezea chama hicho nguvu na umaarufu.
Mwisho wa yote, CCM ikashinda. Rais Magufuli akashika usukani wa kuiongoza nchi kwa umahiri ambao haukutegemewa. Lowassa akaamua kurudi nyumbani. Wabunge, madiwani, wanachama na wananchi walioihama CCM, ambao huko nyuma walikichukia Chama Cha Mapinduzi kwa kukiuka misingi yake wakarudi. Nyumbani CCM kukanoga zaidi!
Kwa muktadha huo, kwa maoni yangu, hata kama Chadema na vyama vingine vikiachiwa vifanye mikutano ya hadhara kila uchao hawataweza kuishinda CCM. Isitoshe, kuachiwa kufanya mikutano kiholela na maudhui ya mikutano hiyo ingekuwa ni kutafuta mambo madogo madogo, kuyakuza na kuyafanya kuwa kipingamizi cha Hapa Kazi tu! Yangekuwa ni mambo yaleyale, rais anataka kujenga bwawa la umeme litakalokuwa na manufaa katika kujenga uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla. Upinzani, kwa kutafuta umaarufu ama kutaka waonekane ni wapinzani, wangeitisha mikutano ya hadhara kuwachanganya wananchi wasiojua mambo, kwa kuwaambia wazo hilo si zuri, bwawa lisijengwe maana wakubwa (mafundi wa kuingilia uhuru wa kujiamulia mambo yetu) wanasema tunapaswa kuzuia uharibifu wa mazingira!
Bila shaka, moja ya mambo ya upande wa pili niliyotakiwa kuyasema ni madai ya uminywaji wa demokrasia, kwa sababu hiyo ya vyama kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara nk. Mataifa makubwa ambayo yanajipambanua kwamba ndio magwiji wa demokrasia na ambao tunaambiwa tuwaige, hawadai mikutano ya hadhara wala kuandamana. Marekani wana vyama vikubwa viwili — Republican na Democrats. Wao wakati wa kampeni za chaguzi zao wanafanya mikutano ya hadhara ya nguvu.
Uchaguzi ukiisha wanaendelea na shughuli zao za kujitafutia na kuimarisha utajiri wao.
Inashangaza kuona vyama vya nchi maskini, nchi ya dunia ya tatu inayotakiwa kukimbia wakati nchi zilizoendelea zinatembea, wanataka waruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara itakayowashirikisha wananchi ambao wanapaswa kuchakarika kwa bidii sana ili wajiletee maendeleo yao.
Nakuja kwenye alilosema mtuma ujumbe kwamba: “Maendeleo si vitu, wala pesa si msingi kamwe.”  Huyu anajaribu kumnukuu Mwalimu aliyosema kuhusu maendeleo, na bila shaka alikuwa ananiambia kwamba anayofanya rais wetu ni maendeleo ya vitu, pia rais anaweka mbele pesa!
Turudi kwenye mambo aliyofanya Mwalimu kwa taifa letu, ambayo yanafanana na anayofanya Rais Magufuli.
Mwalimu alipokuwa akijenga vyuo, shule na kutoa elimu bure alikuwa analenga katika kuleta maendeleo ya watu; alipojenga reli, barabara, alipoanzisha Shirika la ATC alikuwa analenga kuwarahisishia na kuwapatia Watanzania wake usafiri wa uhakika na kuleta maendeleo.
Alipojenga viwanda alikuwa analenga kuwaletea wananchi maendeleo kwa vijana kupata ajira, n.k.
Mwalimu Nyerere hata alipotoka madarakani, aliposema amefuatwa na wafanyabiashara nchini waliomtaka aiambie serikali ikusanye kodi; akalalamika kwamba serikali corrupt zinazoendekeza rushwa ndizo hazikusanyi kodi, alikuwa analenga maendeleo ya nchi, kodi zikusanywe ipasavyo zilete maendeleo ya watu.
Mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni! Inakuwaje sasa Rais Magufuli anafanya yaleyale aliyoyafanya Mwalimu analaumiwa kwamba anakazania maendeleo ya vitu na si watu? Rais anajitahidi kwelikweli kukusanya kodi. Akikusanya, hachoti akazitia mfukoni mwake ama mfukoni kwa Mama Janet, ama mifukoni mwa ndugu na marafiki zake.
