Huwa ninakumbuka sana kauli ya rais wetu anapowatahadharisha watu kwamba hivi hawajui kuwa mambo yamebadilika? Na kuna wakati huwa ninajiuliza, hizi kampuni binafsi zinajua anamaanisha nini? Kama taifa inabidi tusimame pamoja na siku moja tuseme hapana, inatosha kwa mambo kadhaa yanayojitokeza.

Nimeamua kushika kalamu kwa sababu kuna jambo limenikera sana. Watanzania kwa ujumla wetu tumekuwa wanasiasa wa habari za zima moto kila siku, tumegeuza maisha yetu kuwa siasa hata mahali ambapo hapastahili siasa. Sisi ndio Watanzania wepesi wa kusahau kilichotokea jana na wepesi wa kutoa lawama kwa jambo ambalo kila mmoja anaweza akalisimamia.

Miaka kadhaa iliyopita, wakati wa siasa ya ujamaa na kujitegemea, sera ya biashara ilikuwa ni suala la serikali kufanya na kusimamia, serikali ilifanya biashara zote na huduma zilikuwa nzuri sana, tunaokumbuka tupo na tunaweza kuishauri serikali jinsi ya kurudisha mfumo wa biashara kuwa wa serikali katika mambo fulani fulani, kila kitu kinawezekana.

Siku za hivi karibuni serikali iliunda taasisi ambayo kimsingi ilipaswa kusimamia biashara huria ya mafuta, hii ni biashara muhimu sana kwa mustakabali wa uchumi wa taifa lolote lile, suala la mafuta likichezewa linaweza kuyumbisha uchumi wa taifa. Tulianza japokuwa kulikuwa na ukinzani mkubwa lakini hatimaye tulifanikiwa, tunajua vikwazo vya kimizengwe vilivyojitokeza.

EWURA ni chombo chetu ambacho kinaratibu gharama za mafuta kwa kampuni kubwa ambazo zingeweza kuitafuna nchi yetu kwa ujanja wa umoja wao. Hiki ni chombo ambacho kinasimamia haki baina ya wananchi na wenye mitaji ya mafuta. Ni chombo ambacho kinasimamia mapato ya taifa letu kwa niaba ya Watanzania wote.

Kwanini leo nimeamua kuandika waraka huu na kuwataka hawa wenzetu wachukue dhima zaidi katika kusimamia suala la mafuta?  Kuna wajanja wachache ambao bado hawajagundua kuwa mambo ya ujanja ujanja yamebadilika, hayapo tena, japo kwa muda mfupi wanajaribu ujanja na kufanya biashara ya faida kubwa pasi na haki ya wananchi na kukwepa uwepo wa EWURA.

Mimi ni mnunuaji mzuri wa mafuta, si lazima yawe ya gari, lakini kitendo cha baadhi ya vituo vya mafuta kusitisha kuuza mafuta kwa muda kwa kigezo cha kutokuwa na mafuta lakini lengo lao ni kusubiri bei elekezi ya serikali ni uhujumu uchumi. 

Ni uhujumu uchumi ambao EWURA wanapaswa kuuchukulia hatua stahiki, hata ikibidi kuwapeleka watu hao katika ile mahakama. Kwa uzembe wetu na mazoea tunaona kuwa ni jambo dogo na kudharau, kisha maisha yanaendelea.

Kuna moja ya kampuni kubwa za mafuta inamiliki vituo kadhaa vya kuuza mafuta, kwa sasa sitaitaja kwa sababu za kibiashara, ambayo imekuwa na kawaida ya kuacha kuuza mafuta hata saa za mchana wakisubiri bei elekezi itoke usiku ili wao wauze kwa faida maradufu. 

Sina uhakika kama mara zote wanapata faida, lakini ninadhani wana mtandao mzuri wa kujua bei kabla haijatangazwa.

Ukiachilia hilo la kuacha kuuza mafuta kama ambavyo leseni yao inawaelekeza, imekuwa ni kawaida kuanza kuzuia mafuta katika matanki yao kwa kufanya biashara watakavyo ili kubaki na mafuta ya kutosha. 

Haiingii akilini kwa mtu akifika katika kituo cha mafuta na  gari lake kisha akae akisubiri wahudumu ambao wanapiga soga  mahali fulani hapo kituoni. Ni dhahiri kuwa mwenye gari ataondoka kwa hasira na ataona hakuna haja ya kujibizana na wauzaji, kwa kuwa vituo vipo vingi.

Uzoefu umeonyesha kuwa vituo hivyo hufungwa muda wa mchana, na vimekuwa vikifunguliwa mapema sana bei ya mafuta inapopanda kutoka katika bei elekezi. Nadhani kuna ombwe kubwa la usimamiaji wa vituo na bado kuna watu hawajamuelewa mkuu wa nchi.

Tufike mahali tuheshimu mikataba yetu ya biashara. Hauna sababu ya kuomba kufanya biashara ya kuuza mafuta na kupewa eneo la biashara na ukashindwa kutimiza mahitaji ya wanaokuzunguka. Biashara ya mafuta inakwenda na hisia zaidi za madereva na wingi wa mafuta yao katika gari, wanapotegemea kuweka mafuta kituo fulani na wakafika wakaambiwa hayapo ni dhahiri kuwa umewalaza njiani na hukutendea haki sheria za leseni ya biashara.

Ushauri wa bure kwa EWURA – anzisheni TAKUKURU yenu, kuna aina mpya ya rushwa na rushwa hii ni uhujumu uchumi kabisa. Fanyeni upelelezi kama wenzenu wa TAKUKURU katika kuwakamata hawa wababaishaji, vinginevyo tutaendelea kuamini kuwa kuna mikono yenu katika vituo hivyo na tutapaza sauti kwamba hamfai kututetea tena katika nishati hii muhimu kwa maisha yetu.

Wasalamu,

Mzee Zuzu,

Kipatimo.