Ndugu Rais, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere siku zote aliwaita watu wake kwa majina yao wenyewe. Alisikiwa sana. Tujaribu leo, labda tutasikiwa.
Palikuwa na mtu katika nchi ya Tanganyika jina lake aliitwa Juliyasi. Mtu huyu alikuwa mkamilifu na mwenye uelekevu aliye mcha Mungu na kuepuka uovu! Aliwafundisha Watanganyika kuwa na upendo, umoja na mshikamano akiwaasa kila mara katika mafundisho yake kuwa wao ni ndugu.
Kwa mafundisho hayo yaliyompendeza Mungu akawa ameijenga Tanganyika ambayo ilikuwa moja zaidi. Aliwaambia ili waendelee walihitaji vitu vinne – Watu, Ardhi, Siasa Safi na Uongozi Bora. Akawasisitizia kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo. Leo hayupo kati ya haya ni lipi tunafafana nalo? Amekwisha kwenda, nayo yamekwisha kwenda! Kweli pasipo maono taifa huangamia. Na pasipo washauri taifa huanguka. Naiombea nchi yangu rehema kwako, ee Mungu!
Ili tuendelee Juliyasi alisema tunaihitaji ardhi. Ardhi tunayo. Aggrey wa Tabora anasema inafukuliwa mpaka inalia! Alisema tunahitaji watu. Watu ndiyo sisi. Viongozi wetu wanahangaikia vitu. Tunaonekana kama magari modeli ya zamani yaliyokosa matengenezo. Alitaja na siasa safi. Watanzania wanaugulia kwa siasa za kujimwambafai. Akasema na uongozi bora. Tangazo kuwa watakaowatangaza washindi kutoka upinzani watanyang’anywa magari na mishahara ni tangazo mufilisi. Mfano bora wa viongozi wasio bora. Hakuna kiongozi aliyekuja na chochote kutoka kwa wazazi wake. Wanapaswa kutambua kuwa katika wakati wao huu kama hawakuhakikisha kuwa wanayafanya haya manne kutimia, wajue wanapuyanga tu. Kung’ang’ania kununua mwezi kuuteremsha chini ni uthibitisho kuwa baadhi hawajatimia!
Palikuwapo tena na mtu katika nchi ya Tanzania, aliyeitwa Abdulrahman. Alikikuta Chama Cha Mapinduzi juu ya mawe. Kilikuwa kama shati lililokuwa linaliwa na ng’ombe naye akawahi kulichomoa. Kilikuwa ni tambala bovu, hakifai. Chama ndiyo kinaunda serikali, hivyo alijua chama legelege huunda serikali legelege. Alianza kwa kuhakiki utendajikazi wa viongozi. Akawakagua mawaziri wote na wote wabovu akawashitaki kwa Mwenyekiti wake ambaye pia alikuwa ni Rais, hadharani. Akawaita mawaziri wale wabovu kuwa ni mizigo! Ni mizigo kwa serikali, lakini ni mizigo zaidi kwa wananchi. Alitaka neno busara la viongozi bora litimie ili nchi iendelee. Akafanikiwa kuirudisha imani iliyokuwa imepotea. Mkutano Mkuu wa CCM uliokuwa unapitisha jina la mgombea urais, lilipotajwa jina la Abdulrahman, ukumbi mzima ulilipuka kwa vifijo na nderemo kumshangilia kwa kazi nzuri, kubwa aliyokifanyia chama. Wakamwita, ‘jembe, jembe, jembe! Sasa jembe limeenda. Bashiru onyesha kama nawe unalima.
