*Asema udini na ukabila ni ufa unaobomoa Taifa letu
Moja ya hotuba za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, zisizochujuka ni ile aliyoitoa pale Kilimanjaro Hotel mbele ya Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania Machi 13, 1995.
Katika mazungumzo yake siku ile alitaja nyufa tano zinazolitikisa Taifa letu kuanzia kwenye paa, katika dari, kutani hadi kufikia katika msingi ule imara wa Taifa uliojengwa kwa muda mrefu. Nyufa zilizotajwa zilikuwa:-
* Muungano
* Kupuuza na kutojali
* Kuendesha mambo bila kujali sheria
* Rushwa, na
* Ukabila na udini.
Makala yangu itajikita katika huo Ufa Namba 5 – Ukabila na Udini katika Taifa letu. Nimechangamshwa na mawazo endelevu ya ile makala ya Elias Msuya. Msuya alikuwa anajibu tuhuma zilizotolewa na Thuway Owaray Juni 17, 2012. Katika makala yake Msuya ameongelea juu ya Sensa na Mahakama ya Kadhi kadiri yanavyochukuliwa na Waislamu.
Kwa muda mrefu sasa, miaka nenda miaka rudi hapa nchini kumesikika malalamiko au manung’uniko ya wafuasi wa dini moja kudai kukandamizwa au kunyimwa fursa sawa za elimu katika nchi hii.
Mfumo wa elimu umeonekana kuwa kandamizi na Serikali iliyoko madarakani haifanyi lolote kuondoa uonevu wa namna hiyo. Mfano ni ile makala ya Abu Firdaus aliyetoa malalamiko katika gazeti la moja la kila wiki No. 550 la tarehe 22-28 Aprili, 2004 iliyokuwa na kichwa cha habari, “Kweli udini Tanzania upo, tujirekebishe”.
Aidha, yalitolewa madai ya haki za Waislamu kama yalivyotolewa kupitia “Kauli ya Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania mwaka 1993. Mwaka 1998 kulitolewa “Submission” kwa Serikali kulaumu “Kanisa Katoliki na Serikali ya CCM”. Kuna malalamiko yanayojirudiarudia licha ya kutolewa majibu na mamlaka husika. Ndipo ninajiuliza kwani kulikoni?
Daima yanazuka malalamiko namna ile ile na hawa ndugu zangu, rafiki zangu, Watanzania wenzangu wanazuoni wazuri tu, kwa nini hawaridhiki? Huenda kuna jambo linatafutwa. Nikasema hebu nijaribu kuelezea kihistoria na kimila na utamaduni wa Kibantu (Historically and culturally based on indigenous African mentality) labda itasaidia kuona kiini cha yote haya ni nini?
Kwanza niwarudishe nyuma wasomaji wangu vijana mwaka 1962 baada ya Baba wa Taifa kula kiapo cha kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika.
Mwalimu alipokuwa analihutubia Bunge hapo Karimjee Desemba 10, 1962 alikuwa na maneno haya kwa wananchi wote, nanukuu “…as for example, the enmity which could be stirred up by the evil minded between Muslims and Christians; for, as we all know, the colonial government did not concern itself very much with African education and therefore the majority of those who managed to acquire any, did so in the mission schools and therefore Christians but a very large proportion of them are drawn from the Wahaya, Wanyakyusa and the Wachagga peoples (Nyerere: akilihutubia Bunge la kwanza la Jamhuri ya Tanganyika Desemba 10, 1962; taz. Uhuru na Umoja uk. 179).
Maneno haya yanaonyesha kuwapo kwa tatizo kielimu kati ya Wakristo na Waislamu na pia kuwa yapo makabila yaliyonufaika zaidi kielimu kuliko mengine katika nchi yetu. Aidha, lipo onyo la msingi kuwa, watakuwapo wakorofi na wasiokuwa na nia njema kwa uhuru wetu watakaotumia hali hiyo kuchochea manung’uniko na kuleta mtafaruku miongoni mwa wananchi huru.
Na ndivyo inavyotokea sasa watu namna hiyo wanalalamika udini na dhuluma katika kupewa elimu hapa kwetu. Baba wa Taifa kwa kuona mbali juu ya suala hilo alilipa dawa pale aliposema, “There is no easy way to remove the existing disparity in education between Christians and Muslims…” Katika hotuba yake ile ile ya Desemba 10, 1962 (taz. Uhuru na Umoja uk. 181).
Hakukomea kusema hayo tu, bali kama sote tunavyojua, mwaka 1970 Serikali ilitaifisha shule zote za misheni na za binafsi katika nchi yetu kama hatua muhimu ya kupunguza tofauti katika elimu kwa Waislamu na Wakristo maana kuanzia hapo hapakuwapo tena shule za misheni.
Matokeo ya utaifishwaji ule yameharakisha sana upatikanaji wa elimu dunia kwa Waislamu wengi hapa nchini. Hii ilikuwa njia ya kusawazisha upatikanaji wa elimu kwa watoto wote wa Taifa hili kwa kuwalea pamoja ili wajitambue ni watoto wa Taifa moja.
Kule visiwani Zanzibar, shule nyingi (majority) ni Waislamu na kila msichana anavaa hijabu kama sare. Hakujasikika Wakristo wakisema kuna udini, na wanabaguliwa kwa misingi ya dini. Elimu dunia haina dini. Ni utamaduni uliozoeleka kule Visiwani tangu enzi za sultani.
