Huu ni mpango mahsusi wa kuharibu utalii wa Tanzania na kuvutia watalii katika mbuga ya Maasai Mara nchini Kenya.
Wakenya wamejipanga hata katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa Wakenya wanaoishi katika vijiji vya Ololosokwan, Soit Sambu, Arasha, Maaloni na Magaiduru wanachaguliwa kushika nafasi za wenyeviti wa vijiji na wajumbe wa Serikali za Vijiji ili kulinda maslahi yao ya kupata ardhi ya makazi na machungio ya mifugo yao.
Wanachanga hela nyingi kuunga mkono wale watu wao wanaowataka. Katika Kijiji cha Ololosokwan wanamtaka Esofio. Huyu ni Mkikuyu wa Olnderekesi Narok, Kenya. Ni kaka yake Kundai Parmwatt, aliyewahi kuwa Diwani wa Kata ya Soit Sambu kwa kipindi kirefu.
Hapa kunapaswa kuchukuliwa hatua za haraka na za makusudi maana wakipata tu hizo nafasi watajaa kuliko walivyo sasa.
Katika Mji wa Wasso, Wakenya wengi wamenunua viwanja, wamejenga nyumba za kuishi na wanafanya biashara kinyume cha Sheria ya Ardhi inayozuia wageni kumilikishwa ardhi bila kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Uamuzi mwingi unaofanywa katika halmashauri, ngazi ya wilaya na vijiji, unakuwa influenced na Wakenya kupitia mawakala wao wa mashirika yasiyo ya kiserikali na madiwani ambao ni watumishi wa mashirika hayo. Asilimia 60 ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ni watumishi wa mashirika hayo.
Hizi NGOs zinafadhiliwa na watu mbalimbali wakiwamo kutoka Kenya. Ajenda yao kubwa ni kupata ardhi upande wa Tanzania ya kuishi na kuchunga mifugo yao.
Katika Kijiji cha Ololosokwan eneo la Sero na Oloirien wamejaa Wakenya na wanalindwa na mbuge mmoja wa zamani kwa maslahi binafsi. Anapewa ng’ombe na kuchangiwa fedha.
Ndani ya Mbuga ya Taifa ya Serengeti maeneo ya Lemugur, Ilmolelian na Irpalakika wamejaa ng’ombe wa Kenya. Kinachofanyika ni kwamba Wakenya wanachanga pesa na kuwapa ma-park rangers ambao wanawaruhusu kuchunga ndani ya Hifadhi. Hili suala siyo siri tena. Wanachunga na Serikali haifanyi lolote. Katika ziara ya Waziri Mkuu alipopita katika Kijiji cha Maaloni, Masai Joseph Parsambei alimwambia kuwa kulingana na ukame ng’ombe wao wanachunga ndani ya Hifadhi ya Serengeti.
Pia Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, katika majumuisho alikiri kuona ng’ombe ndani ya Hifadhi ya Serengeti waliporuka na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Lazaro Nyalandu.
Katika kikao cha hivi karibuni Ngorongoro, Diwani wa Arash, Mathew Siloma, alimwambia Nyalandu kuwa mifugo yao wanachunga ndani ya Serengeti; hivyo siyo siri tena kuwa ng’ombe wa Kenya wamo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Utalii nchini Kenya
Hivi karibuni biashara ya utalii nchini Kenya ilizorota kwa kiwango kikubwa kutokana na mashambulizi ya Al Shabaab na ugonjwa wa ebola uliosadikiwa kuingia. Kwa sababu hiyo, mbuga zetu zilipata kiasi kikubwa cha watalii. Baada ya Wakenya kuona hivyo walipanga mpango mkakati wa kufanya uhifadhi usio wa kawaida. Walianzisha kitu kinachoitwa Community Conservancies katika jamii zile ambazo zinazunguka Hifadhi ya Maasai Mara. Waliwahamasisha watunze maeneo yao na wala wasiharibu mazingira.
