Fursa hazipotezi muda zikikutana na wale ambao hawajajiandaa, zinapita. Fursa ikikutana na maandalizi kwa pamoja vinazaa bahati. “Nitajiandaa na siku moja fursa yangu itakuja,” alisema Abraham Lincoln. Kutojiandaa ni kuharibu furaha ya kesho, kutojiandaa ni kujiandaa kuyapa mgongo mafanikio.
“Kwa kushindwa kujiandaa, unajiandaa kushindwa,” alisema Benjamin Franklin. Kujiandaa kunatangulia mafanikio. Kuna mambo ambayo yanawafanya watu wasijiandae.
Kwanza ni kuwa katika eneo la faraja. Hili ni eneo ambapo watu wanajiona wako salama, wamefarijika. Hawataki kujisumbua. Kazi ya kweli ya kupigia debe maendeleo ni kuwasumbua waliofarijika na kuwafariji waliosumbuka. Lazima kutoka katika eneo la faraja ambalo linakufanya usifanye lolote la maana na kujiandaa.
Ili kuleta mabadiliko ni lazima kuvunja uzio na ukuta wa eneo la faraja inayokufanya kubweteka. Vuruga kiota cha faraja. Mwewe akiona makinda hawatoki kwenye kiota kujifunza kuruka, anavuruga kiota.
“Faraja ni mtego wako mkubwa na kutoka katika eneo la faraja ni changamoto yako kubwa,” alisema Manoj Arora.
Katika Biblia tuna watu waliovunja ukuta wa eneo la faraja, ni Musa: “Kwa nguvu ya imani, Musa alipofikia utu uzima, alikataa kuitwa mwana wa binti Farao.” (Waebrania 11: 24). Musa alikuwa kwenye eneo la faraja la kuitwa mwana wa binti Farao. Mambo mawili yalimfanya kuacha eneo la faraja: nayo ni nguvu ya imani na utu uzima.
Jambo la pili linalotufanya tusijiandae ni kusitasita. Ngoja ngoja huumiza tumbo. Asubuhi ni wakati wa kuweka kipimo cha kasi utakayotumia. Kuna nguvu ya kufanya mambo mapema.
Kuna mtu aliyeambiwa kuna ng’ombe dume watatu kwenye zizi, ukiweza kukamata mkia wa mmojawapo utapewa zawadi ya Sh milioni mbili. Ng’ombe wa kwanza kujitokeza alikuwa mkali, macho makali, mnene na wa kutisha. Mtu huyo akaogopa kushika mkia wake. Wa pili kujitokeza alikuwa mkali zaidi na wa kutisha zaidi. Mtu huyo akangoja wa tatu. Wa tatu alikuwa amekonda, hana nguvu. Mtu huyo akasema nitashika mkia wa huyo. Bahati mbaya hakuwa na mkia. Alishindwa kufanya mambo mapema. Adui ya nguvu ya mapema ni kusitasita.
Jambo la tatu ambalo linatufanya tusijiandae ni mazoea mabaya. Kuna methali ya Tanzania isemayo: “Huwa ninazaa watoto namna hii, aliuawa na mimba ya tisa.” Mazoea yanaweza kupofusha macho yetu, na kutufanya viziwi.
Ukimtia chura kwenye maji moto ataruka ili atoke. Lakini ukimtia kwenye maji baridi na kupasha joto pole pole chura hatajua ni lini maji yamekuwa ya moto. Mazoea yanamfanya mtu hasishtuke. Mazoe ya kutenda mema yatakusaidia.
Jambo la nne linalotufanya tusijiandae ni inesha au ubaridi au kigugumizi cha kuanza. “Watu wengi hushindwa kwa sababu hawaanzi. Hawaishindi inesha. Hawaanzi,” alisema Ben Stein.
Jiulize umefikaje ulipo: kwa kuelea au kwa kupiga makasia? Kama ni kwa kuelea utakuwa hauna mwelekeo na dira. Kama ni kwa kupiga makasia, ina maana unafanya kitu fulani. Palipo na inesha kuna kushindwa kuonyesha hisia kali au shauku. Hakuna bashasha. Inesha ni kutofanya lolote.
Kuna hadithi ya fisi aliyetoa kipande cha nyama kwenye sufuria. Kilikuwa ni cha moto. Kilimchoma midomo. Fisi wenzake wakamwambia: “Tema.” Akawajibu. “Niteme utamu.” Wakazidi kumshauri, “Meza.” Akawajibu: “Nimeze moto.” Huu ni ubaridi unaoletwa na kukosa uamuzi. Yote yakishasemwa, kupanga ni kufikiria. “Kila kitu kiko tayari, kama akili yetu iko tayari,” alisema William Shakespeare katika kitabu chake, Henry V.