Akifuatilia fikra sahihi za mwenyekiti muasisi wa CCM kuwa kilimo ni uti wa mgongo, Abdulrahaman aliizunguka nchi yote akitembea kila kijiji, akila na kunywa walivyokula masikini. Akawakusanya vijana waliokuwa hawana kazi, akawafungulia mashamba walime. Kama matumizi ya fedha yanayofanywa sasa yangeelekezwa katika kilimo, kijana gani angesema amekosa ajira? Tuliandika tangu zamani kuwa bonde, kwa mfano la Mto Rufiji yangefunguliwa mashamba makubwa vijana wakawezeshwa wakakabidhiwa kulima, nchi hii ingezalisha chakula cha kuitosheleza dunia huku vijana wetu wote wakiwa na ajira. Na hapo kwa hakika maisha bora kwa kila Mtanzania yangetimilika.
Philip, Makamu Mwenyekiti na Bashiru Katibu Mkuu, zirudieni dini zenu watu wa Mungu wanateseka sana. Waelewesheni mpaka timamu waelewe kinachotafutwa kule Rufiji ni nini? Umeme usiwe kisingizio cha kuwafanya wananchi wanyonge wazidi kupukutika kwa kukosa dawa katika hospitali zetu. Wanashindwa hata kukomboa maiti! Mbona tunao umeme mpaka wakumwaga kwenye gesi yetu? Rais Uhuru Kenyatta alisikika akiomba lijengwe bomba mpaka nchini kwake tuiuzie Kenya gesi.
Kama kuchimba tulishachimba tayari. Kama miundombinu tayari.
Kama fedha kidogo tu kati ya zile nyingi zinazomwagwa kule zingeingizwa katika gesi ya kumwaga tuliyonayo, shida za nchi hii zingetoka wapi. Leo hii tusingekuwa na gari wala mitambo inayotumia mafuta. Fedha nyingi zinazotumika kununulia mafuta zingeokolewa. Ni hospitali gani ingekaa bila dawa au vifaatiba? Leo watoto shuleni wanakaa chini. Hawana vitabu, daftari, kalamu na mahali pengine hawana hata mwalimu. Hawa baadhi ya wanasiasa wanapata wapi nguvu za kudanganya wananchi hadharani kuwa duniani kuna nchi inatoa elimu bure?
Baba Bashiru wewe ndiye mtendaji mkuu wa chama chenye serikali. Kumbuka ulivyosoma wewe kwa amani. Viongozi waliokuwapo hapo ulipo walihakikisha unaipata haki hiyo yako bila kwanza kudhalilika. Unapaswa kuhakikisha kuwa hawa wadogo zako wanaopaswa kusoma sasa, wanapata haki sawa na uliyopata wewe. Binti yangu kwa ufaulu mzuri amechaguliwa kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Masomo yameanza mkopo hajapata, lakini ameambiwa ni lazima kwanza alipe ada Sh 1,300,000 na malipo mengine ndipo aingie darasani. Malipo niliyo na uhakika nayo kila mwisho wa mwezi ni pensheni yangu ya Sh 50,000. Baba Bashiru elewa kuwa adha hii siyo yangu mzazi masikini peke yangu. Tuko wazazi wengi masikini. Nimemwambia binti yangu ajipe moyo kwa kuwa kama viongozi waliopo hawatatenda haki, Mwenyezi Mungu yuko upande masikini. Utasoma mpaka mwisho wa upeo wako.
Inauma sana kuona fedha ziko nyingi, lakini zinatolewa bila utaratibu. Inawafaa nini kwa baadhi ya wanasiasa kudai majukwaani kuwa wameongeza fedha za elimu?
Baba Philip kumbuka vizuri. Nilikuambia kuwa ilipolazimu wewe kwenda Njombe kujilimia viazi, mimi na vijana wako tulifunga, tukaingia katika maombi kumwomba Muumba wetu aturudishie wewe katika uongozi. Akasikia kilio cha masikini, akakurudisha. Sasa baba, kama kwa nafasi uliyonayo huwezi kuhakikisha serikali inatenda haki kwa wakati kwa watoto wa taifa hili, utakuwa umeifaa nchi kwa lipi? Baba Philip, yaani tulazimike kurudi tena kwenye maombi na maombi tofauti kwa Muumba wetu?