Walioonekana kutunza kwa bidii Serikali iliwapa ruzuku. Sasa wale Wamaasai walichofanya walihamishia ng’ombe wao ndani ya Serengeti na eneo la mpakani la Ilmasilig na katika Kijiji cha Sero. Waliweza kufanya hivyo kwa kusaidiwa na mawakala walio katika NGOs; mfano ni mtu mmoja Ngoitiko. Huyu amejikatia eneo la karibu ekari 3,000 katika Ilmasilig na kuweka uzio. Mbunge wa zamani, Timan, naye ana eneo kubwa karibu na Klains Camp. Pia alijikatia eneo la ekari 100 karibu na Shule ya Sekondari ya Wasso. Hata nyumba anayoishi iko ndani ya eneo ambalo bila shaka lilipaswa kuwa la Sekondari ya Loliondo. Shule haina kiwanja cha michezo wala eneo la kufanya mafunzo kwa vitendo kama vile kilimo cha bustani kwa kuwa eneo kubwa limechukuliwa.
Mwingine amejikatia mlima mmoja katika Kijiji cha Ololosokwan. Naye anasema ni lake. Watu wanawaingiza Wakenya nchini kulisha mifugo yao na ushawishi wao katika makabila ya Purko na Loitai wanaoishi katika vijiji vya Arash, Maaloni, Magaiduru (Loitai), Ololosokwan, Soitsambu (Purko).
NGOs ambazo zinapata msaada wa moja kwa moja kutoka kwa Wakenya ni PWC (Pastoralist Women Council). Viongozi wao ni wazaliwa wa vijiji vya Arasha na Soitsambu.
Hii NGOs imewaunganisha wazee wa kimila (Malaigwanani) wa Purko na Loitai walioko Tanzania na Kenya kuweka mikakati ya mambo mengi. Ina pesa nyingi sana. Imekuwa ikihamasisha maandamano ya kudai ardhi na kulalamika kuwa wanaonewa mambo mengi.
Ngorongoro kuna watu wanatumia sheria ya Kenya kudai ardhi Tanzania, ndiyo maana hata Balozi Khamis Kagasheki alipotaka kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi Loliondo, ilishindikana kwa kuwa Wamaasai ambao wengi ni Wakenya walipiga kelele na wakaungwa mkono na wabunge — kina Christopher ole Sendeka; Nangoro na Lekule Laizer. Hawa nao ni wafugaji. Kwa hali ya sasa ya ng’ombe kujaa ndani ya Serengeti sijui watakuwa na lipi la kusema.
Zamani kabla ya Sheria ya Ardhi Namba 4 & 5 ya 1999 vijiji vya Kata ya Loliondo na Sale vilipimwa na NGO inayoitwa ADO iliyokuwa ikifadhiliwa na Shirika la Kikatoliki mwaka 1988. Vijiji vilipata hatimiliki. Lakini ikaonekana ni makosa maana kama kijiji kikiwa na hati ina maana mtu mmoja anaweza akauza kijiji chote. Serikali ikaona upungufu huo wakati wa Edward Lowassa alipokuwa Waziri wa Ardhi. Sheria Mpya ya Ardhi ya Vijiji ya 1999 ikafuta hizo hatimiliki na ikataka vijiji vipewe vyeti tu.
Kama kawaida, vijiji vya Ngorongoro vikiwa na ushawishi wa NGOs vikagoma kurudisha. Hata hivyo, hata kama hawakurudisha, lakini sheria imeshazifuta, hazina maana. Vijiji viwili vya Ololosokwan na Engaresero wao wakarudisha na vikapewa vyeti vya vijiji. Hivyo ni vijiji viwili tu ndiyo vyenye vyeti.
Hata hivyo, hivi karibuni Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kupitia ofisi yake ya Kanda ya Kaskazini iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro, iliona pia kuwa ni makosa vijiji kuwa na vyeti katika Pori Tengefu ambalo Sheria Namba 4 ya Ardhi imeweka katika kundi la ardhi ya uhifadhi. Hivyo wametakiwa kuvirudisha hivyo vyeti vifutwe hadi mpango madhubuti wa matumizi bora ya ardhi utakapotekelezwa.
