Ana kwa ana ni tafsiri ya mahojiano baina ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere, na mwandishi wa magazeti, David Martin. Mahojiano haya yalichapishwa katika Gazeti la Kiingereza, New Internationalist, toleo la Mei, 1973.
David Martin ni Mwingereza na ni mwandishi wa magazeti kwa muda mrefu. Aliwahi kufanya kazi Tanzania kama msaidizi wa mhariri wa magazeti ya Serikali – The Standard (Daily News hivi sasa) na Sunday News. Alishika madaraka hayo baina ya mwaka 1970 na 1971.
New Internationalist ni gazeti linalochapishwa Uingereza katika lugha ya Kiingereza, nalo hujishughulisha zaidi na masuala ya nchi zinazoendelea. Endelea na sehemu ya tano ya mahojiano hayo…
Swali: Je, kwa kufuata funzo la Tanzania, viongozi kwa ujumla wameweza vya kutosha kuacha tamaa zao za kutaka kuwa viongozi kwa sababu ya utajiri wao wa kibinafsi au kama njia ya kupatia utajiri?
Jibu: Hapana, siyo kabisa. Nafikiri itakuwa kichekesho kufikiria hakuna viongozi Tanzania ambao hutafuta uongozi kwa sababu ya masilahi ya kibinafsi. Wakati mwingine jambo hili hunifadhaisha.
Wakati mwingine halinifadhaishi sana kwa vile kama ninavyosema mara kwa mara, huwezi kuyawekea sheria mawazo. Halmashauri kuu ya chama inaweza ikatoa mwongozo juu ya tabia za viongozi.
Hivi ni vizuri. Hii inaweza ikachukua nusu saa, saa moja au wiki, si kitu haichukui muda mrefu. Baada ya hapo kikao cha Bunge kinaweza kikaipitisha hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya sheria. Kujitolea kwa upande mwingine ni jambo la moyo.
Mara nyingi rafiki zangu hunilaumu ninaposema ujamaa ni imani ya moyo lakini kujitolea ni jambo dhahiri. Kwa mtu kuukubali na kujitolea inachukua muda mrefu sana.
Swali: Uongozi maskini kwa mfano hapa Tanzania ni rahisi kukaribisha rushwa. Viongozi watokao kwenye jamaa kubwa na wenye matatizo mengine hukabiliwa na wajibu ambao hauwatokei viongozi wa huko Magharibi. Je, hivi sasa hapa rushwa ni tatizo kubwa kiasi gani na vipi mnajaribu kujikinga nalo?
Jibu: Kwanza kabisa hebu niseme kuwa ni kweli watu wetu wana matatizo, wajibu unaotokana na ukubwa wa ukoo. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya watu wetu ni wale waliopo vijijini na kwamba tunaanzisha uchumi wa kifedha na ni wafanyakazi tu wenye fedha.
Haya yanatuletea matatizo makubwa. Mfanyakazi maskini, licha ya kiongozi ana mzigo mkubwa, kuna ndugu zake wanataka fedha na hawana fedha hizo. Mara nyingi wanakuwa na chakula cha kutosha lakini hawana fedha na hili ni tatizo kwa mfanyakazi.
Pengine viongozi katika nchi zilizoendelea zaidi hawana tatizo hili. Lakini basi, inapokuja kwenye suala la rushwa mbona viongozi katika nchi za Magharibi wana tamaa zao?
Kwa sababu hiyo nisingesema kwanba kiongozi Tanzania anatamanishwa zaidi kuliko kiongozi wa Amerika au Uingereza. Wao wana tamaa tofauti na wanaweza wakawa walaji rushwa pia.
Kwa hiyo tunayo mambo ya kusababisha rushwa Tanzania. Nafikiri ugonjwa wa rushwa tunao kiasi. Ni kweli kwamba tunayo sifa ya kuwa afadhali kuliko nchi nyingi Afrika.
Hii haitoshi; mimi sipendi sifa za aina hii. Haitoshi. Sisi Watanzania lazima tujiambie wenyewe kwamba tunayo imani; lakini kiasi gani viongozi wetu wanaiafiki imani hiyo?
Nafikiri tungegundua kwamba hatuiafiki sana imani hiyo. Rushwa ipo kiasi fulani; vipi tunaweza kuepuka kutokana nayo, sijui.
Lakini ningefikiria kuna njia mbili: kwanza, kutumia sheria kwa dhati. Pili, elimu. Mimi naamini elimu. Lazima kuelimisha watu kufahamu kwamba mambo fulani ni mabaya.
Hii haihusiani kabisa na ukubwa wa ukoo na wajibu utokanao na hili au lile. Mtu lazima aamini kwamba rushwa ni makosa. Lazima aseme: “Mimi ni kiongozi kwa hiyo siwezi kukubali kuhongwa.”
