Nilimalizia waraka wangu wa wiki iliyopita nikielezea jinsi nilivyomuona Mwalimu akiwa amechoka katika mapambano ya kuliongoza taifa.
Alichoka kwa kulipitisha taifa katika mambo mengi, lakini hapa kuna sababu kubwa ambayo ningependa Watanzania waijue vizuri.
Wakati taifa hili likipata Uhuru, wasomi wenye digrii walikuwa wachache sana na bila kupepesa macho walikuwa na fikra zao nyingi tofauti. Walikuwepo waliokuwa na mrengo wa kushoto na wale wa mrengo mwingine.
Kiufupi, wasomi wetu wengi wao walikuwa na matumaini makubwa na walikuwa wataalamu wa kupinga mambo mengi kwa hoja.
Ikumbukwe taifa letu lilikuwa na uhaba mkubwa wa wasomi kiasi kwamba wengi waliomaliza darasa la nne wakati huo walikuwa na ajira ya moja kwa moja katika utumishi wa umma, lengo likiwa ni kusaidia taifa katika kuchukua ajira ambazo zilikuwa mikononi mwa Wazungu. Hapa Mwalimu alijenga imani sana kwa vijana waliomaliza shule za awali na kuwapa majukumu.
Vijana hawa ndio waliolishika taifa hili kwa kipindi cha mpito wakati tukitayarisha wataalamu na wanazuoni ambao baadaye walianza kupachikwa kidogo kidogo katika maeneo muhimu kwa mustakabali wa taifa letu. Ni kipindi ambacho Mwalimu alikuwa na wakati mgumu sana kufuatilia mambo ya kila siku katika maeneo mengi.
Kipindi hiki kulikuwa hakuna kujinadi kwa elimu bali kulikuwa na kujinadi kwa misingi ya unawajibika vipi katika nafasi yako na kwa faida ya watu wengine wanaokuzunguka. Ninakumbuka kama ambavyo nilijitanabaisha mara ya kwanza kwamba nilipata nafasi ya kulitumikia taifa langu kama mtumishi katika nafasi mbalimbali.
Nilizungumzia nafasi nilizotumikia katika taifa langu lakini kikubwa ambacho ningependa leo kiwe wazi ni jinsi ambavyo katika utumishi wangu niliweza kutoka katika kijiji changu na kwenda kuishi katika eneo jingine bila kujijua na kuanza kuwa familia yangu.
Haya hayakutokea kwa bahati mbaya, kwani yalikuwa ni maagizo kutoka kwa baadhi ya watu ambao labda leo tungewaita hawakusoma na hatukupaswa kuwasikiliza kwa mujibu wa dhana tulizonazo vichwani leo.
Ni katika kipindi cha hamahama ndipo nilipojikuta nikianza kuwa na mke kutoka eneo jipya, na kutokana na ndoa nikajikuta ninaamua kuishi mahali pengine tofauti na nilipozaliwa. Ni kwa kupitia kazi nikajiona ninastaafu nikiwa Kipatimo ilhali kwetu ni zoni nyingine.
Katika maisha yangu nilijua kwamba kuna siku nitaamua kurudi kwetu lakini kutokana na malezi ya kitaifa nikajikuta ninapageuza ugenini kuwa nyumbani na kwa maana hiyo hata familia yangu sasa hivi imeamua kuishi nilipo na sina shaka kwamba huenda uzee huu nikaumalizia hapa wakati wanangu wakimalizia mikoa mingine.
Suala la mchanganyiko kwa Watanzania ambalo liliasisiwa na watu wachache enzi hizo ndilo lililoleta umoja na kuheshimiana kama ndugu kabisa.
Naandika waraka huu kwa sababu leo hii hakuna eneo ambalo lina watu wa eneo husika bila mchanganyiko. Ni dhahiri kwamba ule uamuzi wa kwenda jeshini mwaka mzima kituo cha mbali watu wengi hawakuuelewa, lakini pia kitendo cha kwenda kusoma elimu ya juu baada ya kufanya kazi miaka miwili kuna watu hawakuelewa kwamba ni sera maalumu ya kuvunja ukabila nchini ambao uliandaliwa na watu enzi hizo taifa likiwa na watu wachache waliopata elimu.
Pamoja na mema yote, ninadhani sasa inabidi tukubaliane kwamba ubora wa elimu si vyeti kama wengi wanavyodhani. Kuna jambo zaidi ya vyeti ili kuweza kujiridhisha kwamba mtu ameelimika. Wapo wenye vyeti vingi lakini katika utendaji wanaonekana wanapwaya sana.
Maisha yaliendelea hadi nilipokuja kufanya kazi katika kampuni kubwa kubwa za wakati huo. Kampuni ambazo nyingi zilikuwa viwanda vyenye kuzalisha bidhaa nyingi na bora, viwanda ambavyo leo hii havipo tena, kampuni ambazo leo hii hazipo tena. Viwanda na kampuni zilizoanzishwa na kuendeshwa na watu ambao wengi wao walikuwa na elimu ya kati.
Sasa hivi taifa letu lina wasomi wengi mno, tena wasomi wenye elimu ya juu kabisa, maelfu kwa maelfu. Jambo baya ni kwamba viwanda vingi vimekufa na ambavyo viko hai havina maisha tena ya uzalishaji kama zamani. Kampuni zimekufa kwa kisingizio cha kukosa mtaji na kadhalika. Kampuni nyingi zinapoajiri zinaangalia makaratasi ya vyeti, si uwezo binafsi wa mtu.
Ninajua nina kazi kubwa ya kuelezea mwendo tuliopita mpaka hapa tulipo. Historia ni lazima iandikwe na waandikaji lazima tuandike sasa ili kizazi kijacho kijue.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.
Mwisho