Katika sehemu iliyopita ya makala hii tuliona historia ya vyama vya siasa hapa nchini tangu wakati wa ukoloni. Tuliona jinsi wakoloni nao walivyowatumia baadhi ya wazawa kuanzisha vyama ambavyo vilikuwa na wanachama Waafrika kwa lengo la kutaka kuwagawa.
Lakini katikati ya ulaghai huo pia kulikuwa na vyama mahiri vya Watanganyika wenyewe kama vile TANU. Tuliona kuwa awali kulikuwa na vyama vikubwa vinne.
Basi, baada ya vyama hivyo vikubwa vinne palizuka pia vyama vingine viwili vya kimkoa navyo vilijulikana kama: The Masasi African Democratic Union — MADU na cha mwisho kiliibuka huko Tanga kwa Wagosi wa Kaya kilichoitwa The All African Tanganyika Federal Independence Party (AATFIP). Hiki hakikuwahi hata kushiriki uchaguzi ule wa mwaka 1958, kilikufa kienyeji tu na wala hakikusikika sana.
Mwingereza alipopanga uchaguzi wake ule wa mseto alitarajia na kutumaini sana UTP na TUMO watachomoza kidedea na kuzima kiherehere cha TANU kudai uhuru.
Ndiyo maana aliandaa uchaguzi wa makundi yote matatu; Wazungu, Wahindi na Waafrika wapate viti sawa katika Baraza la Kutunga Sheria. Kila kundi lilitengewa viti 10 ilimradi weusi wa Wana TANU usiathiri baraza lile jipya!
Serikali ya Mwingereza ndiyo mamlaka iliyoandaa na kusimamia uchaguzi ule. Walitunga kanuni na masharti kwa wapiga kura na kwa wagombea wa viti katika Baraza la Kutunga Sheria. Kwanza kabisa kila mpiga kura alilazimika kuwapigia kura watu watatu tofauti akiwemo Mzungu, Mhindi na Mwafrika.
Baada ya sharti hilo zilitolewa sifa au yalikuwepo masharti kadhaa kwa wapiga kura wenyewe na kwa wagombea watarajiwa wa viti katika Baraza lile jipya la Kutunga Sheria.
Sifa na masharti yaliyotolewa yalikuwa; lazima mpiga kura awe na umri usiopungua miaka 21; awe ameishi Tanganyika kwa muda wa miaka mitatu mpaka wakati wa kujiandikisha; awe ameishi katika jimbo la uchaguzi kwa muda wa miezi sita ya nyuma; au awe amehitimu darasa la VIII shule ya kati siku zile (middle school); awe na kipato cha 3,000/- kwa mwaka; awe mjumbe wa halmashauri iliyopita; awe mjumbe wa halmashauri ya mamlaka ya wananchi kama mjumbe wa halmashauri ya mkoa au wilaya.
Sharti jingine ambalo liliwekwa kwa lengo la kuwaengua wengi kugombea nafasi hizo ni kuwa ni lazima mpiga kura awe mtawala wa jadi/chifu, liwali, akida na kadhalika.
Kwa mazingira ya mwaka 1958 ni Waafrika wachache sana waliweza kustahili kujiandikisha kupiga kura kwa sababu walikosa sifa hii.
Je, mwaka huu 2019 masharti yetu ya kujiandikisha yakoje? Sisi sote tulihimizwa kujiandikisha wala hatukuwa na vikwazo kama vile vya wenzetu mwaka 1958.
Sifa za mgombea
Sifa za mtu aliyetaka kuwania nafasi katika Baraza la Kutunga Sheria zilimtaka mgombea awe na umri usiopungua miaka 25; awe ameishi Tanganyika kwa muda wa miaka minne kabla ya uchaguzi, awe anazijua lugha za Kiingereza na Kiswahili sawasawa ili aweze kusoma nyaraka za baraza bila shida; awe amesoma angalau mpaka darasa la kumi la sekondari; mgombea awe na kipato kisichopungua 4,000/- kwa mwaka; awe amependekezwa na wapiga kura waliojiandikisha wasiopungua 25 wakiwemo Waafrika, Wazungu na Wahindi.
Kama alikuwa Mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria hapo awali, basi awe tayari kula kiapo cha uaminifu kwa serikali ya Malkia wa Uingereza; mgombea awe na sifa za kumwezesha kupiga kura, awe tayari kuweka dhamana ya 500/- ambazo anaweza kuzipokea asipoweza kufikia kiwango maalumu cha kura kilichowekwa.
Masharti haya yaliwafanya Wana TANU wengi kushindwa kufikia sifa, hivyo wakayakataa. Waliyaona kuwa ni masharti kandamizi. Wana TANU walijiona ni wengi kuliko yale mataifa mengine ndipo wakajiuliza iweje wapate viti 10 tu sawa na Wazungu wachache sana na Wahindi? Mataifa haya kamwe hayakushirikiana, sasa Waafika wangewajuaje wagombea wale wengine?
Suala la elimu nalo lilikuwa gumu maana hizo shule za kati (middle school) zilianzishwa miaka ya 1953 — 1954; sasa kweli Waafrika wangapi walimaliza hilo darasa la VIII mwaka 1958? Na ni Wana TANU wangapi walikuwa hata na ile elimu ya darsa la X?
Kumbe masharti yale yote yaliwekwa kwa lengo la kuwapendelea wanachama wa UTP na TUMO. Hapo ndipo karibu wanachama wote wa TANU waliamua kutoshiriki katika uchaguzi ule na ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kusikika kauli ya kususia uchaguzi katika nchi ya Tanganyika.