Hizi ndizo njia mbili. Nafikiri elimu ndiyo bora na yenye kuaminika zaidi. Usipofuata njia hiyo iliyo baki ni kujaribu kuondoa ulaji rushwa kwa kuwatia watu adhabu kwa mujibu wa sheria.
Swali: Siasa ya kujitegemea na utaifishaji wa viwanda mbalimbali baada ya azimio la Arusha imeleta matokeo makubwa katika uwekaji wa mitaji katika biashara na viwanda. Je, ukubwa wa matokeo ya mpango huo umekuwa kama ambavyo ungekuwa kama ungetokea kwenye mitaji ya watu binafsi au zaidi kama ambavyo hutegemewa kutokea kutokana na mitaji iwekwayo kwenye mali ya umma?
Jibu:Nadhani inawezekana kusema kuwa ingekuwa uwekaji wa rasilimali hizo ungetokea mikononi mwa mabepari wachache, labda wangepata faida zaidi.
Bila shaka wangefanya bidii kubwa ya kuendeleza rasilimali hiyo. Kama ambavyo nimekuwa nikisema tukijisahihisha wenyewe tutaweza kusema kuwa ingawa tumekuwa na bidii sana ya kueleza lengo letu na aina ya jamii tunayotaka kujenga, tungeweza kutimiza mipango yetu ya maendeleo kwa ubora zaidi.
Kwa hiyo nafikiri tunaweza kusema bila wasiwasi tungeweza kufanya vizuri zaidi.
Lakini kwa upande mwingine kuna usemi mwingine wa Kiingereza usemao: “Tungeweza kufanya vibaya zaidi!”
Swali je, nini jibu lako kuhusu usemi kuwa maendeleo ya kijamaa katika nchi maskini yanaleta mgawanyo sawa wa umaskini? Haya kusema kweli si mawazo yangu bali ni mawazo ya watu wengi.
Jibu: Nafikiri jibu halisi la swali hilo kinyume na jibu la maneno matupu ni kujenga jamii ya kijamaa kutoka kwenye umaskini. Hili ndilo jibu lake hasa.
Kama ningekubaliana na mawazo kwamba haiwezekani kujenga nchi ya kijamaa kutokana na nchi maskini, basi nisinge jaribu. Lakini mimi naamini kuwa tunaweza.
Kuna fikra kuwa wanaotulaumu pengine wana haki ikiwa ni walaumu wa kweli. Ikiwa siasa ya ujamaa maana yake ni usawa kamili, basi huo haupo hapa. Sinao.
Kama ningejaribu kuuanzisha hivi sasa, basi ina maana kuwa ningekuwa ninagawanya umaskini sawa. Kwa hiyo basi, nchini Tanzania nina jamii ya watu wasio sawa.
Usawa utapatikana nchini wakati umaskini utakapopungua na kupungua kwa kweli ni maendeleo tu pekee yanaweza kuleta usawa huu.
Kwa hiyo kwa upande huo wale wasemao kuwa kutangaza siasa ya ujamaa katika nchi maskini hakuwezi kuleta ujamaa wana haki, kwa sababu ujamaa ni usawa na kama ninyi ni maskini mnaloweza kufanya ni kugawana ufukara tu.
Tanzania si jamii ya watu walio sawa kwa sababu bado kuna tofauti kubwa sana ya mapato. Njia pekee tunayoweza kuitumia kuondoa tofauti hizi na kujenga jamii ya watu sawa ni ile ya maendeleo tu, kwa hiyo mpaka hapo wale ambao wanatulaumu wana haki.
Lakini ikiwa wanayosema ni kuwa tusiendelee kabisa kutoka katika hali hii na kujenga jamii ya kijamaa na tuwe na vitu vingi vitokanavyo na unyonyaji na nguvu ya kibepari na kuweza tu kuongea juu ya ujamaa tukishafika katika hali iliyonayo Ujerumani Magharibi, Uingereza au Amerika.
Hii naikataa. Naikataa kwa sababu zilizo wazi. Kwa hiyo hapa unavyoniona ninajaribu kujenga jamii ya kijamaa kutokana na nchi iliyo maskini na ambayo haijaendelea.
Swali: Mnajaribu kujenga ujamaa wenu kwa kutumia njia ya hiari, lakini katika nchi nyingi ujamaa umejengwa kwa njia ya mabavu- mabavu makubwa. Ni nini kinachofanya uamini kuwa Tanzania inaweza kuwa tofauti, na kwamba si lazima wala haitakuwa lazima kutumia nguvu?
Jibu: Kwa kweli kwa fikra tu jibu ni rahisi. Ni kwamba, kwa tafsiri ujamaa ni siasa ya watu huru. Watanzania wanaweza wasiwe huru hivi sasa; hawana kiwango cha uhuru unachokikisia katika jamii ya kijamaa.
Licha ya yaliyotokea sehemu nyingine tafsiri hasa ya ujamaa inakataa kabisa utumiaji wa mabavu.