Pia ni vema tukakumbuka maneno ya Mzee wetu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, aliyoyatoa siku akifungua ofisi za Shirika la World Muslim League mwaka 1998 Dar es Salaam, alitamka hivi, namnukuu, “… Ndugu Waislamu, punguzeni malalamiko dhidi ya Serikali na muanze kufanya kazi… tujenge vyuo vya elimu ya Kizungu ili tuwaandae watoto wetu kushika nafasi za uongozi…”
Kuna mwongozo bora na safi kuliko huo? Mbona Zanzibari kunajengwa vyuo kadhaa vya Waislamu? Kwa nini Bara tunarudia rudia lalamiko lile lile la kubaguliwa kwa misingi ya dini wakati Serikali ilikwishafuta shule za dini? Kwa nini zisitolewe takwimu za vyuo na shule ngapi wakereketwa na wanaharakati Waislamu wamejenga kuandaa watoto wao kwa kushika uongozi?
Mwaka huu yameibuka malalamiko kwa matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa shule za Waislamu hata kuwafanya wengine wasiwe na imani na uongozi wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA).
Naona maelezo yaliyotolewa na Sadiki Godigodi yanatosheleza. Huyu ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tanzania ya Islamic Peace Foundation, ametoa maelezo ya kueleweka sana katika gazeti la moja la Jumatatu Juni 25, 2012 uk. 3. Ameeleza wasahihishaji wanaona namba za watahiniwa wala si majina yao, hivyo wasahihishaji hawajui karatasi hii ya Mwislamu au ya Mkristo!
Aidha, amekazia kuwa kamati mliyoiamini imefanya kazi kubwa na nzuri na uchunguzi wao umeonyesha wazi kuwa hawakulenga kuwafelisha wanafunzi Waislamu. Somo walilofeli zaidi ni Islamic Knowledge. Sadiki akaonya kuwa wote wanaonufaika na mgogoro huo waache fitina na kueneza chuki ambazo hazina misingi.
Siku za nyuma malalamiko ya mitihani yaliwahi kutokea miaka ile ya 1988-1990 na lilivuja dokezo la Wizara ya Elimu kwa Rais la Oktoba 12, 1988 lenye kuonyesha takwimu za watoto Waislamu waliochaguliwa/walioteuliwa kuingia kidato cha kwanza na wale waliochaguliwa kuingia chuo kikuu, kuthibitisha wanavyokandamizwa kwa mfumo wa elimu uliopo.
Basi, ukaundwa mkakati ulioitwa “Low Profile Operation” katika Wizara kuwapendelea watoto Waislamu! Astaghafirullah! Mkakati ule nao ukavuja na mambo yakamwagika katika vyombo vya habari.
Matokeo ya ile “low profile operation” yalikuja kuvuja na yakabainika kwa umma. Hapo basi vyombo vya habari vikaanza kuyaanika. Gazeti moja la kila siku toleo No. 14377 la Jumatatu, Juni 28, 1993 liliandika wazi upendeleo uliofanywa Dar es Salaam katika kuchagua watoto wa kuingia kidato cha kwanza. Majina ya watoto 84 Wakristo yaliachwa nafasi zao wakapatiwa watoto Waislamu.
Na katika gazeti hilo hilo toleo No. 14399 la Jumatano, Juni 30, 1993 yalitangazwa majina ya walimu 58 waliohusika na kashfa hiyo ya upendeleaji na kwa mujibu wa sheria walisimamishwa kazi Dar es Salaam. Sasa kwa mantiki hiyo ya “low profile operation” katika Taifa zima mikoa yote 21 ni watoto wangapi wasiokuwa Waislamu walidhulumiwa? Je, kulitokea sokomoko lolote kutoka kwa wazee wasiokuwa Waislamu kulaumu?
Basi, Watanzania wote tunapaswa tuwe wavumilivu na tuishi kwa kuimarisha msingi imara wa Taifa letu uliojengwa kwa miaka mingi. Tusiupe mwanya huu ufa wa udini na ukabila utumalize kwa kutumegamega vikundi vya udini au ukabila.
Baba wa Taifa alituasa kwa kusema hivi:- “Our third duty is to avoid the temptation of blaming others for our difficulties. There is no one among our fellow Tanganyikans on whom we could seize and say it was he who invented all these problems for us…” (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 181). Changamoto hapa ni kila mmoja wetu ajaribu kukwepa kishawishi cha kulaumu wengine kwa matatizo yanayotokea. Hakuna mchawi anayesababisha haya matatizo hapa nchini.
Mfano wa ulalamishi usio na msingi ni kama maneno yaliyosemwa na mjumbe mmoja Mwislamu tena kiongozi wa Kigamboni katika kikao pale Karimjee mwaka 2002, alilalamika hivi, “Shule sasa zimekuwa biashara; utakuta sheikh mmoja anafungua shule yake ya sekondari kwa watoto Waislamu, lakini yeye mwenyewe kielimu kakomea darasa la saba tu. Kwa kuwa watoto wanaosoma pale ni Waislamu, Serikali haifanyi lolote kusaidia shule namna hii”.
Je, hapa Serikali inahusikaje? Mbona zipo kanuni na taratibu za kufungua hizi shule za binafsi? Kwa nini Sheikh huyo hakuzifuata? Na vipi wazee wa watoto hao Waislamu wanakubali kupeleka watoto wao hapo? Haya yalianikwa katika gazeti la moja la mchana la Mei 10, 2000.
Itaendelea
Mwandishi wa makala haya, F. X. Mbenna, ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
Anapatikana kwa simu: 0755806758; email: [email protected]