Pesa za kodi hizo zimetumika kujenga mambo chungu nzima kwa kipindi kifupi sana. Ukiacha Awamu ya Kwanza ya miaka 24 ya uongozi wa Mwalimu, aliyofanya Rais Magufuli ndani ya miaka minne ya Awamu ya Tano hayajawahi kufanywa na awamu yoyote ile nyingine.
Niliwahi kuandika makala nikauliza: “Mwalimu angekuwapo angesemaje kuhusu utendaji wa Rais Magufuli?” Hakuna aliyenijibu swali hilo, kwa sababu wanajua kabisa kwamba angempongeza sana rais wetu! Mwalimu angekuwa mshauri wake mkubwa na Rais Magufuli angejisikia raha sana kushauriwa na kukubali ushauri wa Mwalimu, kwa kujua unatolewa kwa nia njema kabisa na si kwa unafiki!
Kuhusu aliyosema mwandishi wa sms: “Mimi ni mmoja kati ya wagombea walioenguliwa eti sijui kusoma na kuandika! Au mtu kuwa chama tofauti na CCM ni uhaini?” 
Kwa maoni yangu, kama mambo ya aina hii yalifanyika kwa makusudi ya kuwaminya washindani wengine, hili ni kosa jingine la kiufundi la watendaji wasiojua wajibu wao.
Pia kama ni mbinu za kuitafutia CCM ushindi, ni mbinu potofu. Kama yalikuwapo maeneo ambayo CCM ilitaka wayapate, hawakupaswa kusubiri kuwaengua watu kwa hila. Kazi nzuri aliyofanya na anayoendelea kuifanya Rais Magufuli inatosha, inarahisisha sana kazi ya kuwahamasisha wapiga kura kuwachagua wagombea wa Chama Cha Mapinduzi.
Pamoja na hayo, CCM bado ina kazi ya kufika mpaka kwenye matawi – chini waliko wananchi wa kawaida kuwahamasisha. Ninasema hivyo kwa sababu ninaishi wanakoishi wanyonge wa Jiji la Dar es Salaam.
Ni zaidi ya miaka saba sasa sijaona kiongozi yeyote wa CCM wa ngazi yoyote ile anapitapita kuwajua wanachama na kuwahamasisha. Bila shaka wanataka wafuatwe ofisini. Wajumbe wa Nyumba Kumi wanaonekana kwenye uuzaji wa maeneo!
Mikutano ya hadhara si lazima, viongozi inabidi wajiongeze. Hata kuwatembelea wanachama waelewe kuna kiongozi, ni hamasa ya kutosha.
Pia, kuna wanaosema kwamba rais hapaswi kuwafokea watendaji hadharani, kwa mfano anapokuwa kwenye ziara mikoani. Rais anayehimiza uwajibikaji, anakwenda sehemu anakutana na wananchi wenye mabango na kero zao ambazo zingeweza kabisa kushughulikiwa na kutatuliwa na watendaji hao.
Afanyeje? Achekecheke tu na kuwaambia wananchi asanteni kwa kero zenu, tulieni nikifika Ikulu ndogo nilikofikia nitamwita mhusika tushauriane! Wananchi watamshangaa! Wanaodai sasa kwamba asikemee na kutumbua hadharani watamshikia bango na kusema rais gani huyu hata hakemei watendaji wabovu! Tukumbuke kwamba rais ni Amiri Jeshi Mkuu!
Yapo mengine ya upande wa pili yanayosemwa mitaani. Mengi ni yale yasiyo na ukweli ama ni nusu ukweli, ambayo yanapikwa na kupelekwa mitaani bila ushahidi wowote. Wananchi wasio na uelewa wa mambo wanayapokea na kuyashabikia wakidhani ndio ukweli wenyewe.
