Wakfu ni nini?
Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa Mali, Sura ya 352 ndiyo sheria inayoeleza masuala yote ya msingi kuhusu habari nzima ya wakfu. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Kifungu cha 140, wakfu ni kutoa mali kulingana na sheria za Kiislamu kwa ajili ya dini, hisani au kwa ajili ya watu/mtu wa familia fulani.
Suala la wakfu huenda sambamba na suala la wadhamini. Kwa mujibu wa kifungu hicho, wadhamini ni watu/mtu ambaye ndiye hupewa jukumu la kusimamia mali ya wakfu.
Kama ni nyumba yenye wapangaji, basi mtu au watu hao ambao ni wadhamini ndio watahusika na kukusanya kodi pamoja na mambo mengine yote yanayohusu nyumba. Na kama kuna maendelezo yoyote ya ukarabati au vinginevyo, hawa ndio watahusika.
Maelekezo ya mtoa wakfu lazima yafuatwe
Siku zote mtoa wakfu hutoa mali kwa malengo maalumu. Yaweza kuwa ni malengo ya kiimani au vinginevyo. Mtoa wakfu anapotoa nyumba/kiwanja kama wakfu hutoa kwa maelekezo ya namna na jinsi kitakavyotumika.
Na mali hiyo itapaswa kutumika kulingana na maelezo yaliyotolewa na mtoa wakfu.
Ni kosa mali ya wakfu kutumika kinyume cha maagizo ya mtoa wakfu. Ikiwa itatumika kinyume, basi kuwe na sababu za msingi ambazo zinalazimisha hivyo. Ziwe ni sababu ambazo hakuna namna isipokuwa ni lazima kufanyika hivyo. Kifungu cha 150(1) cha sheria ya mirathi na usimamizi wa mali kinasema kuwa matumizi ya mali za wakfu ni lazima yazingatie nia na malengo ya mtoa wakfu.
Isipokuwa kifungu hicho kinasisitiza kuwa nia na malengo ya mtoa wakfu yatafuatwa tu pale ambapo nia na malengo hayo yatakuwa halali kisheria.
Ikiwa mtoa wakfu ameelekeza matumizi ambayo hayakubaliki kisheria, basi maelekezo hayo hayatafuatwa. Lakini ikiwa hayapingani na sheria yoyote, basi ni sharti kuyafuata.
Ifahamu Tume ya Wakfu
Kuna chombo cha kisheria kinaitwa Tume/Bodi ya Wakfu Tanzania (Wakfu Commission of Tanzania). Kazi kubwa ya chombo hiki ni kusimamia na kuratibu mali zote za wakfu. Wakfu ili uweze kulindwa na sheria hii hutakiwa kusajiliwa. Chombo hiki ndicho kinachohusika na usajili.
Kifungu cha 145(6) kinasema kuwa mali ya wakfu inatakiwa kusajiliwa ndani ya miezi mitatu tangu iwe mali rasmi ya wakfu.
Pia kamati ya wadhamini ambayo ndiyo inasimamia mali za wakfu nayo hutakiwa kusajiliwa ndani ya miezi mitatu tangu kuundwa kwake. Pia mgogoro wowote unaotokana na mali ya wakfu husuluhishwa na chombo hiki.
Nini ufanye mali ya wakfu inapotumika vibaya?
Wakati mali ya wakfu inapotumika vibaya au kufujwa, yeyote mwenye masilahi anaweza kuibua malalamiko. Kifungu cha 146 cha Sheria ya Mirathi na Usimamizi wa Mali kinasema kuwa malalamiko yatapelekwa kwenye Tume/Bodi ya Wakfu.
Lakini pia kifungu hicho hicho kinatoa mamlaka kwa tume yenyewe kuchukua hatua hata kama hakuna mtu aliyelalamika. Tume itachukua hatua mara moja itakapoona mali ya wakfu inatumika kinyume cha malengo ya mtoa wakfu au kuna ufujaji unaofanywa.
Kifungu hicho kinasema kuwa Tume/Bodi itafanya uchunguzi na ikigundua kuwa kuna mambo hayako sawa katika usimamizi wa wakfu, basi inaweza kuichukua ile mali ya wakfu na kuiweka chini ya usimamizi wake au kuteua wadhamini wengine ili kusimamia vema mali hiyo.
Yapo mengi kuhusu wakfu, lakini kwa leo ni hayo.
Kuhusu sheria za ardhi, mirathi, makampuni, ndoa n.k, tembelea SHERIA YAKUB BLOG.