Ni lazima ardhi hiyo ihaulishwe, itoke katika ardhi ya uhifadhi na kuwa katika matumizi mengine kama ardhi ya vijiji, ardhi ya wazi na kadhalika. Hadi sasa ardhi ya Loliondo ni ardhi ya uhifadhi (reserve land) na mipango mbalimbali ya kufanya matumizi bora ya ardhi kama Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya 2009 inavyoelekeza, waziri mwenye dhamana ya wanyamapori na ardhi kufanya imeshindikana kutokana na harakati za Wakenya kupitia NGOs zipatazo 33 zilizo katika Wilaya ya Ngorongoro pekee.
Ajenda yake ni kuwatafutia Wakenya ardhi ya makazi na ya kuchunga. Kuna kitu kimoja wazawa wote wa nchi hii kwa ujumla wetu tunajua, ila makabila ya Purko na Loitai ambao asili yao ni Kenya hawajui na mara nyingi wanatumia sheria za Kenya humu humu Tanzania na wakati mwingine huandamana hadi Ikulu.
Kitu chenyewe ni kwamba ardhi yote hapa Tanzania ni mali ya umma. Msimamizi mkuu ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huapa kuilinda anapoingia madarakani. Mtu yeyote akipata hati ya kumiliki ardhi au kijiji kikipata cheti huo ni mkataba kati ya mmiliki na Serikali kupitia wizara husika na kwa masharti na muda utakaokuwa umeoneshwa katika hati hiyo mara nyingi ni miaka 33, 66 au 99.
Kama hujatimiza masharti kama ya kutolipa pango la ardhi husika kwa muda mrefu Serikali inaweza kukunyang’anya na kummilikisha mtu mwingine. Kama miaka uliyopewa kumiliki imeisha na hujaomba tena, Serikali inayo mamlaka ya kumpa mtu mwingine.
Ni tofauti na jirani zetu Kenya ambako ardhi ni mali ya mtu binafsi. Unaweza ukakuta watu wawili tu wenye uwezo wamemiliki wilaya nzima na wamezungusha waya – ng’ombe akikanyaga au mtu anakuwa ame-tress pass. Anaweza kupigwa risasi au kama ni mfugo unaweza kutaifishwa.
Wafugaji yaani Wamaasai wa makabila ya Loitai na Purko wanahamahama kutafuta malisho. Baada ya kukosa eneo la kwenda wakaamua kwenda kwa ‘shamba la bibi’ – Tanzania. Wameingia ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Nao wameanza kujikatia maeneo ndani ya Tanzania.
Dhana ya Wamaasai wa Purko na Loitai kusema ardhi yetu…ardhi yetu ni sheria ya Kenya; siyo ya Tanzania. Wanaoandamana Loliondo hadi Ikulu ni Purko na Loitai, Wakenya wakihamasishwa na NGOs za PWC, UCRT na NGONET. Baadhi ya viongozi wao ni Sinandei Mako, Maanda Ngoitiko na Samwel Naingiria.
Wao watoto wao wanasoma katika shule nzuri nzuri huku Wamaasai wa kawaida wakiwa katika umaskini wa kutisha. Watoto wao na ndugu zao hao wenye NGOs wanasoma international schools, watoto wa Kimaasai wenye umri wa kwenda shule hawaendi. Wanachunga ng’ombe na kondoo. Hakuna NGO inayohamasisha watoto machungani waende shule. Wao ni advocacy, conflict resolution, lands right for Maasai. Wamaasai wa Loliondo ndiyo huwa wanaonewa na wanahitaji NGO 30 kuwatetea wakati idadi yao kulingana na sensa iliyopita ni 180,000!
Kwenye maandamano ni vigumu kuwaona Wasonjo au Wamaasai wa kabila la Laitayok. Hao ndiyo wazawa na wanajua hao Purko wamekuja lini Tanzania wakitokea Narok, Kenya. Wanajua wanaishi wapi hapa Loliondo. Wanajua yote hayo na wanathubutu kusema waache Purko na Loitai waandamane maana wao Laitayok wanasema wanafuata sheria na taratibu nchini kama Watanzania wengine.