Siku chache baada ya uteuzi wa viongozi wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii – waziri na naibu wake, niliandika waraka mahsusi uliowahusu. Moja ya mambo niliyoyazungumza ni namna wizara hii ilivyo na vishawishi vingi vinavyotokana na ukwasi wake.

 

Katika makala hiyo na kwenye makala nyingi nilizoandika kuhusu Maliasili na Utalii kwa muongo mmoja sasa, nilisema kwamba Watanzania wengi hawajui ukwasi ulio ndani ya wizara hiyo na namna wageni – kwa kushirikiana na mawakala wao Watanzania – walivyoamua kula kimya kimya.

 

Tunapiga kelele sana kuhusu fedha za madeni ya nje (EPA) lakini ukweli ni kwamba Maliasili ni zaidi ya ‘EPA’ yoyote katika taifa letu.

 

Mara zote nimesema kwamba kuandika mambo yanayolihusu Taifa, hasa ukosefu wa uadilifu miongoni mwa viongozi wetu, ni mzigo mzito. Je, Watanzania wote tukae kimya huku tukiona mambo yakienda mrama? Hapana. Woga ni silaha dhaifu katika vita ya kujiletea ustawi wa maendeleo katika Taifa lolote.

 

Ni kwa sababu hiyo, namuomba ndugu yangu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, aniwie radhi kwa haya nitakayoyasema hapa. Nayasema kwa sababu ya dhamana aliyopewa ya kusaidia kuliokoa Taifa letu kiuchumi.

 

Kwa namna ninavyomwona Nyalandu, sidhani kama kweli anaweza kuwa msaada wa maana kwa Waziri wake, kwa Rais aliyemteua na kwa Watanzania wengi. Nasema sioni.

 

Nyalandu, akiwa hata hajajua mlango wa ofisi yake mpya, aliweza kukutana na viongozi wa chama cha wamiliki wa kampuni za uwindaji wa kitalii Tanzania.

 

Kuna habari za uhakika kwamba kwenye mkutano huo, pamoja na mambo mengine, akakubali kuwa kiungo kati yake na waziri wake. Ndiyo maana, katika kuthibitisha hayo, aliweza kufanikisha mkutano kati ya waziri wake na wafanyabiashara hao.

 

Hapa ikukumbwe kuwa mara zote wafanyabiashara hao wamekuwa makini kuwarubuni viongozi wote wanaoteuliwa kuongoza wizara hii.

 

Kama kweli Nyalandu alikuwa na nia nzuri, bila shaka angemshauri waziri aitishe mkutano wa wadau wote ili wajadili changamoto zinazoikabili tasnia ya uwindaji wa kitalii. Hakufanya hivyo.

 

Wafanyabiashara hao wameanza kutamba kwamba sasa mambo yao yatawanyookea. Wameanza kuendeleza juhudi zao za kuhakikisha “wanawaweka mfukoni viongozi wa wizara”. Jeuri yao ni fedha.

 

Haitashangaza sasa kuwasikia wakianza kukusanya fedha kwa ajili ya kumwaga misaada ya “kibinadamu” katika majimbo ya mawaziri wa wizara hii.

 

Pili, Nyalandu ananipa shaka hasa kwa msimamo wake wa miaka yote, wa kuwatetea wenye hoteli za kitalii wasilipe “concession fee”. Nyalandu amekuwa Mjumbe wa Bodi ya Tanapa kwa miaka kadhaa.

 

Alipata kuongoza kamati ndogo ya Bodi ili kupitia suala la “concession fee”. Kumbukumbu za vikao vya Bodi zinaonyesha kuwa kwa muda wote amekuwa upande wa wenye hoteli ambao hawazidi watatu. Amekuwa akipinga ongezeko hilo.

 

Kimsingi ni kwamba sasa wenye hoteli wanachotakiwa kulipa ni asilimia 10 tu ya bei halisi ya upangaji katika hoteli. Kuna mianya mingi ya ukwepaji kodi.