Mengine yanayozungumzwa mitaani yanahusu utumbuaji na kamatakamata ya mafisadi n.k. Kwanza tunapaswa tuangalie tulikotoka na tulipo. Huko nyuma, wenye pesa, wenye vyeo ama hadhi fulani walikuwa hawaguswi, hata wafanye kosa gani watatumia fedha zao kutoa rushwa wasikamatwe, watatumia vyeo vyao kuwatishia wanaohusika kuchukua hatua n.k. Kwa hiyo waliokuwa wanakwenda kuwa wapangaji magerezani walikuwa watu wa kawaida tu wasio na uwezo wowote. Hivi sasa kila mtu ni mfungwa mtarajiwa! Wapo ambao hawataki hilo.
Kuna kesi zinazowakabili wanasiasa ambazo zipo mahakamani, tunajua chochote kikifika mahakamani tunapaswa kuiachia mahakama ifanye kazi yake.
Lipo jingine la wasomi wa nchi yetu kujifanya wanayajua sana matatizo ya nchi yetu wakati wao wako mijini wakiendesha magari (vitu), wakikaa kwenye ofisi za viyoyozi, wakila milo mitatu kwa siku na kuteremshia mivinyo. Hawajali kujua yanayowasibu wanyonge wa nchi hii na shida zao na wala hawawahurumii.
Kazi yao wao ni kuingia mitandaoni, wanaogelea kwenye kurasa za lugha ya Kiingereza zinazoelezea juu ya haki za binadamu, demokrasia, Rais Trump anafanya nini, anasema nini n.k.
Wakitoka hapo wanataka Tanzania ifanye hivyo hivyo!
Mwalimu Nyerere na wenziwe walipigania Uhuru wa nini mpaka tuamuliwe mambo au tutake kufanya kama ya wengine?
Wasomi haohao wapo wanaosema kwamba kwa nini Kiswahili kipewe kipaumbele na kuhamasishwa kisambae na kwingineko. Hawaoni sababu! Huko nyuma walikuwepo wasomi watoto wa wakulima na wafugaji waliojiona kwamba wao wamekuwa tofauti na vijana wenzao wasiosoma, wakaandamana kukataa kwenda JKT, wakaitusi Serikali ya Mwalimu Nyerere wakadai Afadhali wakati wa mkoloni, mkoloni ambaye hakuchukua hatua zozote za kuelimisha wananchi! Hiyo ndiyo hulka ya baadhi ya wasomi nchini!
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alituasa kwamba tuwe tunachukua mazuri, mabaya tuyaache. Pia alisema na kuandika kijitabu — Tujisahihishe!
Ninafurahi sana kuambiwa ni mpambe wa Rais! Ni cheo kikubwa na kizuri sana. Lakini siko peke yangu, wapo wapambe wengine wengi sana ambao wanaona mazuri ambayo anafanya rais wetu na wanamsifu na kumpongeza sana.
Yupo mpambe mwenzangu aliyenitumia sms akisema: “Asante kwa kuandika. Kazi nzuri unaifanya. Viongozi waliopita wamekuwa na tabia ya kulaumu kuhusu ukosefu wa ajira nchini, n.k. Niseme tu waache Rais Magufuli afanye kazi ya kufufua uchumi. Mwalimu alijenga viwanda karibu kila mkoa, kulikuwa hakuna tatizo la ajira. Darasa la saba, kidato cha nne na sita wote waliajiriwa. Baada ya Mwalimu kuondoka waliuza viwanda vyote. Wao ndio chanzo cha ukosefu wa ajira…Mtazamo wangu ni kwamba elimu bure na kwenda JKT ndiyo nguzo iliyofuta matabaka nchini. Mimi ninatoka kwenye familia maskini kweli, kama si elimu bure ya Mwalimu Nyerere ningekuwa maskini na fukara kweli. Lakini niliweza kusoma shule moja na mtoto wa Mwalimu, Madaraka… Dada endelea kuandika. Sisi maskini wote tuko nyuma ya Jemadari wetu JPM — MAN OF THE PEOPLE (Mtu wa Watu).”
Naam! Nchi nyingine wanasema tutampata lini Rais kama Magufuli! Kwa msingi huo, sipati kigugumizi chochote kumwambia tena: RAIS WETU USIOGOPE, TEMBEA KIFUA MBELE!
 
Anna Julia Mwansasu ni Katibu Muhtasi mstaafu wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Anapatikana kwa simu 0655774967.

Mwisho