Ingawa deni la taifa limeongezeka maradufu miaka ya hivi karibuni na kufikia Sh trilioni 65 miezi mitatu iliyopita, ukubwa wake bado si hatarishi na si mzigo kwa taifa kama ilivyo sehemu nyingine duniani ambako madeni sasa ni tishio la ustawi kwa ujumla.


Kuna tofauti kati ya deni la taifa na deni la serikali. Deni la taifa linajumuisha deni la serikali (deni la ndani na nje) na deni la nje la sekta binafsi. Deni la nje la serikali linajumuisha pia deni la taasisi za serikali,” 

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa BoT, Dk. Suleiman Missango.

Hivi karibuni Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilionya kuwa dunia inazidi kulemewa mzigo wa madeni ambao sasa umeongezeka na kuwa dola za Marekani trilioni 188, kiasi ambacho kinayaumiza mataifa mengi kiuchumi na kuathiri shughuli za maendeleo hasa ya watu wa kawaida.

IMF inadai madeni yanazitesa serikali nyingi duniani na yameziumiza kampuni nyingi huku Tanzania ikisalimika, ingawa deni lake limeongezeka kwa takriban asilimia 60 katika kipindi cha miaka minne iliyopita. 

Deni la taifa liliongezeka kwa Sh trilioni 24.1  kati ya Septemba 2015 na Septemba mwaka huu, kutoka Sh trilioni 40.7 hadi Sh trilioni 64.8. Kiasi hicho ni sawa na Sh milioni 1.16 kwa kila Mtanzania kwa idadi ya watu milioni 56 mwaka huu na Sh 753,704 kwa kila mtu miaka minne iliyopita wakati idadi ya Watanzania ilikuwa milioni 54.

Viongozi wa IMF wanasema mzigo wa madeni duniani sasa ni zaidi ya mara mbili ya pato la dunia nzima ambalo ni kama asilimia 230 ya uzalishaji wote kwa mwaka. Deni hilo ni sawa na fedha za Tanzania Sh trilioni 432,400 ambazo ni sawa na mara 2,730.8 ya pato la taifa ambalo kwa sasa ni kama Sh trilioni 158.34.

“Mzigo wa madeni duniani umefikia rekodi mpya ya asimilia 230 ya pato la dunia, huku deni la sekta binafsi likiwa ndilo kubwa zaidi. Kuongezeka kwa deni hili ni tishio kwa serikali nyingi duniani na kunahatarisha maisha ya watu wa kawaida na maendelo yao kwa ujumla,” shirika hilo ambalo ni kiranja wa shughuli za kifedha duniani lilitahadharisha mwezi uliopita.

Akizungumza wakati wa mkutano kuhusu madeni duniani mjini Washington, Marekani mwezi uliopita, Mkurugenzi Mtendaji wa IMF, Kristalina Georgieva, alisema deni la dunia lilikuwa dola za Marekani trilioni 164 mwaka 2016.

“Deni la taifa linakuwa tatizo na changamoto ya kimaendeleo pale linapokwamisha ukuaji wa uchumi na kuwa mzigo kwa serikali, kutatiza makampuni na kuziumiza hata kaya,” alifafanua bosi huyo mpya wa IMF.

Ingawa mzigo wa deni la taifa umeongezeka kwa zaidi ya Sh trilioni 52 tangu mwaka 2009, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema deni hilo bado ni himilivu.

Pamoja na ukubwa wake, taifa bado linaweza kuendelea kukopa bila kuathiri uchumi, biashara na mapato ya serikali. Pia kukua kwake hakukwazi shughuli za sekta binafsi na maisha ya Watanzania wengi.

Deni hilo limezidi kuongezeka kutokana na serikali kuzidi kukopa kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati na  kushuka mara kwa mara kwa thamani ya shilingi dhidi ya dola ya Marekani.

Septemba mwaka 2005 dola moja ilikuwa sawa na Sh za Tanzania 1,302.7, wakati thamani yake rasmi kwa mwezi uliopita ilikuwa Sh 2,289.4 sawa na ongezeko la asilimia 75.7. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi wa BoT, Dk. Suleiman Missango, viashiria vyote vinavyotumika kupima uhimilivu wa deni vinaonyesha kuwa Tanzania iko vizuri. Mtaalamu huyo pia aliliambia JAMHURI kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya  deni la taifa na deni la serikali.

“Kuna tofauti kati ya deni la taifa na deni la serikali. Deni la taifa linajumuisha deni la serikali (deni la ndani na nje) na deni la nje la sekta binafsi. Deni la nje la serikali linajumuisha pia deni la taasisi za serikali,” Dk. Missango amesema.

“Deni la taifa lilikuwa  dola za Marekani milioni 28,313.6 mwezi Septemba 2019. Deni la nje la serikali na sekta binafsi lilikuwa dola za Marekani milioni 22,171.9. Deni la ndani la serikali lilikuwa sawa na dola za Marekani milioni 6,141.7(Sh bilioni 14,060.8),” mtaalamu huyo aliliambia JAMHURI na kuongeza:

“Deni la serikali lilikuwa dola za Marekani milioni 23,311.2, likijumuisha deni la nje dola za Marekani milioni 17,169.5. Deni la nje la sekta binafsi lilikuwa dola za Marekani milioni 5,002.4.”

Kati ya sababu ambazo wataalamu wa fedha na uchumi wanadai zimechangia kwa kiasi kikubwa kulifanya deni la Tanzania kuwa himilivu kwa muda mrefu ni sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya “dawa ya deni n kulipa.” Tangu iingie madarakani miaka minne iliyopita, serikali imetekeleza mkakati wa makusudi wa kulipa madeni yake.

Akiwasilisha utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2018/19 bungeni hivi karibuni, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema katika kipindi hicho serikali ilitoa jumla ya Sh bilioni 7,701.7 kwa ajili ya kulipia kwa wakati deni kuu na riba kwa mikopo ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Na wakati anachambua mafanikio ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kwa kipindi cha 2016/17 hadi robo ya kwanza ya 2019/20, Dk. Mpango alisema hadi Septemba 2019 serikali ilikuwa imelipa jumla ya Sh bilioni 24,499.2 kwa ajili ya deni lililoiva la fedha zilizokopwa kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. 

Pamoja na uhimilivu wake, kuna wadau wanataka kuongezeka kwa deni la taifa kudhibitiwe tena kwa sheria. Mbunge Sophia Mwakagenda wa Chadema aliliambia Bunge katika kikao chake mwezi uliopita kwamba sheria hiyo iwe ya kuibana serikali isikope kiholela.

Alidai kuwa lugha za kisomi kwamba deni ni himilivu hazina tija wakati linazidi kuwa kubwa.