London, Uingereza
Safari ya Uingereza kujiondoa katika Jumuiya ya Ulaya (EU), maarufu kama Brexit imeiva. Hii ni baada ya Chama cha Conservative chini ya Waziri Mkuu Boris Johnson kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika Desemba 12.
Boris sasa ataweza kupitisha hoja zake za kuiondoa Uingereza EU kwani amepata idadi kubwa ya wabunge ambayo itamwezesha kupata idadi ya kura zinazotakiwa kupitisha hoja hizo bungeni.
Awali, mtangulizi wake, Thereza May na yeye walikwama kupitisha hoja hizo kwani hawakuwa na theluthi mbili ya wabunge, idadi ambayo inatakiwa kupitisha hoja hizo.
Uchaguzi wa majuzi umekipatia chama hicho zaidi ya theluthi mbili ya wabunge, jambo ambalo sasa linampa jeuri Johnson na chama chake kujihakikishia kuwa hoja zao zitapita bila shida.
Johnson mwenyewe ameshatangaza kuwa safari ya Uingereza kutoka EU Januari 31 kama ilivyokuwa imepangwa itatimia, kwani hakuna tena kikwazo.
Wakati Conservative na Johnson wakishangilia, uchaguzi huo umeleta majonzi kwa Chama kikubwa cha Labour chini ya kiongozi wake, Jeremy Corbyn, ambacho kimeshangazwa na matokeo ambayo yamesababisha kushuka kwa idadi yake ya wabunge.
Wabunge wa Labour ndio walikuwa mwiba kwa Uingereza kujitoa EU kwani kila mara walikuwa wanapinga miswada ya sheria inayopelekwa bungeni ili kuiwezesha Brexit.
Johnson aanza mbwembwe
Majuzi Johnson alitembelea kaskazini mwa Uingereza kama sehemu ya kusherehekea ushindi huo mkubwa katika kipindi cha miaka 30.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi hcho Conservative kimefanikiwa kupata ushindi katika maeneo mengi ambayo yalikuwa yametawaliwa na Labour.
Johnson anasema ni matarajio yake kuwa ushindi huo utawezesha chama chake kumalizana na suala la Brexit na kuanza mchakato wa kuponya vidonda vilivyotokana na suala hilo ambalo kwa kiasi kikubwa limeigawa Uingereza.
Uchaguzi huo umekiwezesha Chama cha Conservative kupata wingi wa zaidi wa wabunge 80, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu mwaka 1987.
Tofauti na hilo, Labour kimepata pigo kubwa katika uchaguzi tangu miaka ya 1930.
Corbyn amesema amesikitishwa na matokeo hayo licha ya kujitahidi kufanya yote yaliyo chini ya uwezo wake kuhakikisha Labour kinashinda.
Kutokana na matokeo hayo mabaya, Corbyn ametangaza kuachia ngazi mapema mwakani ili kutoa nafasi kwa mtu mwingine kukiendesha chama hicho.
“Kujiuzulu ndilo jambo la uwajibikaji kulifanya katika mazingira kama haya, lakini siwezi kuondoka na kuacha chama katika hali kama hii, hivyo nitasubiri hadi mapema mwakani,” anasema.
Lakini, wakati Corbyn akijiandaa kuachia ngazi, Johnson amesema anajiandaa kufanya mabadiliko madogo katika baraza lake la mawaziri.
Wabunge waliochaguliwa katika uchaguzi huo wanatarajia kufanya kikao chao cha kwanza leo kuanza mchakato wa kuapishwa kabla malkia hajalifungua bunge lao rasmi keshokutwa Alhamisi katika sherehe zisizo za mbwembwe nyingi.
Johnson anasema anapanga kuurudisha bungeni muswada wake wa Uingereza kujitoa EU kabla ya Sikukuu ya Krismasi.
Hilo litawawezesha wabunge kuanza mchakato wa kutunga sheria itakayoiwezesha Uingereza kujitoa EU ifikapo Januari 31, mwakani. Baada ya hapo mjadala kuhusu mahusiano ya kibiashara kati ya Uingereza na nchi nyingine utaanza mara moja.