Mbinu za ukwepaji kodi unavyofanywa na kampuni za bilionea Mmarekani, Friedkin, zinazidi kufichuka baada ya kubainika kuwa kwa miaka zaidi ya 30 serikali imekoseshwa mabilioni ya shilingi kupitia udanganyifu kwenye mishahara.

Akaunti maalumu kwa mpango huo zimefunguliwa ughaibuni na kutumika kuingiza fedha nyingi huko, na nyingine chache ndizo zinazolipwa hapa nchini.

Kundi la kampuni za Friedkin nchini Tanzania linamilikiwa na bilionea raia wa Marekani, Dan Friedkin; ambaye sehemu kubwa ya utajiri wake inatokana na biashara ya magari ya Toyota katika majimbo ya Oklahoma, Arkansas, Mississippi na Louisiana nchini Marekani.   

Nchini Tanzania, kampuni zake ni Tanzania Game Tracker Safaris Ltd (uwindaji wa kitalii), Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Ltd (uwindaji wa kitalii), Ker & Downey Safaris (Tanzania) Ltd (utalii wa picha), Northern Air Ltd (usafiri wa anga), Mwiba Holding Ltd (ranchi ya wanyamapori na utalii) na The Friedkin Conservation Fund (uhifadhi na maendeleo ya jamii).

Kikosi Kazi kilichoundwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kimebaini mwanya wa ukwepaji kodi ambao ni kupitia malipo ya mishahara na marupurupu manono wanayolipana wawekezaji hao.

Kwa kutumia akaunti zilizofunguliwa nje ya nchi (offshore accounts), Friedkin wanatuhumiwa kutumia kigezo cha kuajiri wataalamu wa kigeni ili kukwepa kodi. Mwaka 2008 fedha zilizowekwa kwenye akaunti hizo kwa mbinu hiyo ni dola 963,879 za Marekani. Kwa kiwango cha sasa cha kubadilishia fedha cha wastani wa dola moja ya Marekani kwa Sh 2,300; hiyo ina maana mwaka huo fedha zilizohamishwa kwa mbinu hiyo ni Sh bilioni 2.216.

Mwaka 2009 dola 849,109 za Marekani (Sh bilioni 1.952) za mishahara ziliingizwa kwenye akaunti hizo; na mwaka 2010 kiwango hicho kilikuwa dola 578,798 za Marekani (Sh bilioni 1.331). Hii ina maana kwa miaka mitatu pekee kiwango cha fedha kilichohamishwa bila kukatwa Kodi ya Ajira (PAYE) na Kodi ya Uendelezaji Ufundi Stadi (SDL) ni Sh bilioni 5.499 ambazo kwa miaka 33 ni Sh bilioni 181.467.

Akaunti hizo zimefunguliwa katika Visiwa vya Cayman, Cyprus, Mauritius na Uswisi. Kampuni ya Kitanzania (jina tunalo), imekuwa ikishirikiana na kampuni nyingine za kimataifa kufungua akaunti mbalimbali za wafanyakazi wa kampuni za Friedkin. Baadhi ya washirika hao ni CIM Corporate Services iliyopo Mauritius.

Mambo mengine yaliyodaiwa kufanywa na kampuni za Friedkin ni ubaguzi wa mishahara kati ya wafanyakazi wageni na wenyeji bila kujali uwezo wao kitaaluma. Wafanyakazi wageni wanalipwa kiasi kidogo cha fedha hapa nchini, ilhali kiwango kikubwa kikiwekwa kwenye akaunti zao zilizofunguliwa ughaibuni.

Mkurugenzi Mkuu, Jean-Claude McManaman anapokea mshahara wa Sh milioni 50 kwa mwezi. Mkurugenzi wa Operesheni wa Mwiba Holdings Limited, Russel Hastings analipwa mshahara wa Sh milioni 49 kwa mwezi. 

Sehemu kubwa ya mshahara huo haikatwi kodi kwa kuwa huingizwa moja kwa moja kwenye akaunti zilizoko ughaibuni. Ofisa Mkuu wa masuala ya Fedha wa Kerr & Downey Limited, Nick Stubbs mshahara wake ni Sh milioni 43.

“Jambo la kusikitisha ni kuwa sehemu kubwa ya mishahara hii inalipwa offshore, kwa hiyo haikatwi kodi wala tozo, lakini kwa wafanyakazi Watanzania ambao wanalipwa kidogo, kodi zote wanakatwa,” kimesema chanzo chetu.

Mchanganuo unaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 hadi mwaka huu (2019), Hasting pekee ‘amekwepa’ kodi ya wastani wa Sh milioni 840; na Stubbs ameikosesha serikali Sh milioni 744 kama kodi na tozo kutoka kwenye mshahara wake pekee.

Wakati wageni hao wakilipwa hivyo, kwa Watanzania walio kwenye ngazi ya umeneja mshahara wa kila mmoja ni wastani wa Sh milioni 9 pekee kwa mwezi; na baada ya makato hubaki na wastani wa Sh milioni 5.

