DAR ES SALAAM
NA AZIZA NANGWA
Daktari bingwa wa magonjwa ya ini katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Ewaldo Komba (pichani), amewataka Watanzania kujenga tabia ya kupima kama njia ya kuhakikisha kuwa haiwaathiri katika hatua za mwisho.
Dk. Komba amesema ugonjwa huo ambao kitaalamu hujulikana kama Hepatitis B, ni moja ya magonjwa yanayosababisha vifo vingi nchini.
Amesema tatizo kubwa la ugonjwa huo ni kuwa dalili zake huchukua muda mrefu kujitokeza wazi wazi, hivyo huua taratibu.
Amesema ugonjwa huo kwa sasa umekuwa ukiongezeka kwa kasi kubwa na wengi wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya tiba huwa wamechelewa sana, kwa sababu dalili zake huchukua muda mrefu kujidhihirisha.
Komba ameongeza kuwa ugonjwa huo unashambulia mwili wa binadamu taratibu kwa hatua za mwanzoni na unapokosa tiba unajenga usugu, hivyo kuwa vigumu sana kuutibu unapogundulika katika hatua za mwisho.
“Tatizo jingine ni kuwa ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya kujamiiana kama vile ukimwi. Lakini wengi hawalitambui hili,” anabainisha.
Ameongeza kuwa kuna aina mbili za ugonjwa huo, nazo ni acute na chronic, pamoja na kujamiiana lakini pia ugonjwa huo unaambukizwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, pamoja na vyanzo vingine kama vile mate au majimaji ya mwili.
Dk. Komba anasema ingawa kuna makundi mengi ya Hebatitis kama vile A,B,C,D,E lakini asilimia kubwa ya Watanzania wanapata Hepatitis ya kundi B, kutokana na asili ya upatikanaji wake unaotokana na njia ya kujamiana na kwa maambukizi ya virusi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Nchi za Ulaya wenzetu wamepiga hatua kubwa sana katika kudhibiti virusi hivi kusambaa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kuliko nchi zinazoendelea kama Tanzania ambako unakadiriwa kuwa asilimia saba ya watu wameambukizwa,” anasema Dk. Komba.
Anaongeza kuwa wagonjwa wakifikia hatua ya acute hepatitis ni rahisi kuudhibiti ugonjwa kwa asilimia 30 lakini katika hatua ya chronic udhibiti wake unakuwa mgumu sana.
Anasema watu wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano wamo katika hatari kubwa ya kuambukizwa Hepatitis C, hivyo kuathirika kimwili na kiakili.
Dk. Komba anasema kuwa virusi vya Hepatitis B vinaweza kuishi kwa muda mrefu katika mwili wa binadamu kama mtu huyo ana kinga kubwa ya mwili.
Anasema dalili za ugonjwa huu hujificha sana, hivyo ni vigumu kwa watu wengi wanaoambukizwa kuubaini katika hatua za mwanzo kama hawatakuwa makini.
“Asilimia kubwa ya watoto wanaopata maambukizi ya ugonjwa huo wanaambukizwa na mama zao wakati wa kuzaliwa. Lakini tatizo ni kuwa baada ya kuambukizwa huchukua muda mrefu kwa dalili zake kuanza kuonekana wazi wazi. Inachukua kati ya miaka minane na kumi kwa dalili kuanza kujionyesha,” anafafanua.
Mwisho