Historia yangu inakwenda mpaka nilipoanza kuaminiwa kusoma na kuandika katika madaftari na vitabu vikubwa kama mkeka. 

Nilivipenda vitabu kwa hadithi zake na kuandika kwa kuchora vizuri na kusifiwa na masista ambao walikuwa walimu wangu. Ni katika kipindi hiki ndipo nilipogundua wengi wetu tulikuwa tunalingana tabia isipokuwa tofauti ilikuwa katika kubadilika.

Nikahitimu darasa la nne na tukawa wahitimu muhimu kwa maendeleo ya vijiji vyetu na kuwafundisha wengine. Vuguvugu la uhuru likaja baada ya miaka michache na tukajiunga kupambana na mkoloni. Jitihada zetu kubwa ilikuwa kuwaelewesha wazazi wetu ambao waliamini katika utumwa na uchifu, tulifungua madarasa ya ngumbaru na tukageuka masista wa kufundisha wazazi wetu.

Niliahidi nitaendelea na simulizi yangu ya maisha yangu katika kitabu changu kidogo kutokana na majukumu ambayo nimeyafanya na nafasi ambazo nimezitumikia katika taifa langu. Najua si haba, lakini mwisho nitawauliza vijana, wao wana nini cha kusimulia katika maisha yao?

Lengo si kuwakatisha tamaa, lakini ninataka wajue kwamba tunapaswa kuandika historia za maisha yetu kwa faida za kizazi kijacho. Najua kabisa wapo watu katika vitabu vyao hawatakuwa na mahali panapozungumzia mchango wao katika taifa au jamii. Historia itakuwa alizaliwa, akafanya ujanja ujanja akafungwa, akatoka, akafungwa, akakata rufaa, akafungwa maisha.

Nirejee katika historia yangu. Wazazi walikwa wagumu kidogo kuwafundisha kutokana na umri lakini sera ya ufundishaji ilikuwa si nzuri. Nahisi ilipaswa tuhamishane vijiji sisi wachache ambao tulikuwa masista. Haikuwa kazi rahisi kumfundisha baba mzazi au mama mzazi, haikuwa rahisi kumshikisha kalamu mjomba au shangazi. 

Waliona kama tunawadharau. Lakini kubwa zaidi ilikuwa muda wa masomo yenyewe, ilikuwa ni jioni ya saa kumi baada ya kazi na ndio muda ambao wengi walikuwa wakipumzika na kupata kinywaji kidogo, lakini alilazimika kuacha hayo yote ili aje darasani chini ya mti. Nadhani mtaelewa jinsi ambavyo walimu tulikuwa na wakati mgumu.

Tulipambana na hali hii mpaka mwishoni mwa mwaka ule wa Uhuru, kisha tukaanza rasmi ndani ya mfumo wetu. Tuliweza kubadilishana walimu kutoka eneo moja kwenda jingine. Zoezi hili la masomo ya ngumbaru lilibadilisha kabisa kiwango cha watu wanaojua kusoma na kuandika katika nchi za Afrika na kuwa katika nafasi za mwanzo kabisa, tulijisikia fahari sana kama walimu.

Vilipoanzishwa vijiji vya ujamaa kabla ya kuamua kuvunja mitaa mingine na kuja na mfumo wa sogeza miaka kumi na mitatu baada ya Uhuru, ninakumbuka nilikuwa mikoa ya kusini kwa majukumu yale ya mwalimu wa kujitolea. Tayari nilikuwa na familia kutoka katika eneo ambalo nililowea kwa muda nikifundisha kusoma na kuandika.

Vijiji vilipokuwa tayari ulianzishwa ushirika wa pamoja, shamba la pamoja, duka la pamoja, mifugo ya pamoja, gari la pamoja na uongozi wa pamoja, sisi wasomi wachache tulipewa majukumu mbalimbali. 

Nakumbuka kwa mara ya kwanza nilikuwa meneja wa duka la kijiji chetu.

Kazi yangu kubwa ilikuwa kufanya tathmini ya bidhaa ambazo zinahitajika katika eneo letu, kuagiza bidhaa kutoka katika shirika la ugawaji wakati huo, kukokotoa gharama na kuweka faida kidogo ili duka lipate faida.

Nakumbuka vizuri kwamba kijiji kiliniamini na kunitaka nifanye kazi hiyo bila malipo. Hivyo hivyo muuzaji wetu hakulipwa chochote. Tuliamini kazi nyingi zilikuwa za kujitolea kwa kuwa nyingi tulifanya baada ya muda wa kazi za kilimo na ufugaji, maduka yalikuwa yakifunguliwa jioni saa kumi baada ya kazi.

Duka likawa kubwa ambapo ungeliweza kupata huduma zote kama vibatari, taa za kandili, pini, sindano, viberiti, rula, kalamu, vikombe, bahasha, air form, stempu, mafuta ya kujipaka, sabuni, utambi, majani ya chai, chumvi, vitambaa vya jora vya Marekani, sindano za kufuma, uzi wa cherehani, khanga na vitenge, uzi wa kufuma vitambaa na bidhaa kedekede ambazo leo hazipo kabisa.

Kijiji kikawa na imani nami na kuamua kwa kauli moja katika mkutano wa hadhara kuwa niwe meneja wa duka na basi la kijiji. Hapo changamoto zilianza kujitokeza, kwa kuwa nilipaswa kuwa kiongozi wa basi letu pia liwapo safarini na wakati huohuo nikirejea niwe ninapitia mahesabu na dukani na kuagiza bidhaa ambazo zimepungua. Hivyo kamati ya maendeleo ya kijiji ikatangaza kuniajiri na mshahara wangu ulikuwa Sh mia moja na kumi na tano kwa mwezi.

Mwanga wa maisha bora kwangu na kijiji ukaanzia hapo.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.