Haben Girm ni mwanamke aliyezaliwa akiwa haoni wala kusikia.  Haben Girm alizaliwa katika familia maskini sana.  

Haben alipozaliwa akiwa haoni wala kusikia watu walimshauri mama  yake amtupe kichakani. Mama yake alikataa  kata  kata. Mama yake alisema: “Siwezi  kumtupa  mtoto wangu kichakani kisa ni kipofu.”  

Haben alikulia katika mazingira magumu sana. Kila mtu, wakiwemo ndugu, jamaa na marafiki walimtazama Haben kama  hasara katika familia yake. Kitu kimoja ambacho watu wengi walikuwa hawakifahamu ni kuwa Haben alikuwa na ndoto  ya kuwa mwanasheria. 

Siku moja Haben alimwambia kaka yake: “Nitakuwa mwanasheria na hiyo ndiyo ndoto yangu.”  Kwa  haraka  kaka  yake  alimjibu: “Hapana. Hauwezi kuwa mwanasheria. Wewe ni kiziwi na  kipofu”.  Haben  alimjibu  kaka yake kwa  kusema: “Udhaifu wangu hauwezi  kunizuia kuwa  mwanasheria.”  

Ndoto ya Haben kuwa mwanasheria ilitimia. Mwaka 2005  Haben alitunukiwa shahada ya sheria kutoka Chuo  Kikuu cha  Harvard cha nchini Marekani. Lisilowezekana  linawezekana.

Watu  unaowafahamu wanaweza wakawa ndio maadui wako wa kwanza katika maisha yako. Ndoto ya Haben  kuwa mwanasheria ilitaka kuzimwa na kaka yake. Kamwe katika maisha,  usikubali  watu  wautumie  udhaifu  wako  kama  kigezo cha kuizima ndoto yako. Usiruhusu  mazingira magumu ya sasa yaue  ndoto  yako  ya  kesho.  Kila ndoto  kubwa  ina  mashambulizi  makubwa.  Ilinde sana ndoto yako.

Watu wote huota ndoto. Kuna ambao  wanaota ndoto wakiwa  wamesinzia lakini kuna ambao wanaota ndoto  wakiwa  macho.  Ndoto  ni  maono.  Ndoto  ni  kesho  yako.  

Katika karne ya 19 ndugu wawili walikuwa na wazo ambalo liligeuka kuwa  mbegu  ya  ukweli.  Ndugu  hao  ni  Orvile  Wright na Wilbur Wright wa Marekani. Wakiwa vijana mwaka 1896 walikuwa ni mafundi wa kutengeneza baiskeli. Mwaka 1899 walifanya jaribio la kurusha tiara. Wakapata wazo la kutengeneza chombo kinachoweza kuruka angani. Walifikiria kutengeneza meli ya angani. Walichekwa sana.  

Wazo la kurusha ndege angani walianza nalo mwaka 1899 kwa kufikiria namna ambavyo rubani  anaweza  kurusha  ndege  angani na asianguke kama vile mtu anavyoweza kuendesha baiskeli na asianguke. 

Gazeti la New York Times la nchini Marekani la  mwaka 1903  liliripoti  kwa  kusema: “Wanasayansi  wasipoteze  muda  na pesa kwa majaribio ya chombo cha angani.”  Wiki  iliyofuata ndugu hao walifanikiwa kurusha ndege angani.  

Ajabu ni kwamba, ndugu hawa hawakuwa na shahada ya chuo kikuu chochote. Hii ndiyo nguvu ya kung’ang’ania  maono. Katika safari ya mafanikio, njiani utakutana na watu ambao watakucheka kama Orvile  Wright na  Wilbur  Wright  walivyochekwa. 

Wengine watakuona kama mwendawazimu. Usiogope kuchekwa. Endelea kuchapa kazi. Endelea kutimiza  malengo uliyojiwekea katika maisha yako.  Endelea  kuitengeneza kesho yako.

Mafanikio ya kweli nyuma yake na mbele yake kuna maadui unaowafahamu na usiowafahamu. Jijaze ujasiri wa  kupambana  na maadui hawa. Usiwakimbie. Kabiliana nao. Watu wengi wameshindwa kutimiza ndoto  zao,  kwa  sababu  wengine walikatishwa tamaa na  watu na wao wakakubali kukata tamaa. Nguvu  uliyonayo ni  kubwa kuliko nguvu  inayotoka kwa maadui wako.  Unapokubali kukata tamaa, unakuwa umekubali kuua nguvu kubwa ya maono  iliyoko ndani yako.

Naomba  kukufundisha jambo hapa.  Haijalishi unafanya kazi au hufanyi kazi, ni  lazima watu watakusema tu.  Bila  kujali  wewe ni mwema kiasi gani, lazima kutakuwa na watu ambao watakushambulia.  Bila kujali wewe ni mkimya kiasi gani,  lazima utakutana na watu wa kukutungia  maneno.   

Kazi ya mdomo ni kusema.  Usiogope kusemwa.  Kwa mfano: Mtu akiwa mkarimu kuna watu watakaojitokeza  na  kusema: “Anajitangaza.” Asipokuwa mkarimu watasema: “Ana gundi vidoleni.”  Mtu  akitoa  hotuba fupi sana, kuna  watu watajitokeza na kusema: “‘Hakujiandaa.”  Akitoa hotuba ndefu watasema:  “Hajui kutunza muda.”  

Akiwa mtoto mchanga watasema ni ‘Malaika’. Akiwa mtu mzima watasema:  “Achana  na  yule shetani.” Akiwa  mcha  Mungu watasema: “Ni Mkatoliki zaidi ya Papa.”  Asipokuwa mcha Mungu wanasema: “Shetani amemweka mfukoni.”  Akiaga dunia katika umri mdogo watasema:  “Angefanya mengi mazuri.”  Akifikia umri wa uzee watasema:  “Miaka yake  aliiharibu tu bila kufanya chochote.”  

Ndoto yako isiongozwe na maneno ya watu.  Acha wakuseme wawezavyo lakini wewe pambana kutimiza ndoto yako.  Acha leo wakuone kichaa ili kesho wakushangae.