Kuna kitu kimenisukuma kuwaza hili hasa baada ya kuona kuna ombwe kubwa sana kati yangu na maisha mapya yaliyopo.
Nitaandika kwa sababu pia nimeona kuna umuhimu wa kukumbuka yote niliyoyaishi katika nyakati tofauti za utoto, ujana, makamo na sasa uzee huu.
Nimewaza kuandika kwa sababu nadhani ninaweza nikaacha historia fupi sana lakini ya muhimu kwa faida ya kizazi changu na si kizazi kingine.
Wapo watakaojifunza kwa maana ya wanangu, wajukuu, vitukuu, vilembwe na vilembwekeza vyangu. Naona taabu kuacha historia katika waraka wangu kwa kuwa nitakuwa nimeweka siri zangu nje ya familia.
Kwanza, nilizaliwa kijijini sana ambako kulikuwa na wakunga wa jadi. Mbali na kumsaidia mzazi, lakini wakunga wale walikuwa na kazi moja kubwa ya kuogofya, hasa mzazi anapojifungua mtoto mlemavu wa aina yoyote. Walikuwa kama mahakimu wa kuhukumu pasi na makubaliano ya mzazi au kusikiliza upande wowote. Mimi ni miongoni mwa watu wachache niliyekoswa na hiyo hukumu.
Sikuwahi kufikiria kukoswa huko mpaka pale nilipokuwa mkubwa na kusikia kutoka kwa watu wengine juu ya ubaya huu wa wakunga wetu pale kijijini. Haya ndiyo maisha kwa yeyote aliyezaliwa wakati huo na akabahatika kukatwa kitovu kule kijijini na ukiona bado anaishi ujue kuwa amekwepa mikuki mingi. Mimi ni miongoni mwa hao wachache ambao tulichaguliwa kuendelea kuishi kwa sababu ya karma tu.
Sikumbuki vizuri ni baada ya miaka mingapi nilipoanza kuchunga mbuzi, lakini akili zangu nyingi sana nimezipata machungani. Nilijua kula chakula cha mchana kwa juhudi zangu, nilijua kuwinda ndege na kumla mbuzi lakini akabaki kuwa hai. Haya yalitokana na njaa kali iliyonikabili nikiwa machungani.
Nakumbuka nilijifunza kusimama kizimbani na kujitetea mara kadhaa kutokana na kesi nyingi za kulisha mbuzi kwenye mashamba ya watu. Nilipitia hukumu nyingi za haki na uonevu, nikajenga sugu ya hukumu za haki na uonevu nikiwa bado kinda. Kutokana na hali hiyo niliaapa kutofuga mbuzi katika maisha yangu na kwamba wanangu hawatachunga mbuzi asilani.
Nilipata bahati ya kuandikishwa shule ya misheni, wakati huo walimu walikuwa masista wa Kikatoliki. Walikuwa walimu wenye upendo uliotukuka sana, walinivumilia sana kutokana na tabia zangu ambazo kimsingi zilijengwa na makuzi ya kukimbizana na mbuzi.
Walinifundisha kuandika kwa kushika vidole vyangu na kalamu kubwa kama chaki wakati huo katika kibao maalumu ambacho tulikuwa tukivaa shingoni kama daftari. Ni zamani na sipendi kukumbuka ili wanangu waishi maisha ya amani lakini leo ninatoa siri.
Kama ilivyo kwa maisha ya kuchunga na kesi zake, halikadhalika hata shuleni nako nilikumbana na changamoto zake, ikiwemo utoro na wizi wa vitu vidogo vidogo. Masista waliniombea na kunipa zawadi kila wakati ili niachane na tabia hizo.
Kwa kiasi kikubwa sana walifanikiwa na taratibu tabia za kuiba na kuwa mtukutu zilianza kuniacha na kuanza kumcha Mola. Hili sitalisahau kamwe katika maisha yangu. Adhabu ya kuombewa na kupewa zawadi badala ya kupigwa viboko visivyo na idadi au kulazwa njaa.
Nakumbuka ilifika wakati katika kipindi cha elimu ya kujitegemea tulikuwa tukivuna karanga na machenza lakini bila kushurutishwa au kutishwa; na bila ulinzi wowote, sikuweza kuthubutu kula hata kipande kimoja. Kilikuwa kipindi kizuri sana cha mpito wa tabia zangu, kutoka tabia za ovyo na kuja katika tabia za ubinadamu.
Historia yangu inakwenda mpaka nilipoanza kuaminiwa kusoma na kuandika katika madaftari na vitabu vikubwa kama mkeka. Nilivipenda vitabu kwa hadithi zake na kuandika kwa kuchora vizuri na kusifiwa na masista ambao walikuwa walimu wangu. Ni katika kipindi hiki ndipo nilipogundua wengi wetu tabia zilikuwa zinalingana isipokuwa tofauti ilikuwa katika kubadilika.
Nikahitimu darasa la nne na tukawa wahitimu muhimu kwa maendeleo ya vijiji vyetu na kuwafundisha wengine. Vuguvugu la uhuru likaja baada ya miaka michache na tukajiunga kupambana na mkoloni. Jitihada zetu kubwa ilikuwa kuwaelewesha wazazi wetu ambao waliamini katika utumwa na uchifu. Tulifungua madarasa ya ngumbaru na tukageuka masista wa kufundisha wazazi wetu.
Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.