Wafanyakazi wa ngazi ya chini kama vile wahudumu wanalipwa mshahara wa wastani wa Sh 400,000 hadi Sh 800,000 kwa mwezi na wanakatwa kodi zote za PAYE, SDL na WCF. Pia wanakatwa NSSF. 

Vilevile imebainika kuwa kwa miaka yote 30 hakuna Mtanzania aliteuliwa kushika nafasi ya juu kwenye menejimenti ya kampuni za Friedkin hapa nchini.

Wawindaji Bingwa (PH) raia wa kigeni wanalipwa dola 12,000 za Marekani (Sh milioni 27.6) kwa mwezi; lakini ‘waswahili’ wanaambulia dola 1,000 za Marekani (Sh milioni 2.3) tu kwa muda kama huo.

Hivi karibuni kampuni za Friedkin zimetakiwa zilipe Sh zaidi ya bilioni 10 kama kodi iliyokwepwa kwa miaka kadhaa.

Kwa miaka yote hiyo, wafanyakazi wataalamu kutoka nje walioajiriwa na kampuni za Friedkin wamekuwa wakilipwa sehemu kubwa ya mishahara yao kwenye benki zilizo ughaibuni ili pamoja na mambo mengine, wasilipe kodi na tozo mbalimbali za kisheria.

Sehemu zinazotajwa kupelekwa fedha hizo ni Visiwa vya Bahamas kwenye taasisi za fedha za Adventure Services na AHIL Trust. Hayo yakiendelea, uchunguzi umeanza kwenye akaunti za Friedkin zilizoko Uswisi na Visiwa vya Cayman.

Wanaotajwa kuwa wanahusika kuidhinisha fedha kutoka ofisi kuu za Friedkin zilizoko Houston Texas, Marekani ni Rais wa kampuni za Friedkin, Dan Friedkin; Mtendaji Mkuu, Marcus Watts; na Mwanasheria Mkuu, Kimberly Jacobson.

Kutokana na tuhuma hizo, Kikosi Kazi kimewapoka baadhi ya wakurugenzi wa kampuni za Friedkin hati za kusafiria. Baadhi yao wameondoka nchini.

Oktoba 25, mwaka huu Kikosi Kazi hicho kilikutana na wawakilishi wa kampuni za Friedkin jijini Arusha. Kwa upande wa Friedkin, waliohudhuria ni Jean-Claude Mcmanaman, Lemmy Bartholomew, Wilfred Mawalla, Elibariki Lucas, Nick Stubbs, Russel Hastings na Alex Rechsteiner.

Taarifa kutoka kwenye kikao hicho zinasema kampuni za Friedkin zinatuhumiwa kwa makosa ya ukwepaji kodi kupitia malipo ya wakurugenzi; na ukwepaji kodi kwenye mikopo na uhamishaji fedha ndani ya kampuni.

Makosa mengine ni kuajiri wataalamu kutoka nje ya nchi wanaofanya kazi kama washauri, lakini wakiwa hawana vibali  wala sifa za kitaaluma; na imebainishwa kuwa baadhi ya wafanyakazi –wamekutwa wakiwa na mishahara zaidi ya mmoja na kwa viwango tofauti.  Pia hakuna makato kwa ajili ya mifuko ya hifadhi ya jamii.

Jingine ni mikataba mingi kwa wataalamu kutoka nje ya nchi, hasa kwa Jean-Claude ambaye amekutwa akiwa na barua ya ajira, lakini ana mkataba mwingine kama mshauri.

Kwenye kikao hicho, Friedkin waliomba wapewe hati zao za kusafiria kwa kile walichodai kuwa baadhi yao wana masuala ya kifamilia huko kwao na wengine wanakwenda katika matibabu na masuala ya kibiashara.

Walikwama kwa maelezo kuwa hilo litawezekana tu endapo watuhumiwa hao watakuwa tayari kuweka kiasi cha fedha kama dhamana.

Friedkin wakawa tayari kutoa Sh milioni 100 na baadaye Sh milioni 200, lakini Kikosi Kazi kikagoma kukubali ofa hiyo. Badala yake, wakaelezwa waweke dhamana ya Sh bilioni 5 kwenye akaunti maalumu ya serikali wakati majadiliano kuhusu kiwango halisi cha kodi kilichokwepwa kikikokotolewa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Friedkin Group Company Ker and Downey Tanzania Ltd., Jean – Claude McManaman, anatajwa kukiri baadhi ya tuhuma za ukwepaji kodi.

“Amekiri mengi tu, na taratibu za kuweka bondi ya Sh bilioni 5 zinaendelea. Kiwango hicho ni dhamana. Wanatarajia baada ya uchunguzi kiwango huenda kikawa kikubwa zaidi ya Sh bilioni 10 kwa sababu wanapitia taarifa za siri za kampuni zao kwenye benki za nje,” kimesema chanzo chetu kilicho karibu na Kikosi Kazi. 

Baadhi ya wakurugenzi walipeleka ujumbe mjini Dodoma kuonana na waziri mkuu ili kumuomba kiasi walichopendekeza kipokewe kama dhamana wakati taratibu nyingine zikiendelea.

