Aliokota chuma chakavu kusaka ada (2)
Sir Nature akaanza kuimba peke yake akijikumbusha mashairi hayo lakini kitendo hicho kikaamsha hisia fulani ndani yake kuhusu muziki.
Hisia hizo ndizo zilimfanya awashawishi vijana wenzake watatu kuanzisha kikundi kilichokuwa likijulikana kwa jina la Four Skills Gangstar (FSG), ambacho kiongozi wake alikuwa yeye, akitumia jina la ‘Nature Man’.
Wenzake wengine katika kundi hili walikuwa ni Mark 2 B, Chriss na Dollo.
Sir Nature alikiri kuwa kikwazo cha kwanza kwenye muziki kilikuwa ni wazazi wake ambao walikuwa wakishawishiwa na majirani zao kuwa muziki ni uhuni, hivyo kijana wao angepotea.
Kutokana na hilo, Sir Nature alilazimika kupanga maneno mazuri ya kumshawishi mama yake ampatie chakula kila anaporudi nyumbani.
Lakini siku zingine mama yake alikuwa mkali hata chakula alikuwa akimnyima.
Sir Nature anaeleza kuwa wakiwa na kundi hilo walipata changamoto nyingi, ikiwemo kutembea kwa miguu umbali mrefu kutafuta maonyesho ya kuimba ili watambulike.
“Tuliwahi kutembea kutoka Posta hadi Kimara baada ya kusikia kuwa kuna onyesho la jamaa fulani linafanyika huko,” anasimulia Sir Nature.
Anasema walitoka Kurasini hadi Posta, kumbe hawakusikia vizuri, lilikuwa likifanyika Kimara. Wakalazimika kutembea kutoka Posta hadi Kimara kwa miguu.
Sir Nature aanasimulia kuwa mwaka 1999, waliingia studio iliyokuwa chini ya mtayarishaji Endrico, inayoitwa Sound Craftaz, ambapo waliweza kurekodi wimbo wa kwanza walioupa jina la ‘Jambo Hili ni Batili’.
Anaeleza kuwa mashairi ya wimbo huo yalikuwa yakilenga kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya, ambazo kwa wakati huo zilikuwa zimeshamiri.
Sir Nature anabainisha kuwa wimbo huo ulifanikiwa kusikika katika kituo cha Radio One.
Kabla ya kuupeleka studio kwa kuwa yeye alikuwa kiongozi, alilazimika kurudi mitaani kuokota chuma chakavu ili kupata fedha za kununulia kaseti ya kurekodia wimbo huo.
Anafafanua kuwa iliwachukua mwezi mzima kutafuta Sh 3,000 za kununulia kaseti tupu.
Mwaka 2000 ndoto yake ya kusoma sekondari ilikamilika baada ya kuhitimu kidato cha nne.
Hata hivyo, katikati ya mwaka huo wa 2000, kundi lao lilivunjika kwa sababu kila mmoja alitafuta njia yake kimaisha baada ya kumaliza shule.
Sir Nature anasema hali hiyo haikumkatisha tamaa kutembea kwa miguu hadi Kimara kutafuta maonyesho ya kuimba ili kujenga urafiki na wanamuziki wakubwa.
“Kipindi hicho nilidhalilishwa sana na makondakta wa daladala. Kuna wakati nilichoka nikaamua kuvaa nguo za shule, nikajifanya mwanafunzi huku nikionekana baba mzima. Nilishushwa njiani kwa kukosa nauli au kushindwa kuelewana na konda,” anasema Sir Nature.
Baadhi ya majirani na watu wanaomfahamu Sir Nature walimwona kama chizi, wakamkejeli, wakimchukulia kuwa ni mwizi, mtukutu, mvuta bangi na mambo yanayofanana na hayo, ingawa ukweli hakuwa na sifa hata moja kati ya hizo.
Jambo la kutoka kimuziki lilikuwa limo ndani ya kichwa chake, hata pale alipoambiwa kuna maonyesho Kibaha, bila kualikwa, akitumaini anaweza kupata nafasi ya kuimba hata wimbo wake mmoja, alikwenda bila kujali kama anayo nauli au la.
Kwa masikitiko Sir Nature anabainisha kuwa hakuna mtu hata mmoja katika familia yake ambaye angemuomba ampe nauli ili aende huko na kukubali, kwa kuwa walimuona ni mhuni na mpuuzi.
Lakini huo ulikuwa ni mwanzo tu, kwa kuwa hakukatishwa tamaa, baadaye alikuja kufanikiwa na kuibuka kuwa mmoja wa wasanii waanzilishi wa muziki uliokuja kuwa maarufu wa ‘Bongo Fleva.’
Baadhi ya nyimbo maarufu za Sir Nature ni pamoja na ‘Inauma Sana’, ‘Hakuna Kulala’, ‘Sitaki Demu’, ‘Kisa Demu’, ‘Utajiju’, ‘Mtoto Iddy’, ‘Nenda’, ‘Tunafanya Kazi’, ‘Mzee wa Busara’, ‘Hili Game’, ‘Hali Ngumu’, ‘Komaa’ na ‘Unga Robo’ alioshirikiana na mwanamuziki FD Q.
Nyimbo nyingine ni ‘Zali la Mentali’ alioshirikishwa na Prof. Jay, ‘Ubinadamu Kazi’, ‘Kidaruso’, ‘Bwana Misosi’ alioshirikiana na Fid Q, ‘Kiboko ya Mabishoo’, alioshirikishwa na Harmo Rapa na nyingine nyingi.
Maisha ya Sir Nature yanaonyesha dhahiri kuwa hakika penye nia pana njia. Kongole kwako Sir Nature.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada mkubwa wa mitandao mbalimbali.
Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0784331200, 0713331200, 0767331200 na 0736331200