Dunia inatawaliwa na wenye maarifa
Tupo katika kipindi ambacho kuwa na maarifa ni jambo la muhimu mno. Dunia ya sasa inatawaliwa na watu wenye maarifa. Bila kuwa na maarifa utajiweka katika wakati mgumu. \
Maarifa yatakufanya uongoze kila unapokwenda. Maarifa yatakufanya upendwe na watu. Watu watahitaji kuwa karibu nawe muda mrefu. Maarifa yatakufanya uwe kinara, maarifa yatakufanya uwe mbobezi. Maarifa yatakufanya uitwe gwiji.
Magwiji wote ambao dunia ya leo inafurahia kazi zao walikuwa na wengine ni watu wenye maarifa. Vijana ambao wanafanya vitu ambavyo magwiji wa dunia walifanya nawaita Vijana wa Maarifa.
Imesemwa mara nyingi kuwa maarifa ni nguvu, maarifa huwa nguvu hasa pale yanapotumika. Kuwa na maarifa na yasitumike haiwezi kuwa nguvu, bali ni hasara. Charles Darwin alikuwa sawa aliposema kitu kisipotumika kwa muda mrefu baadaye hupotea au huishiwa nguvu. Hivyo maarifa yasipotumika nayo pia hupotea.
Maarifa ndiyo yametatua matatizo mengi yanayotuzunguka. Maarifa ndiyo yametatua migogoro mingi katika jamii zetu. Maarifa ni hekima. Wanasema hekima ni matumizi ya maarifa kutatua changamoto zinazotuzunguka. Watu wenye maarifa katika jamii zetu ndiyo tunaowaona kama watu wenye hekima.
Watu wenye maarifa hutumia muda wao mrefu kufikiri namna ya kukumbana na changamoto mbalimbali na kuzitatua. Ni wazi kuwa kuna wakati unaweza kuona kitu kinafanyika mahali fulani na ukasema hata miminiliwahi kufikiria kufanya jambo hilo, lakini sikufikiria kama linaweza kuwa na matokeo makubwa kiasi hiki. Alichokuzidi huyu aliyeanzisha kitu hicho ni maarifa na taarifa. Wewe ulitaka kufanya kitu juu juu mwenzako alizama ndani na kuchimba zaidi.
Kama hauna maarifa, kama hutumii nguvu na hata kipato chako kuwekeza katika maarifa, jiandae kubaki nyuma siku zote. Wale unaowaona kila kukicha wanapiga hatua jua kwamba wamewekeza katika maarifa.
Tupo katika zama ambazo mashine zinakuja kwa kasi na kuondoa watu kazini. Kazi iliyoweza kufanywa na watu watatu ndani ya siku mbili inafanywa sasa na mashine moja, ndani ya saa kadhaa, kazi imekwisha.
Kadri teknolojia inavyokua mashine nyingi zinaanza kufanya kazi za watu, hivyo kutakuwa na watu wengi sana wanaokosa kazi kwa sababu kazi zao zitaanza kufanywa na mashine.
Hakuna asiyejua kwamba zamani ili ufanyiwe operesheni ulihitaji madaktari wasiopungua watatu. Leo operesheni kama hiyo inahitaji daktari mmoja anayetumia muda mfupi. Mambo yamebadilika!
Ukiwa na maarifa katika kipindi kama hiki si rahisi kutoka kazini. Unachotakiwa kufanya ni kujifunza kuendana na mifumo yake. Wale ambao hawako tayari kujifunza maisha kwao yatawabadilikia. Uzuri ni kwamba mashine haiwezi kufikiri kama anavyoweza kufikiri mwanadamu mwenye maarifa,. Yenyewe imetengenezwa kwa mfumo wa kufanya kazi kwa namna fulani. Mtu mwenye maarifa mahali popote atategemewa Kwa sababu uwezo wake wa kuzalisha utakuwa mkubwa.
Kusema kwamba mashine zinawatoa watu kazini simaanishi watu walioajiriwa tu, hata wewe uliyeajiajiri, ama huna maarifa jiandae kuona biashara yako au kazi yako inakufa na inatawaliwa na watu wenye maarifa. Inafanyaw na watu kwenye viwango na ubora wa hali ya juu. Siyasemi haya kumtisha mtu, bali ni kujiandaa na yale yanayokuja mbele yetu. Lisemwalo lipo, kama halipo, basi linakuja.
Kuna watu wanaofikiri kwamba wakihitimu shule mambo ya kujifunza yamekwisha wanasahau kwamba shule rasmi huanza pale wanapohitimu. Maisha ni shule ya kila siku. Hatupaswi kuacha kujifunza kwa sababu maisha yenyewe huwa hayaachi kutupa mambo ya kujifunza.
“Watu wengine wanakufa wakiwa na umri wa miaka 25 na hawazikwi hadi wanapofikisha miaka 75,” alisema Benjamin Franklin. Kuacha kujifunza ni sawa na kukaribisha kifo ukiwa bado hai. Unakuwa mfu anayetembea (walking dead). Kuna ambao ni vijana na wameamua kuwa wazee na kuna wazee ambao bado ni vijana.
Kutokuwa na maarifa ukiwa kijana ni kujizeesha mapema,. Unakuwa umepitwa na wakati. Si jambo jema kama kijana kuitwa mtu aliyepitwa na wakati. Mambo yanapobadilika ni lazima na wewe ubadilike.
Wahenga walisema, “Elimu ni bahari.” Elimu haina mwisho. Jambo jema kuhusu maarifa ni kwamba yanapatikana kila kona, hayajifichi. Maarifa yapovitabuni. Maarifa yapo kwenye intaneti, maarifa wanayo watu wanaotuzunguka.
Ishi katika kutafuta maarifa. Maarifa ni ufunguo wa mafanikio katika mlango unaoitwa maisha.