Kilipoitishwa kikao cha Halmashauri Kuu ya TANU pale Tabora mwaka 1958, ajenda pekee ilikuwa ni ya kususia uchaguzi ule wa mseto.
Kwa vile TANU kilikuwa ndicho chama kikubwa cha upinzani wakati ule, matokeo ya kususa kama kungefanikiwa sijui hali ya Tanganyika ingekuwaje leo hii!
Rais wa TANU alikuwa ni kijana wa umri wa miaka 36 tu naye ndiye Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Umri huo wa Mwalimu Nyerere haulingani kabisa na umri wa viongozi wa vyama vya siasa wa siku hizi. Siku hizi vyama vinaongozwa na watu wazima wenye umri kati ya miaka 55 — 60. Kuna tofauti kubwa sana.
Mwenyekiti wa CCM ana umri wa miaka 60, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Upinzani — CHADEMA, ana umri karibu au hata zaidi ya huo. Na Mwenyekiti wa CUF naye ni mtu mzima. Mwenyekiti wa NCCR — Mageuzi naye ni mtu mzima na Mwenyekiti wa ACT — Wazalendo naye yuko huko kwenye umri wa miaka zaidi ya 50.
Tofauti kati ya kijana yule wa miaka 36 siku zile na watu wazima hawa viongozi wetu wa leo ni moja; kutoa uamuzi wa busara kwa manufaa ya taifa. Wakati kiongozi kijana Nyerere alikabiliwa na masharti kandamizi sana ya uchaguzi mwaka 1958 alitoa uamuzi mgumu kwa wanachama wa TANU kushiriki uchaguzi ule wa mseto.
Mwaka huu viongozi wetu watu wazima hawa tena wote wasomi wa vyuo vikuu na isitoshe karibu wote wamepitia kambi za JKT walikopikika kiuzalendo, wametoa uamuzi wa kususia uchaguzi wa serikali za mitaa. Hapo pana tofauti kubwa sana ya namna ya kuwashawishi wafuasi wao.
Mwalimu alipowakumbusha Halmashauri Kuu ya CCM pale Tabora mwaka 1988 historia ya ule uchaguzi wa mwaka 1958 alisema: “…nilipotoka Dar es Salaam kuja hapa Tabora kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya TANU mwaka 1958, nilikuwa na mambo mawili. Moja ni hilo la kuwaelezea Wana TANU juu ya uchaguzi ule wa mseto na niwaombe Wana TANU tuiombe serikali ya Mwingereza wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria wawe wa kuchaguliwa na wananchi wenyewe. Pili, ni lile la kuomba wajumbe Waafrika wawe wengi katika hilo Baraza la Kutunga Sheria tofauti na ilivyokuwa wakati ule ambapo gavana ndiye alikuwa akiteua wajumbe.”
Wakati huo mpango wa serikali ulikuwa tofauti kabisa na matarajio ya TANU. Serikali ya Mwingereza ilishapanga katika uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria kuwepo na uwakilishi sawa kwa mataifa yote. Wazungu viti 10, Wahindi viti 10 na Waafrika vitu 10. Ndiyo uchaguzi wa mseto.
Mwalimu akisimulia pale Tabora mwaka 1988 akasema: “TANU walikuwa hawapendi hata kidogo uchaguzi wa namna ile, walisema itakuwaje Waafrika milioni tisa tupate viti 10, hawa Wazungu wachache sana (wapatao 25,000 tu wakati ule) nao wapate viti 10 huku Wahindi (waliokadiriwa kuwa watu wapatao 100,000 hivi) nao wapate viti 10? Upuuzi gani huo? Ni dharau kwa Waafrika kulinganishwa na wageni wachache wale. Wanachama wa TANU hawakulikubali jambo lile wakaazimia kususia uchaguzi huo.
Ndipo Mwalimu akaendelea kusema: “Sasa kazi yangu moja ilikuwa kuwashawishi wajumbe wa Halmashauri Kuu ya TANU wakubali kitu ambacho hawakukipenda hata kidogo…. Mimi nilidhani watafanya kosa wakikataa kupiga kura, kwa sababu wale wa vyama vingine watapiga kura. Tayari tulikuwa tuna vyama vya hovyo hovyo hivi, na wangekubali. Vingepiga kura wao kwa hiyo wangeingia hawa watu wa vyama vya hovyo. Wangeingia ndani ya Baraza la Kutunga Sheria na wao ndio wangeonekana duniani kana kwamba wao ndio watetezi wa wananchi. Sasa hili nilidhani ni kosa kubwa sana” …..(Hotuba ya Mwalimu Tabora Februari 5, 1988).
Kwa uamuzi ule wa Kiongozi na Rais wa TANU, uchaguzi ulifanyika na matokeo yake TANU walishinda wakaingia katika Baraza la Kutunga Sheria na kuleta mageuzi endelevu hata tukapata Uhuru Desemba 9, 1961.
Laiti Mwalimu asingesimama kidete kushawishi wanachama wa TANU wakubali uchaguzi ule wa mseto sijui Tanganyika ingepata uhuru lini.
Kwa muda wa siku tatu Mwalimu alikuwa anawashawishi wajumbe wake wa Halmashauri Kuu waukubali uchaguzi ule.
Wana TANU hawakupenda. Cha ajabu ni kuona hata wajumbe wa kutoka Mkoa wake wa Mara kina Bhoke Munanka, Richard Wambura na hata mdogo wake, Joseph Kizurira Nyerere walimpinga Mwalimu. Mwalimu anasema hoja yake ilikuwa Waafrika waingie ndani ya lile Baraza la Kutunga Sheria.
Itaendelea…