Rais mstaafu Benjamin William Mkapa (81), ameandika kitabu kinachoelezea maisha yake ya utotoni hadi urais.
Uzinduzi wa kitabu hicho chenye kurasa zaidi ya 300 umefanywa na Rais John Magufuli na kuhudhuriwa na viongozi, viongozi wastaafu na watu mashuhuri.
Kitabu hicho kimesheheni historia na mambo mengi ya kuvutia. Kina maelezo mengi ya kutubu kutokana na yale ambayo mzee Mkapa anaamini, ama alikengeuka au alipotoshwa wakati wa uongozi wake.
Ameeleza kwa kina ushiriki wake katika siasa za ukombozi wa taifa letu, Bara la Afrika na ulimwengu kwa jumla.
Bila kumng’unya maneno, ameeleza hisia zake kwa mambo makubwa ya haki, uongozi bora na ukuzaji wa demokrasia nchini mwetu. Kwa ufupi ni kwamba mzee Mkapa ameeleza mambo mengi mno kwenye kitabu hicho.
Watanzania wa kada zote watakuwa hawamtendei haki mzee Mkapa endapo watapuuza au kuzembea kusoma yaliyomo kwenye kitabu hicho. Lakini ili hilo liweze kufanyika, mtunzi wa kitabu hana budi kuhakikisha kitabu hicho kinafasiriwa kwa lugha ya Kiswahili inayozungumzwa na kuandikwa na Watanzania wengi. Kwa kufanya hivyo ujumbe uliomo humo utawafikia wengi.
Ni wajibu wa viongozi wa sasa na wajao kuyazingatia yale yaliyoandikwa katika kitabu hicho. Mzee Mkapa amemaliza wajibu wake kwa kutunga kitabu, sasa ni wajibu wetu sote kusoma, kuchambua na kuchukua mengi mazuri kwa manufaa ya taifa letu kwa sasa na kwa miaka mingi ijayo.
Tunaamini mambo kama ya haki kwenye uchaguzi unaoshirikisha vyama vingi vya siasa ni ya msingi kabisa. Tumeona aibu na fedheha kubwa ya kuvurugwa kwa hatua za awali za uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini kote. Mkanganyiko uliotokea ni aibu na doa katika safari yetu ya kuelekea kwenye demokrasia ya kweli.
Matumizi ya madaraka, matumizi ya rasilimali za nchi, usikivu na utendaji haki ni miongoni mwa mambo yaliyosisitizwa na mzee Mkapa. Tumsome mstari kwa mstari, tumwelewe na tutekeleze yale tunayoamini kuwa yana manufaa kwa jamii nzima.
Mzee Mkapa ametoa mwongozo. Amefungua njia. Sasa ni wakati mzuri kwa wastaafu na hata kwa walio madarakani kuandika vitabu wakingali hai. Watu wengi mashuhuri wameaga dunia bila kuacha hazina ya maandishi. Hiyo ni dosari kubwa. Hongera mzee Mkapa. Umefanya jambo jema kwa nafsi yako na kwa walimwengu.