Dunia inatawaliwa na wenye maarifa
Tupo katika kipindi ambacho kuwa na maarifa ni jambo muhimu mno. Dunia ya sasa inatawaliwa na watu wenye maarifa. Bila kuwa na maarifa utajiweka katika wakati mgumu sana.
Maarifa yatakufanya uongoze kila unapokwenda. Maarifa yatakufanya upendwe na watu. Watu watahitaji kuwa karibu nawe muda mrefu. Maarifa yatakufanya uwe kinara. Maarifa yatakufanya uwe mbobezi. Maarifa yatakufanya uitwe gwiji.
Magwiji wote ambao dunia ya leo inafurahia kazi zao walikuwa, na wengine ni watu wenye maarifa. Vijana ambao wanafanya vitu ambavyo magwiji wa dunia walifanya binafsi nawaita Vijana wa Maarifa.
Imesemwa mara nyingi kuwa maarifa ni nguvu, maarifa huwa nguvu hasa pale yanapotumika. Kuwa na maarifa na yasitumike haiwezi kuwa nguvu, bali ni hasara. Charles Darwin alikuwa sawa aliposema kitu kisipotumika kwa muda mrefu hupotea au huishiwa nguvu. Hivyo, maarifa yasipotumika nayo pia hupotea.
Maarifa ndiyo yametatua matatizo mengi yanayotuzunguka. Maarifa ndiyo yametatua migogoro mingi katika jamii zetu, maarifa ni hekima. Wanasema hekima ni matumizi ya maarifa kutatua changamoto zinazotuzunguka. Watu wenye maarifa katika jamii zetu ndio watu tunaowaona kama watu wenye hekima.
Watu wenye maarifa hutumia muda wao mrefu kufikiri namna ya kukumbana na changamoto na kuzitatua. Ni wazi kuwa kuna wakati unaweza kuona kitu kinafanyika mahali fulani na ukasema ‘hata mimi niliwahi kufikiria kufanya jambo hilo, lakini sikufikiria kama linaweza kuwa na matokeo makubwa kiasi hiki.’ Alichokuzidi huyu aliyeanzisha kitu hicho ni maarifa na taarifa. Wewe ulitaka kufanya kitu juu juu, lakini mwenzako alizama ndani na kuchimba zaidi.
Kama huna maarifa, kama hutumii nguvu na hata kipato chako kuwekeza katika maarifa, jiandae kubaki nyuma siku zote. Wale unaowaona kila kukicha wanapiga hatua jua kwamba wamewekeza katika maarifa.
Tupo katika zama ambazo mashine zinakuja kwa kasi na kuondoa watu kazini. Kazi iliyofanywa na watu watatu ndani ya siku mbili inafanywa sasa na mashine moja, ndani ya saa kadhaa, kazi imekwisha. Kadri teknolojia inavyokua, mashine nyingi zinaanza kufanya kazi za watu, hivyo kutakuwa na watu wengi sana wanaokosa kazi kwa sababu kazi zao zitafanywa na mashine.
Zamani ili ufanyiwe upasuaji walihitajika madaktari wasiopungua watatu. Upasuaji kama huo leo unahitaji daktari mmoja anayetumia muda mfupi. Mambo yamebadilika!
Ukiwa na maarifa katika kipindi kama hiki si rahisi kutoka kazini, ni wewe kujifunza kuendana na mifumo yake. Wale ambao hawako tayari kujifunza maisha kwao yatawabadilikia. Uzuri ni kwamba mashine haiwezi kufikiri kama anavyoweza kufikiri mwanadamu mwenye maarifa. Yenyewe imetengenezwa kwa mfumo wa kufanya kazi kwa namna fulani. Mtu mwenye maarifa mahali popote atategemewa kwa sababu uwezo wake wa kuzalisha utakuwa mkubwa.
Kusema kwamba mashine zinawatoa watu kazini simaanishi watu walioajiriwa tu, bali hata wewe uliyejiajiri kama huna maarifa jiandae kuona biashara yako au kazi yako inakufa na inatawaliwa na watu wenye maarifa – inafanywa na watu kwa viwango na ubora wa hali ya juu.
Siyasemi haya kumtisha mtu, bali ni kujiandaa na yale yanayokuja mbele. Lisemwalo lipo, kama halipo basi linakuja.
Kuna watu ambao wanafikiri kwamba wakihitimu shule mambo ya kujifunza yamekwisha, wanasahau kuwa shule rasmi huanza pale wanapohitimu. Maisha ni shule ya kila siku. Hatupaswi kuacha kujifunza kwa sababu maisha yenyewe huwa hayaachi kutupa mambo ya kujifunza.
“Watu wengine wanakufa wakiwa na miaka 25 na hawazikwi hadi wanapofikisha miaka 75,” alisema Benjamin Franklin. Kuacha kujifunza ni sawa na kukaribisha kifo ukiwa bado hai, unakuwa mfu anayetembea (walking dead). Kuna ambao ni vijana na wameamua kuwa wazee na kuna wazee ambao bado ni vijana.
Kutokuwa na maarifa ukiwa kijana ni kujizeesha mapema, unakuwa umepitwa na wakati. Si jambo jema kama kijana kuitwa mtu aliyepitwa na wakati. Mambo yanapobadilika ni lazima na wewe ubadilike.
Wahenga walisema, “Elimu ni bahari.” Elimu haina mwisho. Jambo jema kuhusu maarifa ni kwamba yanapatikana kila kona, hayajifichi. Maarifa yapo vitabuni, maarifa yapo kwenye intaneti, maarifa wanayo watu wanaokuzunguka.
Ishi katika kutafuta maarifa, maarifa ni ufunguo wa mafanikio katika mlango unaoitwa maisha.