Msifikiri Watanzania ni wajinga au hawana akili. Mpango wa kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani haukuwa utashi wa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019. 

Wenye akili wanajua kwamba ulikuwa mpango mahususi ulioandaliwa wa kuigeuza ‘Tanzania kuwa ya kijani.’

Mpango huu ulitanguliwa na ule wa ‘kuunga mkono juhudi’ – kuwarubuni madiwani, wenyeviti wa vitongoji, mitaa, wabunge na viongozi wa ngazi mbalimbali za chama kikuu cha upinzani – Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Lakini kwa waelewa wanajua kuwa ile hatua ya Rais John Magufuli ya kupiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa vya upinzani, ililenga kuudhoofisha upinzani kiasi kwamba wateule wake katika wilaya na mikoa walipiga marufuku vyama ambavyo vipo kikatiba na kisheria kufanya kazi za kisiasa. Mfano ni tamko la aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Steven Kebwe, aliyenukuliwa akisema:

“Marufuku mikutano ya siasa katika mkoa wangu, wasubiri hadi 2020 kama watakuwa hai. Kama wanataka kujifunza siasa watafute pahali pengine. Nitawafuata hata wakiwa watatu ndani.”

Hata baada ya Rais Magufuli kulegeza kamba na kuelekeza kwamba madiwani na wabunge wa kuchaguliwa wanaruhusiwa kufanya mikutano ya wazi katika maeneo na majimbo yao, marufuku ya awali ilikwisha kuharibu mwelekeo wa vyama hivyo.

Vyombo vya dola – hususan Jeshi la Polisi, ambalo linatafsiri kwamba hiyo ilikuwa amri, limeendelea kuwanyanyasa wapinzani kiasi kwamba askari wa upelelezi hutumwa kunusanusa hata kwenye mikutano ya ndani ya wapinzani, kama ilivyotokea hivi karibuni kule wilayani Hai ambako mkuu wa upelelezi wa wilaya hiyo alilazimisha kuhudhuria mkutano wa ndani wa Chadema.

Siyo siri tena kwamba polisi walihusika katika mvutano wa ndani wa Chama cha Wananchi (CUF), ambao uliratibiwa na vyombo vya dola kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Pamoja na viongozi wa CUF upande wa Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad, almaarufu Maalim, kukimbilia mahakamani (baada ya msajili kuonekana anaegemea upande mmoja), ili kukinusuru chama, bado CUF ilisambaratishwa.

Viongozi waliushitukia mwenendo wa Mahakama pia, wakabuni mpango mbadala wa kuhamia chama kingine cha upinzani endapo Mahakama itaamua kinyume cha matarajio yao. CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ilishinda.

Wenye akili waliliona sakata lile lilikuwa la kupikwa, na lengo lake lilikuwa ni kuivuruga CUF ili kukipa nguvu Chama Cha Mapinduzi (CCM) upande wa Zanzibar. 

Baadhi wachambuzi wa masuala ya siasa za Zanzibar wanasema CCM haijawahi kupata ushindi Zanzibar tangu mfumo wa vyama vingi urejeshwe mwaka 1993. Mara zote chama hicho kimevuruga uchaguzi na kuiba ushindi.

Januari 2001, zilitokea vurugu na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 22 na wengine zaidi ya 2,000 kukimbia nchi. Kitendo hicho kiliitia doa Tanzania – nchi ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo tangu ipate uhuru mwaka 1961 imekuwa yenye amani na utulivu na kuwa kimbilio la Waafrika waliokuwa wanakandamizwa na watawala wao.

Wanamkakati wa mpango wa kuivuruga CUF waliamini kuwa ushindi wa Lipumba na kundi lake ungesababisha Maalim Seif na wenzake kuanzisha chama kipya cha siasa. Wangefanya hivyo huenda wangekwamishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.  CCM waliamini kwamba wangeweza kuibuka na ushindi mnono upande wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Mkakati huo umeshindwa vibaya. CUF upande wa Maalim Seif  walihama si tu na viongozi na wanachama wengi, Pemba na Unguja, bali pia na mali zote za chama na kujiunga na ACT-Wazalendo. Uamuzi huo umekipa nguvu kubwa chama hicho na huenda kikashinda upande wa Zanzibar kama uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.

Sambamba na hilo, ulisukwa mpango mahususi pia wa ‘kuwabughudhi’ viongozi wa juu wa vyama vya upinzani ili wasipate nafasi ya kuvijenga vyama vyao. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alitupwa gerezani kwa miezi mitatu kwa madai ya kutofuata masharti ya dhamana.

Wenye akili wanaona kuwa kulikuwa na mkono nyuma ya uamuzi huo. Miezi michache baadaye hakimu aliyemfunga Mbowe aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.

Viongozi wakuu wa Chadema na ACT-Wazalendo, wakiwamo wabunge, wanashinda mahakamani ambako wamefunguliwa mashitaka ya kihalifu. Haitashangaza kama kesi hizo huenda hazitaamuliwa hadi baada ya Uchaguzi Mkuu ujao, hivyo kuwanyima washitakiwa nafasi ya kusimama katika uchaguzi huo.

