Ukijificha fursa nazo zinajificha
Kuna watu wanajua mambo mengi lakini hawataki kutoka nje na kuonyesha yale waliyojaliwa. Kuna watu wana ujuzi mkubwa lakini hawataki kuonyesha ujuzi wao. Kuna watu wana mawazo mazuri ya biashara lakini hawataki kuanza kuyafanyia kazi. Kila unayemwona amefanikiwa ni kwamba aliona fursa mahali fulani akaanza kuifanyia kazi na ikampa matokeo makubwa. Unaweza ukawa na kipaji zaidi ya watu wengi lakini wale wanaojitoa na kuonyesha kipaji chao ndio dunia inawapokea na kuwaona kuwa ni bora. Ukijificha na fursa zinajificha pia. Ukijificha na fursa zinakukimbia.
Katika kitabu chake cha ‘Think And Grow Rich’, mwandishi Napoleon Hill anamzungumzia mtu aliyeitwa Edwin Barnes ambaye alikuwa na wazo na ndoto ya kufanya biashara pamoja na baba wa umeme duniani ambaye ni mgunduzi wa balbu ya umeme, Thomas Edson. Barnes alimwendea Thomas Edson na kumweleza kuwa yeye anaweza kumsaidia kufanya mauzo makubwa ya bidhaa alizokuwa akiziuza. Mungu si Athumani, Edwin alikubaliwa kuanza kufanya kazi na Thomas kama mtu aliyehusika na mauzo. Ukijificha na fursa zinajificha.
Askofu T.D. Jakes alikuwa mhubiri katika kijiji kinachoitwa West Virginia huko Marekani. Siku moja binti mmoja alimsikia Askofu T. D. Jakes akihubiri. Binti huyu aliona kitu ambacho T.D. Jakes anaweza kuieleza dunia. Hivyo aliamua kwenda kwa mchungaji wake kumwomba amruhusu T.D. Jakes ahubiri pale kanisani kwao. Mchungaji alimwambia binti yule: “Una uhakika na mtu huyu au ni kama wengine ambao hujidai wanalijua neno la Mungu?”
Binti yule alijibu: “Ndiyo nina uhakika na mtu huyo.” Kisha mchungaji akamwambia: “Kwa kuwa ninakuamini wewe, nitampa nafasi.”
Baada ya kupata nafasi ya kuhubiri, siku ya kwanza akiwa anahubiri, Paul Crouch, mmoja kati ya waanzilishi wa TBN (Trinity Broadcasting Network) alimsikia na alipendezwa na mahubiri yake, kisha akasema: “Itanipasa kumweka mtu huyu katika vipindi vya televisheni yangu.” Kilichofuata ni historia.
Leo hii T.D. Jakes ni mchungaji maarufu duniani lakini pia ni mwandishi mzuri sana wa vitabu ambavyo vimebadili maisha ya wengi. Ukijificha na fursa zinajificha. “Bahati ni kile kinachotokea pale maandalizi yanapokutana na fursa,” alisema Seneca, Mwanafalsafa wa Kirumi.
Pasipo na maandalizi fursa zinaweza zikaja upande wako lakini usizitambue hata kama ni fursa. Ni wale tu waliojiandaa ambao hufanikiwa kukumbatia fursa hizo.
Muda mwingine fursa zinakuja zikiwa zimevalia mavazi yasiyopendeza lakini ndizo zinakuwa fursa zenyewe. Mwaka 2018 kijana kutoka Mali, Mamoudou Gassama, aliingia kinyemela katika nchi ya Ufaransa. Siku moja akipita katika mitaa ya nchi hiyo alikuta kundi kubwa la watu wakipiga kelele na wakitazama juu. Alipotazama pia ili kujua kilichokuwa kinaendelea, alikuta ni mtoto wa miaka minne aliyekuwa anakaribia kudondoka kutoka ghorofa ya nne.
Mamoudou kwa haraka haraka akaanza kupanda akiruka kutoka ghorofa moja hadi nyingine na hatimaye aliweza kumwokoa mtoto huyo. Dunia nzima ilimtambua kama shujaa, akapewa kazi na uraia wa Ufaransa.
“Fursa haziji zikiwa na muhuri wa thamani yake,” aliwahi kusema mtu mmoja, na mlango wa fursa hauna alama ya ‘SUKUMA’ au ‘VUTA’. Kila fursa inapojitokeza mbele yake anza kuifanyia kazi, hauwezi kujua kesho na kesho kutwa itakupeleka wapi.
Kitabu ulichonacho kiandike. Nyimbo ulizonazo ziimbe. Makala ulizonazo ziandike. Ushauri ulionao utoe. Mashairi uliyonayo yaandike. Biashara uliyonayo ianzishe. Kipaji ulichonacho kitumie. Ujuzi ulionao utumie.
Uwezo ulionao uonyeshe. Utaalamu ulionao uonyeshe. Hakikisha unatumia fursa zinazokuja mbele yako kwa uweledi wa hali ya juu. Ilimlazimu Thomas Edson aanze kufunga umeme bure katika maofisi kabla ya mtu yeyote hajatamani hata kutazama kile alichokifanya.
Huko London nchini Uingereza, Gordon Ramsey alikuwa na wazo la biashara ambalo lilikuwa ni kuwafundisha wafungwa jinsi ya kutengeneza keki ambazo ziliuzwa nje ya gereza kwa wananchi. Hii iliwasaidia wafungwa kupata fedha za kujikimu, pia kupata ujuzi ambao ungewasaidia kupata na kufanya kazi baada ya muda wao wa kifungo kwisha.
Wewe pia unaweza kuwa Gordon Ramsey kwa kuifanya dunia iwe mahali pa furaha baada ya kuchukua fursa unayoificha. Jitoe sasa na onyesha fursa uliyoibeba mkononi, maana ukijificha na fursa zinajificha.