Na Aziza Nangwa


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Juma Abed, ametinga mahakamani akikabiliwa na mashitaka mawili ya kushawishi na kupokea rushwa.
Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Euphrazia Kakiko, amesema wakati akisoma mashitaka dhidi ya mwenyekiti huyo kuwa mtuhumiwa Januari 1, 2019 na Julai 22, mwaka huu alitenda makosa mawili kwa nyakati tofauti.
Kakiko amesema mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa anashitakiwa kwa kosa la kujihusisha na vitendo vya rushwa kinyume cha Kifungu Na. (1)(a) na (2) cha Sheria Na. 11 ya mwaka 2007.
Kosa la pili ni kupokea rushwa ya Sh 220,000 kutoka kwa Bashiru Omary Chande kumshawishi amsaidie kumpatia uhamisho mke wake ambaye ni mwalimu kutoka Wilaya ya Babati kwenda Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani. Malipo ya ushawishi huo yalifanyika kwa njia ya simu.
Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu hakimu wa wilaya ambaye alikuwa anatakiwa kusililiza kesi yake alikuwa amepata udhuru, hakuwapo mahakamani hapo, hivyo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, Veroni John, akaomba mtuhumiwa apangiwe tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Mtuhumiwa amepewa dhamana ya Sh milioni moja na wadhamini wawili, ambapo alikamilisha masharti na yuko nje kwa dhamana.
Kesi yake ilitajwa tena katika Mahakama ya Wilaya ya Mkuranga kwa Hakimu Kennedy Mloso, ambapo mshitakiwa amesomewa tena mashitaka yote Desemba 4, mwaka huu na akakana mashitaka yote mawili. Kesi imepangwa kusikilizwa tena Desemba 18, mwaka huu.
 
Mwisho