DAR ES SALAAM
NA MWANDISHI WETU
Mgogoro wa kibiashara baina ya wajasiriamali wawili, Jesca Kikumbi na Tausi John wote wa jijini Dar es Salaam umewaingiza baadhi ya askari kutoka Kituo cha Polisi cha Ukonga Stakishari kwenye kashfa ya kuihujumu Baa ya Seven Eleven iliyopo Tabata Segerea.
Tausi John, ambaye ni mmiliki wa nyumba ilimo baa hiyo, anawatuhumu baadhi ya askari katika kituo hicho kutumiwa na Jesca, aliyekuwa mpangaji wa jengo lake kwa miezi sita, kuhujumu baa hiyo pamoja na mpangaji wake wa sasa, Chuki Shabani.
Anasema amekwisha kukamatwa mara kadhaa na kufikishwa kituoni hapo kwa tuhuma mbalimbali lakini wameshindwa kumfikisha mahakamani kwa sababu hakuna kosa alilolifanya.
Anasema katika siku za hivi karibuni, alikamatwa na kufikishwa kituoni hapo baada ya Jesca kumtuhumu kuiba vifaa vyake vyenye thamani ya Sh milioni 30 ambavyo alikuwa ameviweka kwenye nyumba hiyo.
Anasema cha kushangaza ni kuwa yeye amewahi kufikisha kituoni hapo malalamiko kadhaa dhidi ya Jesca lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa.
“Hivi unaweza kufungua eneo lako kihalali halafu mtu baki akaja na hoja kwamba umebomoa na kuiba, mtu mwenyewe nilimpangisha kwa miezi sita mkataba wake ulishakwisha lakini anataka kuendelea kukaa,” anasema Tausi.
Anasema migogoro iliyopo katika baa hiyo inatokana na chuki ya kibiashara inayotengenezwa na Jesca kwa kushirikiana na polisi wa Kituo cha Stakishari ili kumkwamisha kibiashara.
Awali baa hiyo ilikuwa inafahamika kwa jina la Kitambala Cheupe, jina ambalo lilikuwa linatumiwa na Jesca wakati amepanga humo.
Wakati huo Jesca akawapangisha watu wengine kinyemela na hapo ndipo sokomoko lilipoanza.
Tausi anasema Jesca alishindwa kukaa kwa amani na wapangaji aliowapangisha kinyemela kwa kile kinachoelezwa kuwa wivu wa kibiashara baina yake na wao.
“Jesca nilimpangisha mimi naye akatafuta wapangaji wa kwake bila kunishirikisha, alimpangisha Chuki Shabani na mke wake ili wauze chakula naye auze vinywaji, lakini wivu wa kibiashara ukawa unamsumbua dhidi yao,” anasema Tausi.
Kutokana na wivu huo, Jesca aliwataka Chuki na mke wake kumpatia sehemu ya kuweka jiko ili naye auze chakula wakagoma kwa hoja kuwa si makubaliano waliyoingia.
Baada ya kushindwa kuelewana, Juni mwaka huu Jesca alikodi mabaunsa wakafanya vurugu katika baa ili Chuki na mke wake waondoke.
Inaelezwa tukio hilo liliripotiwa Kituo cha Polisi Stakishari na mmoja wa mabaunsa waliohusika akakamatwa lakini baada ya kupewa dhamana alitoroka.
Aliyempa dhamana baunsa huyo anatajwa kuwa ni Jesca mwenyewe, lakini akawahi kuripoti kwa Kamanda Msaidizi wa Jeshi la Polisi Ilala, Zuberi.
Alipotafutwa na JAMHURI, Chemberwa alikiri kufuatwa na Tausi na Chuki kuhusiana na suala hilo na kuagiza uchunguzi ufanywe.
Pia kamanda huyo wa Polisi amemtaka mfanyabiashara Chuki Shabani anayeendesha biashara ya kuuza vinywaji katika baa hiyo kuendesha bishara hiyo kwa kuzingatia sheria ya mazingira.
Baa hiyo inalalamikiwa na wakazi wa maeneo hayo kwamba inapiga muziki mkubwa na kusababisha kero ya makelele, hasa kwa mmiliki wa Hospitali binafsi ya General Hospital iliyopo jirani na baa hiyo.
Kamanda Chemberwa amesema ataendelea kusimamia suala la upigaji muziki katika kumbi zote za starehe kwenye maeneo anayoyaongoza kwa sababu lipo kisheria.
Amemuagiza Chuki Shabani kuhakikisha anawasimamia ipasavyo wafanyakazi wake wasipige muziki mkubwa ili kuondoa malalamiko ya wakazi wa eneo hilo kumpigia simu kila mara wakimtaarifu juu ya uwepo wa kelele za muziki.
“Nakuomba ufanye biashara kistaarabu, uachane na masuala ya wapambe. Ninalifuatilia kwa ukaribu suala la hiyo baa kupiga muziki. Nimefika kwenye eneo la baa hiyo mara mbili, kuna siku nilikuja muda wa saa mbili usiku nikasikia muziki umepigwa kwa nguvu halafu ghafla ukazimwa.
“Niliwaagiza askari wangu kumkamata DJ na vyombo vyake, aliletwa hadi hapa ofisini kwangu nikamueleza akwambie ufuate taratibu za kupiga muziki katika baa yako ili sote tulindiane vibarua,” amesema Chemberwa.
Naye, Chuki Shabani amemuomba RPC Chemberwa kuwaelekeza askari wa kituo cha polisi kufanya kazi kwa weledi ili kuondoa maneno ya mitaani kwamba askari wamewekwa mfukoni na Jesca.
“Kila mara polisi wanakuja kunikamata kwamba ninapiga muziki mkubwa wakati si kweli. Nimejaribu kuhoji lakini ninajibiwa na polisi wa Stakishari kuwa wao wanatekeleza maagizo kutoka juu, sasa hili mheshimiwa linampa kiburi Jesca kuwa ana mtandao mkubwa hadi ofisini kwako, hivyo atatuendesha anavyotaka,” anasema Chuki alipokutana na Chemberwa.
JAMHURI lilipowasiliana na mama wa Jesca, maarufu kwa jina la Mama King Kiki baada ya kumkosa Jesca, alitoa tahadhari kwa mwandishi akimtaka kutojiingiza kwenye mgogoro huo.
“Habari za waandishi kuniuliza mambo ya mwanangu sipendi, hayo ni mambo ya kipumbavu, sitaki kusikia habari za huyo mpumbavu anayekutuma wala mpumbavu wa serikali ya mtaa. Usijiingize kwenye jambo usilolijua utapoteza maisha bure,” anasema Mama King Kiki.
Naye, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Segerea, Peter Moses, amelieleza JAMHURI kuwa hawezi kuongea chochote, na kusisitiza kuwa hataki ushirikiano tena na Tausi ili kujiepusha na shida kwenye kazi zake.
Tamati…