Matumizi ya simu, hasa za mikononi kwa ajili ya mawasiliano yamezidi kuimarika huku kampuni zinazotoa huduma hiyo nchini zikitengeneza fedha nyingi na kuifanya biashara hiyo kuwa miongoni mwa zile zenye faida kubwa nchini.

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miezi sita ya kwanza mwaka 2019 mauzo ya huduma za simu yalikuwa zaidi ya Sh trilioni 2.5 ambazo Watanzania walizitumia kufanya mawasiliano mbalimbali.

Kiasi hicho ni sawa na matumizi ya Sh bilioni 416.6 kwa mwezi au Sh milioni 13.8 kila siku. Kwa idadi ya laini za simu milioni 43 zilizokuwa mikononi mwa Watanzania hadi kufikia katikati ya mwaka huu, matumizi ya kila siku ilikuwa ni wastani wa Sh 320.9 kwa gharama ya kila mtu na laini zake kwa mwezi ilikuwa Sh 9,678.3.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), kiasi cha Sh trilioni 1.27 kilitumika kati ya Januari na Machi huku gharama za kuwasiliana kwa simu kati ya Aprili na Juni zikiwa Sh trilioni 1.24.

Hizo si fedha chache, hasa upande huu wa dunia ambako ni kazi kubwa kwa kaya nyingi kumudu milo miwili kamili kwa siku huku watu wengi wakitumia chini ya Sh elfu tano kwa siku kwa ajili ya chakula.

Umoja wa Makampuni ya Simu za Mikononi Duniani (GSMA) unasema Tanzania ni miongoni mwa masoko mabubwa ya biashara zinazohusiana na simu za mikononi barani Afrika. Pia ni kati ya masoko yenye ushindani mkubwa kutokana na wingi wa kampuni zinazofanya biashara hizo ambazo kwa sasa ni saba.

GSMA inasema watu wenye simu za mikononi nchini wameongezeka kutoka milioni tano mwaka 2007 hadi milioni 25.2 sasa hivi, huku wengi wakimiliki zaidi ya laini moja ya simu. Umoja huo unaongeza kwamba wastani wa pato kutoka kila mtumiaji wa simu za mkononi (average revenue per user – ARPU) wa dola 2.5 (takriban Sh 5,750) kwa mwezi ni miongoni mwa viwango vya chini kwenye ukanda huu.

Mbali na huduma za maongezi na ujumbe mfupi (SMS), kampuni za simu pia zinapata faida kubwa kwenye biashara ya pesa mtandaoni na matumizi ya data, ambavyo sasa hivi ni vitengo vikubwa kwenye sekta hii.

Biashara na huduma hizi imekuwa na mchango mkubwa katika kuifanya sekta ya habari na mawasiliano kuwa miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi sana kwenye uchumi wa taifa na uchangiaji mkubwa wa ukuaji wa pato la taifa. Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2019, sekta hii ilikuwa ya tatu bora baada ya kukua kwa asilimia 10.7 nyuma ya uchimbaji madini na mawe (asilimia 13.7) na ujenzi (asilimia 16.5).

“Shughuli za habari na mawasiliano zilikua kwa kiwango cha asilimia 10.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2019 ukilinganisha na asilimia 12.4 kipindi kama hicho mwaka 2018. Ukuaji huu ulitokana na kuongezeka kwa matumizi ya muda wa maongezi ya wateja wa simu za mikononi na kupanuka kwa shughuli za utangazaji na huduma za intaneti,” NBS ilisema hivi karibuni.

Takwimu zake zinaonyesha kuwa mauzo ya huduma za simu yalikuwa Sh bilioni 542 kwenye robo ya kwanza mwaka 2014 kabla ya kuongezeka hadi Sh bilioni 667 kipindi kama hicho mwaka uliofuata. Gharama za mawasiliano ya simu kati ya Januari na Machi mwaka 2016, 2017 na 2018 zilikuwa Sh bilioni 807,997 na 1,154 mtawalia.

Matumizi ya kuwasiliana kwa simu kwenye robo ya pili mwaka 2015 yalipanda hadi Sh bilioni 736 mwaka 2015 na Sh bilioni 854 mwaka 2016. Kwa mwaka 2017 na 2018, gharama za mawasiliano kati ya Aprili na Juni zilikuwa Sh bilioni 989 na 1,123 mtawalia.