Mkakati uliokuwa umepangwa wa kuufuta upinzani na kuifanya Tanzania ya kijani, ulilenga kuwanyima wapinzani nafasi zote za uongozi katika ngazi zote, hasa katika maeneo ambayo ni ngome zao.

CCM wanajinadi kwamba ni chama pendwa, hivyo kuwaaminisha wananchi kwamba upinzani umekwisha kufa na kuzikwa, kama igizo lililofanywa na Naibu Spika, Tulia Ackson, kule Mbeya Mjini hivi karibuni. Tukio lile halikuwa la bahati mbaya.

CCM wanasahau kwamba utamu wa mchezo wa mpira ni pale timu unayoipenda inapata ushindi uwanjani dhidi ya mahasimu wake. Lakini katika sarakasi ya uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, hakuna msisimko. Uwanja hauko sawa, serikali ni ya CCM, sheria na kanuni zimetungwa na serikali hiyo hiyo. Wasimamizi na wasaidizi wao ni wateule wa serikali. Kuna kitu hapo?

Haijawahi kutokea tangu Tanzania ipate uhuru, watendaji wote – kata, halmashauri zote na wakuu wa wilaya na mikoa kukutana Ikulu na rais huku kukiwa na uchaguzi mbele. 

Lakini ukiangalia haya yanayotokea sasa kuhusiana na uchaguzi huo, wenye akili wanajua kwamba watendaji na wasimamizi waliitwa Ikulu na rais ambaye ndiye Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kupata maelekezo maalumu.

Kwa hiyo sarakasi zinazoendelea kwenye mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni matokeo ya mkakati uliobuniwa na CCM na kutekelezwa na serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Pombe Magufuli. Katika mazingira hayo, utakuwa ni muujiza kwa vyama vya upinzani kushinda.

Dawa kubwa ya songombingo hizi zote ni Katiba Mpya ili kuweka uwanja wa kisiasa sawa.

Wanaofikiri vizuri walianza kuona dalili za mkakati huo kushindwa kabla ya kutekelezwa. Serikali ilitunga sheria na kanuni za uendeshaji wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Wapinzani walipendekeza marekebisho ya baadhi ya vipengele vya sheria na kanuni hizo. Hawakusikilizwa.

Serikali ilishituka baada ya kuona mwitikio hafifu wa uandikishaji wa wapiga kura, matokeo ya kuviminya vyama vya upinzani kufanya siasa. Hapakuwa na uhamasishaji wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha na kupiga kura. 

Katika baadhi ya maeneo baadhi ya viongozi wa serikali wakatoa matamko kuwalazimisha watumishi wa umma wakiwamo walimu na wanafunzi kujiandikisha, huku wakionya kwamba kama hawatajiandikisha watachukuliwa hatua.

Serikali ikaongeza muda wa kujiandikisha kwa siku saba. Baada ya hapo, Waziri Jafo akatangaza kwamba uandikishaji ulikuwa umevuka lengo na kufikia asilimia 80 badala ya asilimia kati ya 60 na 64.

Baada ya hapo likaja zoezi la watia nia kwenda kuchukua fomu za kuomba nafasi za uongozi.  Wanachama wa CCM wakawahi kuchukua fomu katika baadhi ya maeneo na ofisi za wasimamizi wa uchaguzi wasaidizi zikafungwa. Katika baadhi ya wilaya, watia nia wa upinzani wakawa wanashinda kwenye ofisi hizo bila mafanikio mpaka muda wa kuchukua fomu ukaisha. Hawakupata fomu.

Imeripotiwa kwamba sehemu ambazo watia nia wa upinzani walichukua fomu, walishindwa kuzirejesha kwa sababu wahusika walikuwa hawakai ofisini na watia nia wa CCM walirudisha kwa wakati! 

Wagombea wa upinzani waliofanikiwa kurudisha fomu hawakuteuliwa kutokana na sababu mbali mbali, ikiwemo kukosea kujaza au kutojua kusoma na kuandika na wengine kuwekewa pingamizi kwamba si raia wa Tanzania.

Kwa maelezo ya Mbowe, zaidi ya asilimia 90 ya watia nia wa Chadema nchi nzima walienguliwa kwa hila. Chama hicho kilikuwa cha kwanza kutangaza kwamba hakitashiriki uchaguzi huo, kikifuatiwa na vyama vingine sita; ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, CUF, NLD, CHAUMA na UPDP.  

Serikali imefuta uamuzi wa wasimamizi wa kuwaengua wagombea wa vyama vya upinzani. Waziri Jafo amesema ‘hakuna kujitoa.’ Lakini sheria inasema mtu hawezi kugombea nafasi yoyote ya uongozi wa kisiasa bila kupitia chama cha siasa. Itakuwaje! CCM wamekwisha kutangaza ushindi. Wamepita bila kupingwa, uchaguzi ni wa nini?

Balinagwe Mwambungu ni mwandishi/mhariri mwandamizi wa kujitegemea.