Nina shauku kubwa ya kusoma kitabu cha Rais mstaafu Benjamin William Mkapa kuhusu maisha yake kinachoitwa ‘My Life, My Purpose’ (Maisha Yangu, Kusudio Langu).
Nina shauku kufahamu mtazamo wake juu ya masuala mbalimbali ya uongozi lakini nikiwa na hofu kuwa yapo mengi hayatasemwa.
Kila rais amekalia nafasi inayompa taarifa na uzoefu ambao raia wengine hatupati. Anayoyaandika yana uzito mkubwa ilimradi yapangiliwe vema. Yakiandikwa vizuri tunajifunza na kuishiwa maswali, yakiandikwa vibaya yanatujaza maswali.
Ni Rais Jakaya Kikwete, kama sikosei, aliyesema kuwa hatuna shule ya urais. Shule ya rais mteule inaanza anapoapishwa. Ushindi wake unampa uhakika wa kuandikishwa tu. Suala ambalo hana uhakika nalo ni kufaulu mitihani yote atakayopambana nayo.
Wapiga kura, tofauti na wazazi ambao watahangaika kugharamia elimu ya watoto wao, hawana subira isiyo na kikomo kusikiliza matatizo ya kiongozi. Kiongozi anayeshinda mitihani yake ni wetu sote, anaposhindwa anabaki peke yake.
Kitabu kinapaswa kuelimisha viongozi waliopo na wale watarajiwa, na si kwa wale wanaowania urais tu; masuala mengi ya uongozi ni masuala ya msingi ambayo yanaweza kutumika katika ngazi zote.
Lakini uzoefu wa kiongozi unaweza kuwa na manufaa hata kwa wale ambao si viongozi. Fursa (wengine wanaita balaa) ya kukalia moja ya viti vyenye moto kuliko vyote kwenye taifa inatoa somo muhimu kwa wote.
Tunatarajia kitabu kifafanue sababu za baadhi ya maamuzi ambayo Rais Mkapa aliyofanya. Nyakati zote hujitokeza tafsiri mbalimbali juu ya maamuzi ya viongozi, na tafsiri hizo huwa hazifanani na zile ambazo kiongozi mwenyewe anakusudia zieleweke. Kitabu kinamsaidia kuweka taarifa sawa kwa maelezo yake mwenyewe.
Si ajabu kwamba uamuzi mmoja unaweza kubeba tafsiri nyingi na zilizo tofauti na zile ambazo mhusika mwenyewe ataelezea. Nikiwa mdogo, wakati Rais Nyerere akiwa madarakani, nilihudhuria moja ya magwaride ya vikosi vya majeshi kwenye uliokuwa Uwanja wa Taifa. Baada ya kufanya mzunguko wa ukaguzi alielekeza aitwe mmoja wa askari aliyekuwa kwenye gwaride na tulishuhudia akiongea naye huku akiwa amemgusa begani.
Nilimsikia aliyekaa karibu yangu akitafsiri kuguswa begani kama ishara ya yule askari kupandishwa cheo. Tuliporudi nyumbani na kutaka kufahamu sababu za Mwalimu kumpandisha cheo yule askari alisema hakumpandisha cheo ila alibaini kasoro katika unadhifu wake na alimuita kumueleza hivyo.
Hili la askari kusahau kuchana nywele ni suala dogo kwenye historia ya kiongozi lakini yapo masuala ambayo, hata akijaribu kuyafafanua kwa kiasi gani yeye mwenyewe, bado hayatamaliza ubishi juu ya masuala yenyewe au sababu za yeye kufanya maamuzi aliyoyapitisha.
La muhimu zaidi ni yeye kuweka bayana suala lenyewe na kulisimulia kwa jinsi ambayo analiona. Hukumu juu yake na uongozi wake, kama nilivyosikia mzee Mkapa mwenyewe akiashiria, anamwachia Mwenyezi Mungu na Watanzania.
Pamoja na kuwa sijasoma kitabu chake, nina hakika kuwa hakitabadilisha hulka moja ya Watanzania: uwezo mdogo wa kusema ukweli.
Tatizo la kupata ukweli lina sura nyingi. Unaweza kufahamu ukweli na ukausema wote bila kusita. Hapo hakuna tatizo. Unaweza kufahamu ukweli lakini ukaamua kutousema, au ukausema kidogo na kuacha kiporo ambacho asubuhi kitatupwa. Hii ndiyo hulka ya Watanzania, na ninaamini itaibuka kwenye kitabu cha mzee Mkapa.
Kusema ukweli si jambo rahisi lakini tukubaliane kuwa kama uzoefu wa rais mstaafu unaweza kupimwa kuwa na manufaa yoyote, basi ni muhimu, kwa kadiri inavyowezekana, kuwa mkweli na muwazi wa kiwango kinacholingana na kaulimbiu ya utawala wake.
Lakini itakuwa muujiza kusoma rais mstaafu akiandika kujuta kumteua kiongozi aliyemuamini lakini baadaye kugundua kuwa ameteua mtu ambaye amekosa sifa hata ya kujiongoza mwenyewe, acha umati wa Watanzania.
Si mara chache nimesikia wagombea wa nafasi za uongozi wakisemwa chini chini kuwa ni wala rushwa wakubwa ambao wakishika uongozi wataifilisi nchi lakini hujitokeza kugombea uongozi na tutasikia wakirushiwa vijembe ambavyo mpiga kura wa kawaida hudhani ni porojo tu za kisiasa. Hatari iliyopo ni kuwa kwa kutosema ukweli, na ukweli wote, basi wale wenye taarifa za uhakika wanatoa mwanya kwa kiongozi mbovu kuhamia Ikulu wakati anapaswa kupelekwa Segerea.
Unaweza kuisema Marekani kwa mengi lakini Wamarekani wanastahili sifa ya umahiri wao wa kuchambua raia wenzao wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi, na kuhakikisha kuwa wanaochaguliwa wanalinda hadhi ya vyeo vyao.
Tofauti ya Marekani na nchi kama Tanzania ni kuwa ukweli, kwa raia wa kawaida na taasisi zisizo za kiserikali, unapatikana kwa urahisi zaidi Marekani kuliko kwetu. Raia wa kawaida Mtanzania hana uwezo wa kupata taarifa anazopata rais wake. Nadhani, bila kuhatarisha taarifa nyeti, rais mstaafu ana wajibu kutoa simulizi ambazo zinaelimisha, lakini pia zinalinda masilahi ya umma.
Pamoja na wasiwasi wangu kuwa sitasoma ukweli wote, bado ninayo shauku ya kusoma kitabu cha Rais mstaafu Mkapa. Nadhani ni Rais Ali Hassan Mwinyi aliyesema: Kila zama na kitabu chake. Kila jambo litajitokeza ukiwadia wakati wake.
Barua pepe: [email protected]