Kifo ni mauti, ni hilaki. Ni tukio au tendo la kufikia mwisho wa uhai. Ni tendo la lazima kutokea kwa binadamu. Kwa hiyo kila nafsi itaonja mauti. “Inna Lilah Wainna Lilah Rajuun.” Yaani, sisi wote ni waja wa Mwenyezi Mungu na hakika kwake tutarejea. 

Binadamu hapendi na anaogopa kifo kisimfike, kwa sababu kinaondoa uhai wake. Anapenda uhai ili apate nafasi kutenda mambo yake na kufurahia anasa za duniani. Mambo ambayo si aliyoagizwa na kusisitizwa kuyatenda na Muumba wake. 

Mwenyezi Mungu amemuumba binadamu na kumpa sharti moja kubwa la kumwabudu yeye kila siku katika kipindi chote cha uhai wake. Lakini binadamu anafanya ajizi na kusahau kuabudu. Kifo kinapotokea ni kumkumbusha arejee kwa Mungu wake. 

Kifo si tendo linalomfurahisha binadamu kama lilivyo tendo la kucheza ngoma, kufunga goli au kuhubiri siasa jukwaani. Ni tendo linalojaza taharuki, huzuni na kilio kwa mfiwa. Kifo huonekana ni adui wa uhai, kwa sababu kinapotokea uhai wa binadamu unakwisha. 

Siku zote kifo ni mgeni na hazoeleki kwa binadamu. Hata kwa wacha Mungu na washindao misikitini, mahekaluni na makanisani kwao pia ni mgeni asiyezuilika kuwafikia. Hakika kifo hakina hisani, huruma wala aibu na woga kutua kwa mtoto, kijana, mzee, maskini au tajiri. 

Kwa vile kifo ni tendo la kufikia mwisho wa uhai, binadamu hajazi hamu au shauku kama anavyojaza simulizi ya maisha, ndoa au uhusiano. Simulizi ya kifo hujazwa huzuni, kilio na maombolezi, ambayo hujenga mazingira ya ukimya eneo la tukio, na mzizimo katika mwili wa binadamu. 

Ukiwasikia au ukiwaona wanadamu wanatabasamu au wanashangilia kifo nyumbani mwao au katika jamii yao, fahamu na utambue wana jambo au wana dalili ya kuwa kama maafkani! Kifo si burudani, si kete ya ushindi. Ni faradhi. Vipi wafurahie? Hii si maana ya “Kifo cha wengi harusi.” Tafakari. 

Waswahili tunasema: “Kifo ki kisogoni mwako.” Yaani, mwanadamu kufa ni jambo jepesi, ni kama vile anatembea na kifo, hivyo tunaaswa tusijione hai na kusahau ukweli huu. Kwa mantiki hii hupaswi kumwombea au kumtangazia mwenzako kifo. Acha papara, dunia pana na ina mapito.

Kumtangazia binadamu mwenzako kifo ni laana kutoka kwa Mungu. Kumwombea kifo kimfike binadamu mwenzako ni uadui na uhasama. Nani anakupa jeuri na mamlaka hayo? Mtanzania mwenzangu tuchunge ndimi zetu. Tuchague ya kusema. 

Watanzania katika umoja na utaifa wetu tuna mila na desturi za kutambuana, kuthaminiana, kuheshimiana na kujaliana ubinadamu wetu, kwa sababu binadamu wote ni sawa na tunayo haki sawa ya uhai. Kutia dosari uhai wa Mtanzania ni kumvunjia hadhi na heshima yake. 

Mtanzania mmoja hivi karibuni alitoa maelezo hadharani kuwa “Mungu wake” amemuotesha aseme kuwa kiongozi wa nchi asipojirekebisha au kuacha kufanya mambo yake kwa wananchi atakufa kabla ya mwaka 2020. Wenzake katika umoja wao wakashabikia na kutangaza hadharani. 

Watanzania wazalendo tukashikwa fadhaa na taharuki, kusikia peke peke mitaani kiongozi huyo mgonjwa mahututi. Ama!  Kumbe si kweli. Si kweli. Si kweli. Ghafla, mwotaruya na wenzake katika umoja wao, wakaondoa maelezo yao ya uzandiki hadharani, baada ya kutanabahi ‘jicho la busara’ litawaangazia na kuwatia hatiani. 

Iwapo ruya yao ni ya kweli, vipi waondoe maelezo yao na wao kuingia mitini? Hapa pana jambo na namna. Hii si dalili njema kwa taifa letu. Wananchi wazalendo tusikubali kuacha azima yetu ya kujenga nchi ya viwanda na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Watanzania tusikubali kudanganywa eti binadamu fulani kateremshiwa wahyi na Mwenyezi Mungu. Wakati wa mitume na manabii kuteremshiwa wahyi katika njozi umepita. Tafadhalini na chonde chonde wanasiasa muache kujitangazia wahyi kwa lengo la kuleta ghasia  na vita nchini.