Misemo ya wahenga ina mengi ya kufundisha, na mingi hutabiri yanayotokea kwenye jamii. Mfano, msemo kwamba panapofuka moshi chini kuna moto, una maana yake. 

Msemo huo umejionyesha ndani ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera, KCU (1990) Ltd baada ya mwanachama mmoja, asiyehadaika kwa tamaa binafsi na kuwasaliti wenzake kwa kuwaibia kilicho chao, Archard Muhandiki, kuonyesha wazi kuwa hapa kuna ufisadi.

Muhandiki alikuwa na kila ushahidi wa ufisadi huo, ambapo mwanzoni alikuwa akisema kwa uhakika kwamba ni kwa nini kifanyike kitu fulani ilhali kuna kitu cha aina ileile mahali palepale, lakini hakusikilizwa hata kidogo na huo kuwa mwendelezo wa kufanyika mambo yasiyo na tija yoyote, iwe kwa chama chenyewe wala kwa wanaushirika, wakulima wa kahawa wa Kagera.

Matokeo yake ni chama kuanza kuzorota na wakulima kudidimia kiuchumi wakati utitiri wa pesa unaonekana umetumika pasipo kuonekana kilichofanyika!

Kwa hiyo, msemo huo unaendana na kilichojiri ndani ya chama hicho kikuu cha ushirika mkoani Kagera, KCU (1990) Ltd.

Chama hicho kilifanya mambo mengi yanayoonyesha hasara bila wahusika kuitilia maanani hasara hiyo. Kwa vile waliona hakuna anayejali, basi likageuka shamba la bibi, kila anayetaka anajipakulia bila kujali kama chakula kimeiva au la.

Ndipo akajitokeza mwanaushirika huyo machachari, Muhandiki, akaona uchungu wa kwa nini mali ya wanaushirika ipotee namna hiyo bila mtu yeyote kujali.

Alipofanya mpango ili awe mmoja wa wanaohusika kwenye uongozi wa ushirika huo akaonekana si mwenzao, kwa maana ya timu ya uongozi wa ushirika huo. Akashambuliwa sana, ikiwa ni pamoja na kuzushiwa kashfa nyingi zisizomithilika.

Wapo waliofikia kusema kwamba hata yeye anatafuta kuingia kwenye uongozi wa ushirika huo kusudi akajinufaishe na kilichokuwa kikitafunwa. Ila tofauti na mawazo hayo, yeye alikuwa akionyesha kwamba hapa kuna upungufu wa hiki na pale kuna upungufu wa kile, kitu ambacho si cha kawaida kwa mtu anayetaka kupora kitu huku akionyesha jinsi kilivyokaa mahali pasipo salama.

Sababu kama angekuwa amekusudia kupora kitu asingesema kiwekwe vizuri mahali ambapo kisingefikiwa kwa urahisi. Lakini Muhandiki akaendelea kusema bila kukata tamaa huku akizongwa na kejeli za kila aina.

Aliendelea kupaza sauti akiyataja mambo yaliyoenda kombo kwenye ushirika huo hadi uongozi wa ushirika  ulipomtenga na kumzuia kuukaribia. Alionekana ni adui asiyefaa kuwa pamoja nao!

Jambo hilo la kumtenga linaonyesha kabisa kuwa yeye si mmoja wao, linamsafisha kabisa. Pengine wangemuacha akaendelea kuwa pamoja nao angekuwa kama Waingereza wasemavyo “in for it” – kwamba ni mmoja wao.

Kwa hiyo akakubali kujitenga na kuendeleza kelele zake akiwa pembeni akishirikiana tu na vyombo vya habari.

Mara likatimka timbwili la Serikali ya Awamu ya Tano kuhusu wahujumu uchumi wa nchi.  Ulipotangazwa msamaha kwa walio na pesa za wananchi, kwamba watakaokubali kurudisha wataachiwa bila kuchukuliwa hatua zaidi za kisheria, aliyoyasema Muhandiki yakaanza kujionyesha.

Ndipo ikabainika kuwa kuna pesa zilizochukuliwa na kwamba zitarudishwa! Sijui zitarudishwa kutoka wapi wakati ilishasemwa kwamba hakuna kilichochukuliwa kinyume cha utaratibu uliokuwepo!

Hapa ndipo msemo wa wahenga wa panapofuka moshi chini kuna moto ukajionyesha, na si msemo tu, ila wahusika wakaonyesha moto wenyewe ulipo wakiwa wamedhamiria kuuzima!

Sasa tumfikirieje huyu aliyekuwa akiwaambia wenzake kuwa pale ni lazima kuna moto huku wengine wakitaka kumtoa macho? Kwa nini mtu huyu asipewe nishani ya aina yake ya ujasiri baada ya wahusika kukiri na kukubali kukirudisha walichokipoteza?

Ila bado Muhandiki hakubali kuwa kilichosemwa kurudishwa ndicho kilichoporwa. Anaendelea kuwapigania wakulima akisema kilichopotezwa ni kingi zaidi. Maadamu anasema ushahidi anao, tusubiri tuone hatima yake.

La kuzingatia ni kwamba misemo hiyo ya wahenga haituachi watupu, yapo mengi inayotuachia.

Nani alidhani kuwa ipo siku watu hawa wangekubali wenyewe kuwa walipora pesa za wakulima na sasa watazirudisha pesa hizo, wakati mwanzoni walikuwa wakikataa katakata kufanya ufisadi huo?

Kama tunavyoyaona na kuyashangaa hayo, pia tusije kuyashangaa haya anayoyasema Muhandiki kwa sasa kwamba kilichosemwa kurudishwa hakifikii hata robo ya kilichochukuliwa.

Mimi ninadhani Rais Dk. John Magufuli, angebuni nishani za kuwatunukia watu wanaojitoa mhanga kukabiliana na wahujumu uchumi. Vita aliyopigana Muhandiki kuhakikisha uchumi wa wananchi, hasa wakulima wanyonge, unalindwa ni kubwa, ni vita inayostahili nishani.

Kama ambavyo rais alibuni mbinu ya kutangaza msamaha kwa wanaoshitakiwa kwa uhujumu uchumi kurudisha pesa waliyoifisidi na kuachiwa, vilevile angebuni namna ya kuwapatia nishani wanaowezesha kukabiliana na wahujumu uchumi ili kulifanya hilo kuwa zoezi endelevu.