Kuna watu wana msemo kuwa bahati mbaya mambo siyo, lakini sisi wahenga tunaamini hakuna bahati mbaya, bali kuna bahati tu na isivyo bahati. 

Sasa kwa bahati mazingira ya maisha yetu yanatufanya tukubali matokeo. Ukweli ni kwamba tumeanza kuyakubali na kunyooka kwa kiasi chake kwa kipindi kifupi tu.

Kuna baadhi ya semi nyingi sana zinazoambatana na vitendo zimepotea, na semi zile hazikuwa tatizo kubwa kwa watumiaji bali kwa wasikilizaji. Sitaki kusema nani kazitoa lakini ninaamini ni mfumo mzuri ambao umetengenezwa na unaendelea kutengenezwa kwa ufanisi zaidi.

Nchi iliharibika kwa kiasi fulani kutokana na watu wachache kuhodhi mamlaka zetu na kuwafanya wenye mamlaka kuwa chui wa picha katika karatasi.

Ninajua wengi mnaelewa ninasema nini lakini kwa kukumbushana tu ni kwamba nchi ilikuwa inaweza kusimama kwa muda mfupi kutokana na kauli ya mtu ambaye labda hana hata mamlaka ya kikatiba katika kuongea au kutenda. Hapa ninawakumbuka mapapaa wengi ambao walimiliki kundi kubwa la ‘wapambe nuksi’ ambao nao walikuwa miungu watu ndani ya taifa hili.

Hivi tulikosea wapi mpaka tukafikia hapo? Maswali ni mengi sana na majibu ni mengi pia, lakini ninaamini tumeona katika mikutano mingi ya viongozi jinsi ambavyo upigaji na uvunjaji wa sheria ulivyokuwa umetamalaki katika taifa letu, taifa ambalo lilikuwa huru na tuliamini katika ilani yetu ya chama kwamba kila mtu ana haki sawa na mwingine.

Julius aliposema kwamba azimio letu lilianza kuugulia Arusha na kufia Zanzibar, wengi hawakuelewa na hata tulivyoingia katika semi mbalimbali ilikuwa ni katika mtiririko wa maradhi ya kuelekea katika kifo cha kupoteza haki za watu na utu wa watu.

Watu wachache wakawa na maana zaidi kuliko taifa letu, taifa ambalo tulipigania uhuru ili tuwe huru na tupate haki zetu.

Katika kipindi chote hicho cha mpito, mambo mengi yalikuwa kama ni ya kawaida, hatukujua kama kiongozi anapaswa kuwatumikia wananchi mpaka pale tulipoanza kuona uwajibikaji na kuwajibishwa kwa kutotekeleza majukumu yao.

Tulijua kwamba vifo vya vyama vya ushirika vilitokana na msukosuko wa kiuchumi duniani kumbe ilitokana na watu wachache kuamua kutupiga mchana kweupe na kuingia mitini na fedha zetu.

Tulijua kwamba mtaji wa serikali yetu umefilisika ndiyo maana miradi mingi mikubwa inakwama kumbe hapo katikati walikuwepo wazee wa kushughulika na uchumi binafsi na kusahau kuwa miradi hiyo ilikuwa ya umma na si miradi binafsi.

Ni heshima tu ambayo tumejiwekea kama taifa ya kutofukua makaburi lakini kama ingekuwa hivyo ninaamini hata usiloliamini ungelisikia.

Yapo mambo mengi sana ambayo hatukujua kuwa yanawezekana na wanaojua sasa siyo sisi bali wao. Zamani vyeo vilikuwa vya kurithishana, kulikuwa na majina ambayo panga pangua lazima yawepo lakini leo ninaona ni juhudi ya mtu katika utendaji kazi.

Kuna watu walikuwa wanajua kuwa lazima wawepo katika madaraka hata kama walikuwa hawajui ni katika idara, taasisi, wizara au ushirika gani, hii ndiyo ninayosema tunaanza kuelewa.

Tunaanza kuelewa kwa sababu hata mahakama sasa zinapokea majina ya watu ambao zamani walisema haiwezekani kwenda mahakamani. Mahakama zilikuwa za watu wanyonge ambao hata kama wakipewa haki yao bado ilipingwa kwa nguvu ya fedha katika utekelezaji, haki ni jambo muhimu sana, ikinunuliwa watu hupoteza matumaini kwa taifa lao, hususan viongozi.

Leo nimeandika barua hii kwa kuwa kuna harufu kwa mbali ya kurudi kule ambako sote tulikuwa kitu kimoja katika kudai uhuru wa taifa letu, tulikuwa wamoja  katika kumiliki aridhi na mali za umma, tulikuwa wamoja katika ulinzi na uzalendo kabla ya ugonjwa wa ubinafsi haujaanza kututafuna.

Japo mafanikio hayo mazuri yapo, hakukosekani kasoro za hapa na pale katika kufikia malengo. Ninaamini wengi wamezungumza, kuna tatizo kubwa sana na baadhi kutwaa madaraka makubwa sana tofauti na teuzi zao kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yao. Wanawakwaza viongozi wenzao na kuwakwaza wananchi kwa ujumla.

Ni vema viongozi wetu wakawa na muda wa kupitia maandiko mbalimbali ya nyuma na kuona wenzao walifanya nini katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku. 

Baadhi ya viongozi wamekuwa wakikalia fedha za maendeleo ya wananchi kwa hofu kwamba matumizi hayatakuwa sahihi, tukumbuke maisha ni leo, tufanye cha leo.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.