Jana, Desemba 9, 2019 taifa letu limetimiza mwaka wa 58 tangu Tanganyika ijipatie Uhuru wake. Huwa tunajivunia tukio hili, lakini kiulimwengu sisi bado wachanga mno kimaendeleo tukilinganishwa na nchi za magharibi.
Wale wenzetu wanaitwa kimaendeleo nchi za ulimwengu wa kwanza wakati sisi ndiyo wa ulimwengu wa tatu.
Hizo nchi za ulimwengu wa kwanza zimepitia hatua mabalimbali kihistoria tangu enzi zile zinajulikana kama:
1: The Dark-Ages
2. The Stone-Age
3. Medieval Times
4. Renaissance
5. Industrial Revolution
Mpaka wakafikia hii hali ya kisasa inayoitwa “Modern Times”. Imewachukua karne nyingi kufikia hali waliyonayo leo.
Sisi Watanganyika ndiyo kwanza tumepita nusu karne ya Uhuru wetu, na tukiwa Watanzania mwakani tutaufikia mwaka wa 56 wa huo u-Tanzania wetu. Ndipo ninajiuliza, tunawezaje kujilinganisha kidemokrasia na wale wa nchi za magharibi? Tunawezaje kudai tuendeshe uchaguzi wetu kama wale wenzetu wa ulimwengu wa kwanza? Naona kama ni ndoto za alinacha tu.
Hebu tufikirie! Marekani waliotawaliwa na Waingereza na Wafaransa walijikomboa Julai 4, 1774. Ndipo walipojitangazia uhuru wao. Hata hivyo, uchaguzi wa kutumia visanduku vya kura walianza kutumia tangu mwaka 1884 wakati sisi tumeanza kuvitumia tangu mwaka 1958, wapi na wapi?
Tukiangalia hao Waingereza waliotutawala, wameanza mambo haya ya uchaguzi toka enzi za “Medieval Times” na baada ya kupitia maboresho mengi ndipo enzi za Mfalme Henry wa VIII, baada ya mageuzi makubwa yalitokea mwaka 1688 ndipo wakafikia kulipata Bunge lenye sura tunayoiona siku hizi. Ulipofikia mwaka 1911 ndipo Bunge la Uingereza likatuama na sisi tunastaajabia hiyo demokrasia yao. Basi ni upuuzi mtupu kwa wanasiasa wetu kuotea Tanzania tuwe na demokrasia kama ile ya Uingereza au Marekani au Ujerumani. Si ndio tunakwenda hatua kwa hatua tukiboresha huu uchaguzi wetu kwa matumaini ya kukamilika hapo baadaye. Tunahitaji uzoefu “Experiancia docet” walisema Walatini enzi za kale utawala wa Warumi.
Nchini Tanzania tulianza kupiga kura kwa masanduku mwaka 1958. Uchaguzi ule ulioendeshwa na Mwingereza mimi ningeita ulikuwa wa kutuhadaa Waafrika. Walituletea aina ya uchaguzi haujapata kutumika popote katika dunia hii wala sijui mkoloni aliubunije au alituonaje hata kutuletea uchaguzi kwa misingi ya rangi za wakazi wa Tanganyika (election based on racial status).
Mkoloni alisema kila mpiga kura anapaswa kuchagua Mzungu, Mhindi na Mwafrika. Nchi gani kumewahi kusikika uchaguzi namna hii? Hata kule Marekani kwenye mchanganyiko wa mataifa ya rangi zote duniani hakujawahi kutumika uchaguzi namna ile.
Kwanza, mkoloni hakutoa elimu ya kutosha juu ya uchaguzi ule wala hakutumia njia wanazotumia wenyewe Waingereza kuchaguana. Kwa hiyo sisi Tanganyika tulikuwa ni uwanja wa majaribio ya uchaguzi kwa misingi ya rangi.
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuliona hilo jaribio aliamua kupambana nalo mpaka lishindwe maana alishajua hila za mkoloni kutaka Tanganyika ionekane duniani kuwa ni nchi ya mfano kwa uchaguzi wa mseto (multiracial elections). Hakuwa tayari kwa hilo.
Chama cha Tanganyika African National Union (TANU) kilikuwa kinadai haki ya wazawa Waafrika wajitawale wenyewe. Wakadai Gavana Twining aache utaratibu wake wa kuteua wajumbe katika Baraza la Kutunga Sheria na badala yake uwepo uchaguzi, wananchi wawe na wawakilishi wao. Pili, siyo bora wawakilishi, bali katika Baraza la Kutunga Sheria wawepo Waafrika wengi zaidi kuliko yale mataifa ya wageni kama Wazungu na Wahindi.
Gavana Twaining akabuni uchaguzi wa kupata wajumbe katika lile Baraza la Kutunga Sheria eti wachague sawa Wahindi 10, Waafrika 10 na Wazungu 10. Loo! Hapo TANU hawakukubali walichachamaa na kwa vile ndio Chama Kikuu cha Upinzani siku zile wakaamua kabisa kugomea uchaguzi namna ile.
Hapo ndipo kwa mara ya kwanza kusikika kauli ya “kususia uchaguzi” katika nchi yetu. TANU walijua wasipoususia uchaguzi ule nchi yetu ingeweza kuingizwa kwenye mkenge. Mimi leo hii ninaposikia upinzani wanatamka KUSUSIA Uchaguzi wa Serikali za Mitaa sishangai maana nakumbuka hali yetu ile ya mwaka 1958 TANU walipokusudia kususia kushirika kwenye uchaguzi wa hovyo hovyo ule.
Mwaka ule 1958 hapa Tanganyika vilikuwepo vyama vya siasa kama sita hivi. Vyama vyenyewe vilikuwa The United Tanganyika Party – U.T.P, hiki kilianzishwa na serikali ya Mwingereza na kiliwajumuisha Wazungu walowezi, Wahindi wafanyabiashara na Waafrika waliokuwa vibaraka. Chama kingine kikubwa kilikuwa Tanganyika African National Union – TANU, hiki kilikuwa cha wananchi kilianza kutoka kwenye kile Chama cha Waafrika kilichoitwa TAA. Kukazuka Chama kingine kilichotoka kwenye TANU hiki kilikuwa African National Congress – ANC, chenye msimamo na siasa kali – ni cha watu weusi tupu. Halafu kulikuwepo na chama cha wajumbe wote wa Baraza la Kutunga Sheria walioteuliwa na Gavana, hiki kilikuwa The Tanganyika Unofficial Members Organisation – TUMO.