Pamoja na kutoa mchango mkubwa katika ujenzi wa uchumi imara, benki zinazofanya biashara hapa nchini zimetakiwa pia kuchangia zaidi kwenye maendeleo binafsi ya Watanzania kupitia huduma bora na kuwekeza vyakutosha katika shughuli za kijamii.

Kwa mujibu wa wadau mbalimbali, benki na taasisi nyingine za fedha bado hazijatoa mchango unaostahili kusaidia wananchi wengi kujikwamua kiuchumi na kuwa na maisha bora.

Wadau wanabainisha kuwa taasisi za fedha zitasaidia kuinua maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha huduma zao zinapatikana kirahisi na kwa haraka na kwa gharama nafuu wakati wowote na mahali popote.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya NMB wilayani Ubungo, jijini Dar es Salaam hivi karibuni, wadau hao walisema pia ubunifu wa hali ya juu unahitajika kupanua wigo wa huduma za kifedha na kibenki ili wananchi wengi wanufaike nazo.

Eneo jingine litakalosaidia benki kuchangia kuleta neema haraka kwa wananchi ni kwa taasisi hizo kuwekeza katika teknolojia za kisasa hasa zile za kidijitali kupitia Tehama.

Huo pia ndio mtazamo na matarajio ya serikali na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) chini ya uongozi wa Gavana Prof. Florens Luoga. Kutokana na unyeti wake, suala hili lilikuwa miongoni mwa mada kubwa wakati wa Mkutano wa 19 wa Taasisi za Fedha nchini uliofanyika kwa siku mbili Dar es Salaam wiki iliyopita.

Katika hotuba yake akifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais John Magufuli, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisisitiza umuhimu wa kupanuliwa kwa huduma za fedha ili kuwafikia wananchi wengi hasa vijijini. Alisema sekta ya fedha ambayo ni wezeshi ni ile yenye wigo mpana wa bidhaa na huduma za aina mbalimbali zinazopatikana kwa gharama ambazo wananchi wengi wanazimudu.

Naye Prof. Luoga alisema mchango wa benki na taasisi nyingine za fedha kujenga nchi na ukuaji wa uchumi lazima ijumuishe huduma za uhakika kwa wananchi. Alisema Benki Kuu imekuwa ikisisitiza upatikanaji wa huduma karibu na wananchi na kuzipongeza taasisi zote zinazoendelea kufanya hivyo kupitia matawi, mawakala na njia mbadala za utoaji huduma za fedha kielektroniki na kupitia simu za mikononi.

Wakati wa ufunguzi wa Tawi la NMB Mbezi Louis, mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori, alisema upatikanaji wa huduma za kibenki ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kuwaletea watu maendeleo hasa zinapokuwa karibu nao na kupatikana kirahisi kwa gharama nafuu. 

“Benki zina mchango mkubwa kwenye ujenzi wa uchumi imara na zinaweza kuchangia sana kuleta maendeleo binafsi kwa kusaidia kutengeneza ajira  kwa kutoa mikopo kwa wananchi na kupitia fursa mbalimbali katika kusambaza huduma za taasisi hizo,” Makori alifafanua.

Aliongeza kusema kwamba ufunguzi wa Tawi la NMB Mbezi Louis ambalo ni la tano wilayani Ubungo na la 28 mkoani Dar es Salaam utasaidia kukuza idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki ambao kwa hivi sasa wapo chini ya asilimia 20.

Mkazi wa Kibamba aliyehudhuria hafla ya uzinduzi wa tawi hilo la NMB, Mugisha Godwin, aliliambia JAMHURI kuwa baadhi ya benki zipo zaidi kimasilahi binafsi kuliko kulihudumia taifa na kuwasaidia Watanzania wengi.

“Haiingii akilini benki inafanya biashara nchini zaidi ya miaka mitano hadi kumi ikiwa na tawi moja tu, tena katikati ya jiji (Dar es Salaam),” alisema na kuongeza: “Pia tulitegemea wingi wa benki ungesaidia kushusha gharama za huduma muhimu kama vile mikopo lakini hii imekuwa tofauti. Riba bado ni kubwa na baadhi ya masharti ni magumu sana.”

Mjasiriamali kwenye kituo cha mabasi cha Mbezi Louis, Jovina Jovis, alisema pamoja na yeye kupata mahitaji yake mengi ya kifedha kupitia simu ya kiganjani, bado umuhimu wa kuwepo matawi zaidi ya benki upo. Alizitaka benki ambazo hazina matawi katika maeneo ya pembezoni kuiga mfano wa NMB kufungua matawi katika maeneo hayo ili kuwafikia wananchi wa kawaida.

NMB tayari imefikisha matawi zaidi ya 220 nchi nzima, idadi ambayo ni kubwa kuliko idadi ya wilaya zote nchini na zaidi ya robo ya matawi ya benki zote.

Kwa sasa kuna benki 52 zilizosajiliwa kufanya kzi nchini ukilinganisha na benki 58 mwaka 2017. Kati ya hizo, 39 ni benki za biashara, tano ni zile zinazotoa huduma ndogo za fedha (microfinance banks), sita ni benki za kijamii (community banks) na mbili ni taasisi za fedha za maendeleo.

Ni benki chache tu kati ya hizi ambazo zina matawi kila mkoa au wilaya huku nyingi zikipatikana Dar es Salaam tu, hali ambayo wachumi wanadai ni kasoro kubwa kimaendeleo. Nyingi ya benki hizi pia zimeshindwa kujiongeza na kuwahudumia Watanzania kupitia vyanzo vya kibunifu kama mawakala ambao idadi yao nchi nzima sasa hivi ni 22,481.

“NMB imekuwa mstari wa mbele kuwa na bidhaa bora za kufikisha huduma zake kwa Watanzania kidijitali kama vile NMB Mkononi inayowezesha watu kufungua akaunti ya benki hii moja kwa moja kwa kutumia simu za mikononi bila kulazimika kwenda katika tawi lolote la benki,” Mkuu wa Wilaya Makori alisisitiza katika hotuba yake.

Maofisa wa benki hiyo walisema kufunguliwa kwa Tawi la Mbezi Louis ni  utekelezaji wa mpango wa NMB wa kufikisha huduma za kibenki kwa Watanzania wengi ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa NMB, Omari Mtiga, alisema kufunguliwa kwa tawi hilo la 224 ni mwendelezo wa mafanikio mengi ya benki hiyo tangu ibinafsishwe miaka 15 iliyopita. Kwa mujibu wake, NMB tayari inazo ATM 800 na ushei zilizosambaa kila kona ya nchi na mawakala zaidi ya elfu sita.

Mtiga alisema uamuzi wa kufungua Tawi la Mbezi Louis umetokana na tafiti mbalimbali zilizoonyesha kuwa eneo hilo linakua kwa kasi kiuchumi.

“Tumeona eneo hili linakua kwa kasi sana kibiashara lakini wateja wetu bado wamekuwa wakilazimika kusafiri kilometa 15 wakifuata huduma zetu katika matawi ya Ubungo, Sinza, Mlimani City na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,” alifafanua.

Pia Mtiga alisema benki yao mwaka huu imejipanga kuwekeza asilimia moja ya faida itakayopatikana kwenye shughuli za kijamii (CSR) kiasi ambacho ni kama Sh bilioni moja. 

Mpaka sasa tayari Sh milioni 850 zimetumika kuwahudumia wananchi kwenye masuala ya elimu, afya na majanga huku zaidi ya Sh milioni 200 ya fedha hizo zikiwekezwa mkoani Dar es Salaam peke yake.