Kwenye majadiliano hayo, Friedkin walitaka mwezao, Alex Rechsteiner, aondolewe kwenye orodha ya wakurugenzi walionyang’anywa hati za kusafiria kwa maelezo kwamba yeye si mkurugenzi, bali ni meneja.

“Walisema Alex ni meneja, kwa hiyo arejeshewe hati yake ya kusafiria, hilo likaonekana kama mbinu ya kumnyofoa kwenye sakata hili la ukwepaji kodi. Kikosi Kazi kiligoma,” kimesema chanzo cha habari.

Friedkin Group wanamtumia Mwanasheria Lemmy Bartholomew wa Kampuni ya Mawalla Advocates ya jijini Arusha.

Wakati wataalamu na wakurugenzi wa Friedkin wakizuiwa kusafiri nje ya nchi, ‘mshauri’ mkuu wa Friedkin Group, Fabia Bausch kutoka Chem Chem Safaris, yeye aliwahi na akafanikiwa kukimbilia nje ya nchi.

“Tuhuma za ukwepaji kodi zinazowakabili ni nyingi na kubwa. Ukiwarejeshea hati za kusafiria maana yake unasema hili suala limekwisha. Imani yetu ni kuwa kiasi cha kodi kilichokwepwa ni kikubwa kuliko hiki tulichokiona, kwa hiyo kuwaruhusu waondoke nchini maana yake ni kuharibu kazi yote iliyokwisha kufanyika,” kimesema chanzo chetu.

Wakati wakurugenzi wa Friedkin wakiwa huru licha ya kukabiliwa na tuhuma za ufisadi na uhujumu uchumi, wengine wenye tuhuma kama hizo wako rumande. Miongoni mwao ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Uwindaji wa Kitalii ya OBC, Isaack Mollel, aliyeko rumande tangu Februari, mwaka huu.

Licha ya ombi la Rais John Magufuli ambalo lilikubaliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) la kuingia makubaliano na washitakiwa ili waombe radhi, walipe fedha na waachiwe, Mollel na washitakiwa wengine wamefanya hivyo, lakini hadi sasa bado wako rumande.

Ugomvi wa vitalu vya uwindaji umetawala taarifa za uhusiano wa kampuni za Friedkin na kampuni nyingine za uwindaji wa kitalii. Tukio la karibuni ni la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangalla,  kutangaza kuifutia leseni Kampuni ya Green Mile Safaris (GMS) inayomilikiwa na raia wa Tanzania. 

Lakini kabla ya barua hiyo kutolewa kwa umma, ilianza kuonekana kwenye safu ya mtandao wa kijamii binafsi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ikiwa hata haina sahihi ya waziri mhusika.

Kumekuwapo taarifa za wazi kuwa GMS inapokwa kitalu hicho ili wapewe Friedkin kwa madai kwamba kilikuwa chao.

Taarifa za ndani zinasema viongozi wa Friedkin wako kwenye mvutano na baadhi ya viongozi waandamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kile kinachodaiwa kwamba ni kushindwa kwao kuwapa kitalu kinachomilikiwa na GMS kama walivyokuwa wamewaahidi.

Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ni miongoni mwa wanaotajwa kuwa marafiki wakuu wa Friedkin. Mwaka 2015 akiwa na wadhifa huo, alitumia helikopta za Friedkin kwenye kampeni zake za ubunge.

Nyalandu alihakikisha wanapata Hadhi ya Uwekezaji Mahiri (SIS) kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kutumia nyaraka zenye shaka. SIS ilitolewa na TIC kwa Friedkin siku moja [Agosti 20, 2015] na kuridhiwa siku hiyo hiyo na Nyalandu; kasi ambayo si ya kawaida kwa utendaji serikalini.

Familia ya bilionea Friedkin ilianza kuwekeza nchini Tanzania mwaka 1987 baada ya kununua Kampuni ya Ker & Downey Safaris (Tanzania) Limited (KDT) na Tanzania Game Tracker Safaris Limited (TGTS). 

KDT inajihusisha na utalii wa picha na TGTS ni ya uwindaji wa kitalii. Mwaka 1994, taasisi isiyolenga kutengeneza faida ya Friedkin Conservation Fund (FCF) ilianzishwa kwa kile kinachotajwa kuwa ni kufanya miradi ya maendeleo ya jamii na kuendesha operesheni dhidi ya ujangili katika vitalu kwa niaba ya TGTS.

Familia ya Friedkin imewekeza kwenye biashara ya ndege chini ya TGTS kuanzia mwaka 1992 na baadaye walitenganisha na kuanzisha Northern Air (NA) kama kampuni ya kibiashara ya usafiri wa anga mwaka 2005. 

Mwaka 2002, familia ya Friedkin iliinunua Wengert Windrose Safaris (Tanzania) Limited (WWS), ambayo ni kampuni ya uwindaji wa kitalii iliyoanzishwa mwaka 1985.

Mwaka 2007, Mwiba Holding Limited (MHL) ilianzishwa. MHL ndiyo iliyoanzisha Mwiba Wildlife Ranch na kuibua kelele kutoka kwa wahifadhi kuwa kisheria wakati huo ranchi haikupaswa kuanzishwa umbali wa kilometa sifuri kutoka hifadhi ya taifa.