Mabalozi wa nchi za SADC walioko Qatar wameunda umoja unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kimaendeleo na taifa hilo tajiri la Mashariki ya Kati ambalo ni moja kati ya wazalishaji wakubwa wa gesi asilia duniani.
Ikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania kupitia Balozi wake
nchini Qatar, Fatma Mohammed Rajab (pichani), iliongoza mchakato wa kuundwa kwa umoja huo ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 24, Oktoba mwaka huu.
Balozi Fatma ndiye mwenyekiti wa umoja huo unaojumuisha pia mabalozi wa Afrika Kusini na Eswatini ambao ni Faizel Moosa na Sicelo Dlamini mtawalia. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, umoja huo unaziwakilisha nchi zote za SADC hata zile 13 ambazo hazina mabalozi nchini humo kwa sasa kupitia sekretarieti ya jumuiya hiyo.
Mwanadiplomasia huyo amesema moja ya sababu kubwa ya kuanzishwa kwa umoja huo ni kuwa na ushirikiano wa karibu kiuchumi kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji na biashara kati ya taifa hilo na nchi za SADC. Mikakati iliyowekwa kufanikisha hilo ni pamoja na kuandaliwa mara kwa mara maonyesho ya kuzitangaza fursa na bidhaa zinazopatikana kwenye nchi hizi.
“Umoja huu wa mabalozi wa nchi za SADC Qatar ambao wanatoka Tanzania, Afrika Kusini na Eswatini ulizinduliwa
rasmi tarehe 24, Oktoba 2019 katika Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar,” Balozi Fatma aliliambia JAMHURI
wiki iliyopita.
“Lengo kuu la kuanzisha umoja huu ni kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za SADC na Qatar, hasa katika
sekta ya madini, viwanda, kilimo, elimu, michezo, utalii, biashara na uwekezaji,” alifafanua na kuongeza kuwa taifa
hilo litasaidia sana hata kwenye eneo la utafutaji wa gesi na maendeleo ya sekta hiyo kwa ujumla katika ukanda huu.
Kuundwa kwa umoja huo ni mwendelezo wa utaratibu wa nchi za SADC kujenga ushirikiano wa karibu na nchi na
jumuiya mbalimbali duniani kama tayari ilivyofanyika kwa Urusi, China na Umoja wa Ulaya. Sababu nyingine kubwa
iliyochangia Qatar kushirikishwa kwenye mpango huu ni kukua kwa ushirikiano kati ya nchi za SADC na Qatar miaka
ya hivi karibuni.
Hiyo ni baada ya taifa hilo kufungua milango zaidi ya kushirikiana na nchi za Afrika na tayari kwenye ukanda huu
imewekeza vilivyo Msumbji, imeimarisha usafiri wa bahari na Angola na Afrika Kusini ambayo pia ina mahusiano
makubwa kibiashara na nchi hiyo.
Kwa upande wa Tanzania, Balozi Fatma alisema wawekezaji wa Qatar tayari wanazifanyia kazi fursa zilizoko kwenye
sekta ya madini hasa utafutaji wa dhahabu. Pia Tanzania ingependa kuuza bidhaa zake za kilimo moja kwa moja
Qatar na kuondokana na hali ilivyo sasa hivi kwani nyingi zinapitia Kenya na Uganda.
“Ushirikiano baina ya nchini za SADC na Qatar unakua kwa kasi hivi sasa hasa baada ya Qatar kufungua milango zaidi ya
kushirikiana na nchi za Afrika. Tayari Qatar imewekeza kwenye sekta ya gesi nchini Msumbiji na imeanzisha
ushirikiano wa bandari na Afrika Kusini na Angola ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka na kwenda bandari
ya Hamad ya Qatar.
“Tayari bidhaa za chakula kutoka Afrika Kusini zimefurika kwenye soko la Qatar hasa nyama na matunda mbalimbali.
Tanzania pia inaleta bidhaa zake za maharage, mbaazi na viungo (spices), pia maparachichi ambayo yanapitia Kenya na Uganda. Afrika Kusini imefungua migahawa ya Nandos na maduka ya chakula ya Spur hapa Qatar,” mwanadiplomasia huyo aliliambia JAMHURI.
Pia alisema jitihada za makusudi zinafanyika kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Qatar ambazo
ukubwa wa biashara kati yao ulikuwa dola za Marekani milioni 38 mwaka 2018. Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Qatar ndiyo iliyonufaika sana baada ya kufanya mauzo ya takriban dola milioni 21.6 ukilinganisha na zaidi ya dola milioni 16.6 ilizozipata Tanzania.