Serikali ni chombo cha utawala chenye kusimamia kanuni na sheria za nchi na kuhakikisha zinafuatwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi iliyokubaliwa na wananchi. Chama cha siasa ni chombo cha uongozi, chenye kushughulika na masuala ya kuhamasisha, kuelimisha na kuona wananchi wanakuwa waaminifu kwa serikali na nchi yao.
Kwa mtazamo wa haraka haraka unaweza kuona ni vyombo viwili tofauti vinavyokinzana katika kushughulikia usalama na amani, utiifu na uaminifu kwa wananchi, kutokana na kauli na matendo yao, dhidi yao wenyewe kwa wenyewe katika kuwatumikia wananchi.
Kumbe katika mtazamo wa subira na umakini vyombo hivi ni vimoja vinapowatumikia wananchi katika kupata mahitaji yao, usalama wao, maendeleo yao na uchumi wao kwa amani. Hasa pale chama cha siasa kinapojitengenezea serikali yake kupitia uchaguzi huru wa taifa.
Serikali ambayo ni ya watu kwa ajili ya watu na kwa manufaa ya watu, ina wajibu wa kutunza usalama wa watu na mali zao, na kusimamia kanuni na sheria zilizowekwa na watu wenyewe. Katika utaratibu huu serikali inapata nguvu za kisheria kutawala kihalali.
Serikali yoyote haipendi wala haitaki kuona inapuuzwa, inahujumiwa au inadhalilishwa na raia wake au watu fulani ndani au nje ya nchi. Pindi ikitokea kufanywa hivyo, kwa nia ya kuvuruga usalama wa nchi, serikali huwa haisiti kuzima matukio. Nguvu hutumika.
Kwa vile chama cha siasa ni chombo cha uongozi, hufanya kazi ya kuhamasisha na kuelimisha watu kuhusu itikadi yake pia kuelezea sera na mipango ya serikali. Kina wajibu mkubwa pia wa kujenga umoja wa taifa, usawa wa hali za watu na haki inapatikana kwa wananchi.
Katika nchi huru na inayotekeleza demokrasia ya ukweli iliyoridhiwa na wananchi, chama cha siasa kina jukumu la kudhihirisha kwa umma wa watu kwa kauli na matendo utekelezaji wa demokrasia. Katika kupata wanachama, viongozi wa chama na serikali.
Serikali huwekwa madarakani na chama kilichoshinda uchaguzi halali baada ya kuvishinda vyama vingine katika kuwania nafasi hiyo. Vyama vilivyoshindwa vinakuwa ni chachu, washauri na washiriki katika utekelezaji wa mipango na sera za serikali iliyoko madarakani.
Katika falsafa hii ya uchachu, ushauri na ushiriki, vyama vya siasa na serikali havipaswi kila kimoja kuwa ni chombo cha kukomoa, kukinza au kusaliti chombo chochote katika harakati zake. Chombo kikifanya ubaya au hiyana dhidi ya kingine, nchi huingia matatani. Amani inapotea na kuirudisha si rahisi.
Mwanaharakati awe katika chama au serikali anahitaji mabadiliko katika chama chake au katika serikali yake, kuleta maendeleo ya watu kwa kupitia pia ujenzi wa vitu bora na imara kuwa nyenzo za kuharakisha kupatikana maendeleo. Maendeleo ya watu yanakwenda na maendeleo ya vitu.
Aidha, ibainike kwamba sifa moja wapo ya mtu huru katika nchi huru ni kusema ukweli. Na ukweli daima unahitaji uthubutu. Chama cha siasa au serikali inahitaji uthubutu na ukweli kuleta mabadiliko baada ya kuona tulikotoka, tulipo na tuendako.
Harakati zinazofanywa hivi sasa na Serikali ya Tanzania na kukubalika na baadhi ya vyama vya siasa ni kutaka kuleta mabadilko ya kweli katika nchi yetu. Hali hii inatokana na ujuzi, hekima na upendo wa viongozi wetu waaminifu. Ni busara na wajibu sisi wananchi kuwemo katika harakati hizi.
Ninaposema haya sina nia kuwatia hofu watu na wanaharakati wa siasa na serikali, mbele kuna mauti, la hasha! Kufa ni lazima wote tutakufa. Lakini mtu unakufa katika hali gani? Kuleta chokochoko katika nchi watu wafe hiyo haikubaliki na ni dhuluma ya nafsi, na laana kwa Mwenyezi Mungu.
Watanzania wenzangu tujitambue sisi ni watu wema waungwana na wakarimu. Tusikubali kutiwa hofu na watu wachache na tukajengewa mazingira ya uasi tukatumbukia shimoni. Tafadhali zingatia msemo huu: “Mwacha kwao ni muasi, aendako hana kiasi.”