Wapo ambao walimsifia na wengine wakamponda wakati alipoamua kuhama kutoka kwenye lebo ya Wasafi na kuamua kusimama kivyake kama msanii anayejitegemea. 

Lakini hiki alichokifanya msanii Harmonize ni moja ya mambo ambayo yanaonyesha kukua kwa msanii ingawa asipocheza vema gemu inaweza kuwa ndiyo njia ya kuelekea kifo chake kisanii.

Kila zama na zama zake wapo wanamuziki wengi waliotingisha katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva humu nchini, wengi wao wamefifia ama hawapo tena kimuziki. Kipindi hiki jina la Harmonize ndilo linalotajwa kila kona kwa jinsi alivyoweza kukonga nyoyo za wapenda muziki huo, kwani ameamua kuachia ngoma baada ya ngoma baada ya kuachana na Wasafi.

Maudhui ya nyimbo zake yamesababisha kualikwa kwenye shughuli kubwa za kitaifa, ambako amekuwa akiwanyanyua vitini baadhi ya viongozi wakubwa, wakimtuza pamoja na kucheza naye.

Mfano halisi ni kwenye sherehe za kuzima Mwenge wa Uhuru na kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere zilizofanyika mjini Lindi, Oktoba 14, 2019.

Harmonize alifanya ‘kufuru’ kwa wimbo wake anaomsifia Rais John Pombe Magufuli kwa mambo makubwa ya maendeleo ya nchi yaliyofanywa kwa kipindi kifupi na Serikali ya Awamu ya Tano chini.

Wakati wimbo huo ukipigwa, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alikuwa mmoja wa watu walioinuka kwenye viti kwenda kumtuza Harmonize wakati akitumbuiza. 

Ingawa alibaki akifurahia kwenye kiti chake, lakini inaonekana wimbo huo ulimkuna pia Rais John Magufuli kiasi kuwa siku chache baadaye akampigia chapuo Harmonize kuwania ubunge katika eneo anakotokea katika Jimbo la Tandahimba.

Inaonekana kuwa hilo limempendeza Harmonize pia kwa sababu hajaonyesha kukataa wito huo.

Kuipitia ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, Harmonize amemjibu rais kwa  kusema: “Thanks a lot…!!! My President…!!! Doctor John Pombe Magufuli. Kama ilivyo ada ya kwamba kauli yako tukufu ni sheria, nikiwa kama mwananchi wa kawaida sinabudi kutii…!!! Lakini pia wananchi wenzangu wa Tandahimba wameipata hii kauli yako tukufu…!!! Bila shaka kwa pamoja tunaifanyia kazi…!!! Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Serikali ya Awamu ya Tano.”

Harmonize ni nani?

Ingawa wengi wanaweza kuwa hivi sasa ndiyo wanaanza kumfahamu Harmonize, lakini ni mwanamuziki ambaye amepitia milima na mabonde kufika pale alipo leo. Alizaliwa Aprili 15, 1994, katika Kijiji cha Chitoholi mkoani Mtwara, alipewa jina la Rajab Abdul Kahali, japo baada ya kupata umaarufu kimuziki, amejibatiza jina la ‘Konde Boy’.

Ni mwanamuziki mwenye talanta za kutunga na kuimba nyimbo za miziki ya Bongo Fleva pamoja na Afro Pop, wakati mwingine hupiga piano. Pia ni mtayarishaji wa nyimbo, hivyo nyimbo zake nyingi anatunga mwenyewe na kushiriki kwenye utayarishaji wake.

Miaka ya nyuma Mkoa wa Mtwara ulitoa wanamuziki waliokuwa wakipiga muziki hususan wa asili ya Kimakonde. Baadhi yao ni kama Halila Tongolaga na Che Mundugwao.

Pia kulikuwa na bendi ya Mitonga Jazz, iliyokuwa ikiwasha moto kwa muziki wa asili hususan katika wimbo wao wa ‘Mariana’.

Katika miaka ya 1990 hadi 2000, tulimshuhudia msanii maarufu wa kucheza na nyoka, Norbert Chenga, ambaye ni wa kabila la Wamakonde kutoka mkoani Mtwara, aliyekuwa akiongoza kikudi cha Muungano Dancing Troupe cha jijini Dar es Salaam.

Harmonize alianza kuvuma kwa vibao vyake vya kwanza, ikiwamo ‘Aiyola’ cha mwaka 2015, ‘Bado’ cha mwaka 2016, ‘Matatizo’ cha mwaka 2016 na baadaye akatoa nyimbo akishirikiana na msanii mwenzie kutoka lebo moja ya Wasafi Classic Baby (WCB), Diamond Platnumz.

Wimbo ‘Kwangwaru’ ni moja ya nyimbo ambazo zilianza kumpaisha Harmonize kimuziki kwani ulibamba karibia maeneo yote ya Afrika Mashariki na Kati kabla ya kuachia kibao kingine kiitwacho ‘Inama’, ambacho kiliongezewa nakshi kwa sauti ya mwanamuziki Fally Ipupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Utamu wa radha ya wimbo huo uliongezeka baada ya kumshirikisha msanii kutoka nje ya Tanzania, aitwaye Burna pamoja na Diamond Platnumz.

Kwa leo tuishie hapa, wiki ijayo tutaendelea kuangalia historia ya mwanamuziki huyu ambaye amepitia mambo mengi kabla ya kupata umaarufu kwenye sanaa.