Uwekezaji wa kampuni zinazotoa huduma za simu za mikononi umefikia Sh trilioni 6 ambazo zimekuwa na tija kubwa kwa taifa na kuifanya sekta ya mawasiliano kuwa miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi kubwa hapa nchini.
Wakati uchumi ukikua kwa asilimia 7.2 katika robo ya pili mwaka huu, takwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) zinaonyesha kuwa sekta ya habari na mawasiliano ilikua kwa asilimia 10.3.
Huu ulikuwa ni ukuaji wa kasi wa tatu baada ya shughuli za ujenzi (asilimia 19.6) na madini (asilimia 17.2) hasa kutokana na wateja wa simu za viganjani kuongeza ununuzi wa muda wa maongezi. Ukuaji wa sekta ya habari na mawasiliano pia ulichochewa na kupanuka kwa shughuli za utangazaji na huduma za intaneti ambazo zimeimarika na kusambaa sana kupitia simu za mikononi.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Makampuni ya Simu za Mikononi Duniani (GSMA), sekta hii ni moja ya biashara nzuri Tanzania zinazotengeneza faida kubwa.
GSMA inafafanua katika ripoti yake kuwa pesa zilizowekezwa na kampuni hizo hadi sasa zimetumika kwa kiasi kikubwa kujenga miundombinu ya mitandao ya mawasiliano, matumizi ya teknolojia za kisasa na kuweka mifumo mbalimbali ya huduma za kidijitali kama vile huduma za pesa mtandaoni.
Umoja huo unaongeza kwamba teknolojia ya mawasiliano ya simu za mikononi pia imekuwa mhimili muhimu wa mabadiliko makubwa ya kidijitali yanayoendelea kutokea humu nchini. Kati ya faida nyingi zilizopatikana kutokana na uwekezaji na mabadiliko haya ni pamoja na kuwepo kwa huduma mbalimbali zilizoleta nafuu kubwa kimaisha, kurahisisha shughuli za biashara, kuongeza tija na ufanisi kwenye sekta mbalimbali na kuimarisha utawala bora.
“Sekta ya mawasiliano ya simu za mikononi pamoja na teknolojia yake vimetoa mchango mkubwa kwenye kukua kwa uchumi na maendeleo ya jamii. Mwaka 2016, thamani iliyoongezwa na kampuni za simu kwenye pato la taifa (GDP) ilikuwa dola za Marekani bilioni 2.5 ambazo zilikuwa sawa na asilimia 5.2 ya pato lote. Pia sekta hii inaajiri zaidi ya watu milioni 1.5, moja kwa moja na kupitia shughuli zingine ambayo ni kama asilimia 2.6 ya watu wote nchini,” inasema ripoti ya GSMA.
“Tanzania ni moja ya masoko makubwa ya pesa mtandaoni barani Afrika na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na kampuni za simu za mikononi ambazo pia zinashirikiana kwa karibu sana kuwahudumia wananchi,” GSMA inafafanua zaidi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, pia Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye masoko yenye ushindani mkubwa katika biashara ya mawasiliano ya simu za mikononi miongoni mwa nchi zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hadi Juni mwaka huu, kulikuwa na kampuni nane zilizokuwa zinatoa huduma hizo nchini lakini kwa sasa zimebaki kampuni saba baada ya moja kuzidiwa na ushindani na kufunga biashara yake hivi karibuni.
Msemaji wa TCRA, Semu Mwakyanjala, aliliambia JAMHURI wiki iliyopita kuwa kampuni hiyo ni Benson Informatics ambayo ilijulikana kibiashara kama Smart.
Mwakyanjala alizitaja kampuni zilizobaki kuwa ni Airtel, Halotel, Tigo, TTCL, Vodacom, Zantel na Smile. GSMA inasema kwa sasa hivi asilimia 96 ya soko la mawasiliano ya simu za mikononi imekamatwa na kampuni nne ambazo ni Airtel, Halotel, Tigo and Vodacom.
“Mwaka 2017, kampuni za simu za mikononi zilitengeneza mapato ya pamoja yenye thamani ya Sh trilioni 2.9 (sawa na dola bilioni 1.25), ambayo asilimia 15 yake iliwekezwa kuiboresha na kuipanua mitandao yao,” ripoti ya GSMA inasema na kuongeza:
“Uwekezaji katika kujenga miundombinu ya mitandao na kutoa huduma mbalimbali kupitia simu za mikononi ndio msingi mkubwa wa sekta hii kuchangia katika maendeleo ya Tanzania. Hadi sasa kampuni za simu za mikononi zimewekeza takriban Sh trilioni 6 (sawa na dola bilioni 2.6) nchini.”
Takwimu za TCRA zinaonyesha kuwa Vodacom Tanzania ndiyo iliyokuwa kinara wa biashara ya huduma za mawasiliano kufikia katikati ya mwaka huu, kwa kuwa na asilimia 33 ya laini zote za simu zilizokuwa sokoni. Ya pili ilikuwa Tigo na asilimia 27, halafu Airtel (asilimia 26), huku Halotel, Zantel na TTCL zikiwa na asilimia kumi, tatu na moja mtawalia.
Hadi Juni mwaka huu, laini za simu za mkononi zilizokuwa zinatumika ni zaidi ya milioni 43.6 ukilinganisha na milioni 39.6 za Desemba mwaka 2015. Wakati mtu mmoja anaweza kumiliki zaidi ya laini moja, GSMA inasema idadi ya watu wenye simu za mikononi nchini imeongezeka kutoka watu milioni tano mwaka 2007 hadi watu milioni 25.2 sasa hivi.
Kwa upande wa huduma za kifedha, GSMA inasema ubunifu na uvumbuzi wa hali ya juu hasa wa pesa mtandaoni ni miongoni mwa faida na matokeo lukuki ya kijamii na kiuchumi yaliyoletwa na uwekezaji wa makampuni ya simu.
Huduma ya pesa mtandaoni ilianza kutolewa rasmi nchini mwaka 2008 na kufikia Juni mwaka 2018, kampuni sita ambazo ni Airtel, Halotel, Tigo, TTCL, Vodacom na Zantel zilikuwa na akaunti za huduma hiyo zifikiazo milioni 21.
“Akauti za pesa mtandaoni sasa hivi zimefika milioni 23 kutoka milioni 22.7 mwezi Aprili, hali inayoonyesha kuenea kwa huduma za kifedha miongoni mwa Watanzania.
Huduma za pesa mtandaoni zinatolewa na mitandao sita kati ya saba inayotoa huduma za simu za mkononi,” TCRA inadokeza kwenye jarida lake la The Regulator, toleo la Julai – Septemba, 2019.
Mitandao hiyo ni Vodacom (M-Pesa), Tigo (Tigo Pesa), Airtel (Airtel Money), Halotel (Halopesa), TTCL (T-Pesa) na Zantel (Ezy Pesa).