Chama cha Wazee Waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia wameziomba asasi za kiraia kuwasaidia katika mapambano ya kudai haki zao ambazo wangependa wazipate kabla hawajapoteza maisha.
Akizungumza na JAMHURI, Katibu Mkuu wa chama hicho, Steven Chacha, amesema wakijitokeza wadau wa kuwasaidia kusukuma mbele gurudumu la kufanya mali za wazee hao zipatikane haraka itakuwa imesadia sana wazee hao kuishi katika mazingira mazuri kuliko wanavyoishi hivi sasa.
“Wapo wenzetu wengi ambao wametangulia mbele ya haki bila kupata haki zao. Tuna wasiwasi na sisi wachache tuliobaki tunaweza kufariki dunia kabla hatujapata haki zetu. Ndiyo maana tunaomba msaada, maana na sisi nguvu zinatuishia,” amesema mzee Chacha.
Chacha amesema awali chama chao kilikuwa na wanachama 8,560 lakini hivi sasa wamesalia 168 tu. Amesema baadhi yao wamefariki dunia na kuacha wajane na watoto ambao nao wanaishi katika hali ngumu sana.
“Hatuna msaada kutoka kokote… hatuna fedha za kujikimu, matibabu au kugharamia mazishi ya mwenzetu pale mmoja wetu anapofariki dunia,” amebainisha.
Amesema kutokana na hali yao ya uzee na kuishi katika mazingira magumu wamekuwa
wakiugua mara kwa mara.
“Ndiyo maana tumekuwa tukiomba serikali ifikirie kutupatia bima za afya ili angalau tuweze kuwa na uhakika wa matibabu tunapougua, maana hatuna njia yoyote ya kutuingizia kipato, nguvu zimetuishia na tumezitumia nguvu hizo kuipigania nchi,” amesema.
Amesema wapo baadhi ya wanachama wao ambao wanaishi mikoani na huko hali ni mbaya pia.
“Kuna baadhi ambao ndugu zao wamejitolea kuwalea baadhi ya watoto wao,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa jitihada zake na kushirikiana na baadhi ya wazee hao walifanikiwa kurejesha baadhi ya mali za chama hicho zilizomo katika mikoa mbalimbali ingawa zingine bado zinatumiwa na serikali kwenye halmashauri.
Amesema hivi sasa wanashukuru Wizara ya Mambo ya Ndani imeanza kufuatilia suala hilo kwa lengo la kuwasaidia wapate mali zao zilizochukuliwa na baadhi ya halmashauri.
“Zamani tulikuwa vizuri tu, maana tulikuwa na rasilimali lakini kuna baadhi ya viongozi waliturubuni, wakatuingiza katika mikataba mibaya tukapoteza kila kitu, sasa tumebaki tunahangaika,” amefafanua Chacha na kuongeza: “Kutokana na hilo ulizaliwa mgogoro mkubwa kuhusu kiwanja cha Upanga, serikali ikaingilia kati ikawaondoa wale waliotaka kutudhulumu ingawa jengo lililokuwepo lilivunjwa.”
Mzee mwingine, Ezekiel Chacha, amesema kuna wajanja wachache ambao wanajinufaisha kwa kutumia mali zao ambazo sasa zimewekwa chini ya RITA (Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini).
Akizungumzia matatizo ya chama hicho, Msajili wa Vyama katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Jesca Shangana, amesema ofisi yake inazifahamu changamoto za wazee hao na wizara imeshaanza kuzishughulikia.