Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wamefanikiwa kuwabaini wajanja waliokuwa wanataka kuuibia mfuko huo Sh bilioni 7.4 kupitia madai hewa.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga, aliyesema kuwa hilo limewafanya wazidi kuimarisha mikakati mbalimbali ya kupambana na vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya watoa huduma, wanachama na watumishi wa mfuko wasio waaminifu.

Konga alikuwa akizungumza na JAMHURI kuhusiana na mafanikio ambayo mfuko huo umeyapata katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli.

“Aprili 2018 mfuko uliimarisha mifumo yake ya kupambana na udanganyifu kwa kuanzisha kitengo cha kudhibiti udanganyifu na tangu kuanzishwa kwa mfumo huo mfuko umefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh bilioni 7.4 kati ya Aprili 2018 hadi Agosti mwaka huu,” amesema Konga.

Konga ameelezea njia kuu tatu ambazo zinatumika kulinda uhai wa mfuko na kuhakikisha unaendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania wengi. 

Kwanza, amesema kuwa ni kuyapa uangalizi wa karibu maeneo yote ambayo yana viashiria vya udanganyifu.

“Maeneo ambayo ni hatarishi zaidi kwa uhai na uendelevu wa mfuko ni pamoja na ya uandaaji na uchakataji wa madai kwa malipo ya watoa huduma, matumizi yasiyo sahihi vya vitambulisho vya matibabu, uandaaji wa vitambulisho kinyume cha utaratibu na uwasilishaji wa michango ya udanganyifu kwa kampuni binafsi,” amefafanua.

Aidha, ametaja mkakati mwingine kuwa ni hatua walizochukua kuhakikisha kwamba mfuko unazuia na kukomesha kabisa vitendo hivyo vya udanganyifu.

Amesema hilo limefanyika kupitia elimu kwa watumishi wa umma dhidi ya madhara ya vitendo vya udanganyifu, kufanya uchunguzi kwa kina dhidi ya watoa huduma na watumishi wa mfuko wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya udanganyifu, kuhakikisha fedha zote zilizolipwa kwa watoa huduma kutokana na udanganyifu zinarejeshwa na kufungua mashitaka, kuwafukuza kazi, kusitisha mikataba na watoa huduma wanaobainika kuhujumu fedha za umma kupitia uwasilishaji wa madai yenye utata na kuzuia matumizi ya kadi kwa wanachama wanaobainika kutumia kadi kinyume cha utaratibu.

Konga amebainisha pia kuwa wanashirikiana na Takukuru katika mapambano yao dhidi ya vitendo vya udanganyifu, wanaimarisha mifumo ya TEHAMA inayotumika katika kuhakiki wanachama, kuchakata madai, kuandaa vitambulisho vya madai, kudhibiti uwasilishaji wa madai kutoka katika maduka ya dawa, kupokea michango ya wanachama, waajiri na malipo mengineyo, kutoa elimu kuhusu madhara ya vitendo vya udanganyifu kwa watoa huduma.

“Pia tunafanya mapitio ya mara kwa mara ya vitita vya mafao kwa kuimarisha masharti na vigezo vya utumiaji wa huduma na kudhibiti matumizi mabaya ya huduma na kingine ni kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa watumishi wa mfuko, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi,” amesema Konga.

Amesema hata hatua ya kubadili vitambulisho vya zamani na kuleta vipya ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na undanganyifu, kwani vitambulisho vipya vimetengenezwa kwa teknolojia ambayo ni ngumu kughushi.

Konga amesema pia NHIF ina mfumo mpya wa kupokea malipo kwa njia za kielektroniki kutoka kwa watoa huduma za afya na mfumo wa kuwasilisha madai moja kwa moja mara baada ya kutoa huduma kwa mwanachama.

Konga alitoa wito kwa umma kutoshiriki katika vitendo hivyo vya ubadhirifu kwani wakibainika watakabiliwa na adhabu kali. Pia amewataka wananchi kutoa taarifa haraka wanapobaini hujuma zozote dhidi ya NHIF.