Wapo mawakala na wapo wanaohitaji kuwa mawakala. Kwa sasa biashara ya uwakala ni moja ya biashara kubwa nchini. Wapo mawakala katika mitandao ya simu kama Tigo, Airtel, Voda n.k. 

Mawakala wa kampuni za usafirishaji kama mabasi, malori n.k, na makampuni mengine mengi. Mtindo wa biashara ya uwakala umekua sana katika siku za hivi karibuni. 

Ni kutokana na ongezeko la kampuni na kukua kwa biashara, upo umuhimu mkubwa wa kuijua biashara ya uwakala kwa undani, hasa katika misingi ya kisheria. Hii itakusaidia kuzijua haki zako. Usipozijua haki zako za kisheria katika biashara kama hii, ni vigumu kunufaika.

Hii ni kwa sababu hautajua unastahili nini na nini haustahili. Ili kuliepuka hili, unajikuta katika ulazima wa kuzijua taratibu za kisheria zinazohusu uwakala. Usiingie katika biashara hii bila kujua japo mambo kidogo ya msingi ya kisheria yanayohusu uwakala.

Wakala ni nani?

Sura ya 345, Kifungu cha 134 cha Sheria ya Mikataba kinaeleza nini maana ya wakala. Kinasema kuwa wakala ni mtu aliyeajiriwa kufanya kazi au kitu chochote kwa niaba ya mwingine au  kumwakilisha mtu mwingine katika shughuli fulani. Kwa hiyo wakala ni mtu anayesimama badala ya mtu mwingine. 

Huyo mtu mwingine huitwa mhusika mkuu. Kwa hiyo wakala hufanya kazi kwa niaba ya mhusika mkuu. Humwakilisha mhusika mkuu.

2.  Sifa za kuwa wakala

Vifungu vya 135 na 136 vya sheria hiyo vinaeleza sifa za mtu kuwa wakala au kuwa mhusika mkuu. Vinaeleza kuwa mtu yeyote mwenye umri wa mtu mzima,  yaani mwenye umri wa  miaka 18 na zaidi, anaweza kuwa wakala. Lakini pia ni lazima awe na akili timamu.  Kwa sifa hizi, pia unaweza kuwa mhusika mkuu.  

Hata hivyo hizi ni sifa za jumla za kisheria, yumkini zipo sifa nyingine kutegemea na mhusika mkuu anahitaji wakala wa aina gani kwa ajili ya biashara zake.

3. Mamlaka aliyonayo wakala

Kwa mujibu wa Kifungu cha 38, wakala anayo mamlaka makuu ya aina mbili. Kwanza, mamlaka ya kutamkwa (express); pili, mamlaka ya kumaanisha (implied). Mamlaka ya kutamkwa ni yale yote ambayo ameambiwa kwa mdomo au kwa maandishi kuyatekeleza.  Ni yale yaliyo katika mkataba wake alioingia na mhusika mkuu.

Pili, ni mamlaka ya kumaanisha. Haya hayapo katika mkataba wake na wala hakuambiwa na mhusika mkuu lakini ameyatekeleza. Haya ni yale ambayo wakala huyatekeleza kwa nia nzuri au kwa lengo la kuiokoa biashara dhidi ya jambo fulani ambalo limetokea ama kwa dharura au vinginevyo. 

Ikiwa wakala amefanya jambo jema na kwa nia njema, hata kama halipo katika makubaliano kati yake na mhusika mkuu, basi jambo hilo huhesabika ni sehemu ya mamlaka yake na mhusika mkuu hawezi kukataa kuliwajibikia kwa kisingizio kuwa halipo katika makubaliano.

4. Haki ya wakala kuzuia malipo ya mhusika mkuu

Ikiwa wakala anafanya biashara ambayo anatakiwa kuwasilisha pesa za mauzo kwa mhusika mkuu na ikatokea kuwa hajalipwa malipo yake, basi anaweza kuzuia malipo ya pesa hizo ili kufidia fedha anayodai. Muhimu ni kuwa asizuie fedha nyingi zaidi kuliko kiasi anachodai.

Pamoja na hayo, Kifungu cha 172 cha sheria kinasema hakutakuwa na malipo kwa wakala kwa kazi aliyoiharibu. Wakala anatakiwa kuwa mwangalifu, mtiifu kwa maelekezo ya mhusika mkuu na kujiepusha na uzembe au kutojali. Hasara anayoisababisha kutokana na haya itakatwa katika malipo yake.

5. Wakala kulipwa pesa isiyokuwa katika makubaliano

Ikiwa  wakala amefanya jambo jema na la faida kwa mhusika mkuu, basi wakala anastahili malipo ya jambo hilo hata kama malipo hayo hayamo katika makubaliano. Hii ni kwa mujibu wa Kifungu cha 174 cha Sheria ya Mikataba.

6. Fidia kwa kujiondoa katika uwakala

Yeyote kati ya mhusika mkuu au wakala anaweza kujiondoa katika uwakala. Yeyote atakayejiondoa katika uwakala kabla ya muda wa makubaliano kwisha, basi atalazimika kumlipa fidia mwingine. Akijiondoa wakala, fidia italipwa kwa mhusika mkuu, halikadhalika mhusika mkuu akijiondoa, fidia italipwa kwa wakala. Taarifa ya muda wa kutosha ni lazima itolewe kabla ya kujiondoa, la sivyo aliyejiondoa atalazimika kulipa fidia nyingine zaidi kwa madhara yaliyotokana na kujiondoa kwake ghafla.

Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.