Leo naandika juu ya uanaharakati kama nyenzo inayotumika na watu au makundi ya watu kuendesha kampeni za kuleta mabadiliko ndani yajamii.

Tumezoea kuhusisha uanaharakati na siasa pekee, lakini ni mada pana inayovuka uwanda wa siasa. Najikita juu ya jinsi gani uongozi unavyoweza kuwa chachu ya mafanikio lakini, wakati huo huo, kuwa kikwazo cha kufanikisha malengo ya harakati.

Raia wa India, Vandana Shiva, ni mwanaharakati anayejulikana kwa mengi. Ni msomi, mwandishi wa vitabu, na mtetezi mkubwa wa wakulima wadogo. Anapinga matumizi makubwa ya pembejeo za viwandani yanayoathiri usalama wa ardhi katika kuzalisha mazao ya kilimo. Ni mtetezi wa ulinzi wa urithi wa dunia wa mimea na wanyama; suala ambalo huaminika kuwa muhimu kwa viumbe vyote.

Lakini anajulikana zaidi kwenye makundi yanayopinga matumizi ya bidhaa na mbegu za GMO, mbegu ambazo makundi hayo yanasema zina athari kubwa za kiafya kwa matumizi ya binadamu.

Natumia neno “yanasema” kuepuka mashambulizi ya kisheria yanayoweza kuanzishwa na vinara wa kutengeneza mbegu hizo ambao wanasema kuwa tafiti hazithibitishi kuwa mbegu hizo zina madhara yoyote.

Matokeo ya tafiti zinazolipiwa na kampuni zenye biashara ya GMO hayaonyeshi kuwapo madhara. Lakini tafiti nyingine huru zinaonyesha kuwa yapo madhara. Matokeo ya utafiti yaliyotolewa na serikali ya Austria yanaonyesha kuwa panya wa maabara waliolishwa mahindi yaliyozalishwa kutokana na mbegu za GMO walizaa panya wachache zaidi kuliko wale ambao walilishwa mahindi ambayo hayakutokana na mbegu hizo.

Utafiti mwingine uliyofanywa Ufaransa unaonyesha kuwa panya waliolishwa mahindi ya GMO kwa kipindi cha miaka miwili walipata saratani, na maradhi ya figo na maini na kufa mapema. Wanaoshabikia matumizi ya GMO wamekosoa utafiti huu kwa kuwa na hitilafu za kimchakato.

Kisichokuwa na ubishi ni kupanuka kwa matumizi ya mbegu hizi kwa kutumika nguvu kubwa ya kiuchumi ya kampuni zinazozalisha mbegu hizi; nguvu inayolenga kudhibiti desturi ya wakulima ya kuhifadhi mbegu asilia na kuzitumia kupanda kwa misimu inayofuata. Sifa moja ya mbegu za GMO ni kutumika mara moja tu na hivyo kumlazimisha mkulima kununua mbegu kila anapotaka kupanda upya.

Katika hili, Shiva amepaza sauti dhidi ya jitihada za kampuni kubwa zinazozalisha mbegu kusajili hatimiliki za mbegu, akipinga kwa nguvu mkataba wa mwaka 1994 wa Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) unaotoa tafsiri pana ya hatimiliki inayotoa kinga kisheria ya kusajili hatimiliki ya viumbe hai.

Ubishi wa kitafiti unahitaji wanaharakati wasomi wanaoweza kujibu hoja kinzani zinazoibuliwa na wanufaika wakuu wa biashara ya GMO. Lakini inafahamika kuwa usomi pekee hautoshi kupambana na uwezo mkubwa wa baadhi ya kampuni hzi ambazo zimekuwa na uwezo hata wa kushawishi serikali mbalimbali kutunga sheria zinazolinda maslahi yao na wakati mwingine kupuuza haki za wakulima wadogo.

Na ni hapa tunapoona ukomo wa ushawishi wa mwanaharakati mmoja au kundi dogo la wanaharakati kuweza kutetea na kulinda maslahi ya wengi.

Wanaharakati kama Shiva na wenzake ni kundi dogo la watu linalozungumzia athari zinazoweza kutishia afya ya mabilioni ya watu ulimwenguni. Lakini sehemu kubwa ya hao watu wanaendelea na maisha bila kufuatilia kwa karibu yanayosemwa kwa niaba yao.

Zipo sababu za kuwapo hali hii. Kwanza, ni uelewa mdogo wa wanaotetewa juu ya athari inayowakabili. Ni kosa lile lile la elimu kubaki vyuoni, ikijadiliwa na wasomi na wanaharakati, bila kuwapo mikakati ya kuishusha kwa wale ambao hawako vyuoni na ambao wanaathirika zaidi na suala linalojadiliwa.

Mkulima masikini ambaye kila msimu anakabiliwa na suala la kununua mbegu hahitaji kuelezwa athari za mbegu za GMO na mbegu zinazozalishwa viwandani. Anazifahamu kwa sababu anaathirika nazo kila msimu.

Nje ya harakati za masuala kama GMO, yapo masuala ambayo yanahitaji somo la muda mrefu kubainisha athari ambazo mlengwa anaweza kuzipata kutokana na uamuzi ambao hauwezi kuunganishwa moja kwa moja na athari zitakazojitokeza.

Hii inamaanisha kuwa elimu ni kipengele muhimu sana cha harakati yoyote; elimu juu ya jinsi gani lengo linalokusudiwa linaweza kumaliza tatizo ambalo linakabili walengwa.

Uhakika wa mafanikio unawalazimu waongoza harakati kuuona mchakato wote kama kazi ya wengi na siyo inayowategemea viongozi pekee. Ni tatizo kwa viongozi kuamini kuwa bila wao harakati hazitafanikiwa. Timu iliyopo uwanjani inahitaji kina Maradona, lakini Maradona peke yake bila msaada wa wengine hawezi kufanikisha ushindi.

Tatizo ni kubwa zaidi iwapo umma nao unaamini kuwa bila kiongozi, basi malengo hayafikiwi, badala ya kuamini kuwa hata kama kiongozi mmoja hayupo, basi kiongozi mwingine anaweza kuibuka miongoni mwao na kuendeleza kazi ambayo haijakamilika.

Kiongozi mzuri wa kusimamia harakati ni yule anayejiona kama kiungo kinachokoleza au kukamilisha chakula kinachopikwa.

Kina Vandana Shiva ni muhimu sana, lakini ufanisi wa kazi yao unahakikishiwa na umma unaopokea somo, kulielewa, na kuliona kuwa suluhisho la changamoto zilizopo. Umma unapoamua ushindi unanukia.

Barua pepe: [email protected]