 

Kwa mfano, zipo hoteli ambazo hutoza wageni dola 500 au zaidi kwa usiku mmoja. Ili kuiibia Serikali, wamekuwa wakidanganya kwamba wanatoza dola 50 au 100. asilimia 10 ya dola 50 ni dola tano! Asilimia 10 ya dola 100 ni dola 10! Hiki ndicho kiwango kinacholipwa serikalini!

 

Ili kukwepa wizi huo, ndipo wenye kuipenda nchi wakasema bora kuwepo na kiwango maalumu kwa kila kichwa. Ikapendekezwa kuwa kiwango hicho kiwe dola 40 hadi 50 kwa hoteli zilizo ukanda wa kaskazini ambako utalii ni wa hali ya juu; na kiasi cha dola 20 au zaidi kwa hoteli zilizo katika maeneo ya kusini au magharibi mwa nchi ambako utalii haujashamiri.

 

Kwa utaratibu wa sasa wa kutoza kwa asilimia, Tanapa au serikali inaambulia Sh bilioni 4 pekee kwa mwaka. Lakini kwa utaratibu wa “concession fee” unaopendekezwa, endapo utatekelezwa kikamilifu, mapato yatapanda hadi Sh bilioni 21 kwa mwaka! Kwa maneno mengine ni kwamba kwa sasa, kwa kitengo hiki kidogo pekee, Tanzania inapoteza Sh bilioni 17 kila mwaka!

 

Wakati Bodi ya Tanapa na wadau wengine wakihaha kuona mapato haya yakipanda, Nyalandu anakwaza jambo hili. Hapa lazima tuwe na shaka na dhima yake kwa taifa hili.

 

Hoja yake ni kwamba kutoza “concession fee” kutakimbiza watalii! Hii si kweli. Huu ni ulaghai kwa sababu kwenye “campsite” tayari utaratibu huo wa malipo unafanyika, na kwa kweli ndiyo unaosaidia kuongeza kipato cha Tanapa. Kama “campsite” zimefanya hivyo, kwanini wenye hoteli, tena wachache, wapinge?

 

Ni ajabu kwamba Tanapa ndilo shirika pekee Afrika ambalo linaloingiza asilimia 90 ya mapato yake kupitia viingilio katika hifadhi, na asilimia 10 tu ndiyo inayotokana na wageni wanaolala hotelini. Afrika Kusini ni kinyume. Hili nitalieleza vizuri katika matoleo yanayofuata.

 

Nyalandu alianza mpango huu wa kuwatetea wageni hawa akiwa mjumbe wa Tanapa hadi pale ujumbe ulipokoma kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara. Baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, kapata mwanya mzuri wa kuwatetea rafiki zake.

 

Wiki kadhaa baada ya kushika wadhifa huo, akaitisha kikao cha Menejimenti ya Tanapa. Akaiagiza isaini mkataba (MoU) wa kumalizana na wenye hoteli. Kwa maneno mengine akataka mpango wa “concession fee” ufe.

 

Yeye akatoa maelekezo hayo makali kwa kuwa ndiye aliyekuwa Mwenyekiti. Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa alitoa maagizo hayo makubwa kwa kuwashirikisha wakubwa wake.

 

Kwa bahati nzuri menejimenti ya Tanapa ikamkatalia. Ikasema uamuzi wa suala hilo utatolewa na Bodi. Bodi ilipoketi, ikapinga agizo lake. Ikawa aibu ya kwanza kwa Nyalandu kama Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Hajakata tamaa.

 

Watu walio karibu naye wanasema anachojivunia sana ni ukaribu wake na aliyemteua. Lakini wanaomjua Rais Kikwete wanasema anajidanganya kwa sababu Rais Kikwete hatakuwa tayari kuharibu mambo kwa urafiki tu katika dakika hizi za machweo za uongozi wake.

 

Sina sifa ya utabiri, lakini akili ya kawaida inanituma niamini kuwa Nyalandu atakuwa tatizo kubwa katika Wizara ya Maliasili na Utalii pengine kuliko watangulizi wake wengi. Nasema mimi si mtabiri, lakini utashi wa kawaida unanituma kuamini hivyo.

 

Miezi kadhaa iliyopita, ni Nyalandu huyu huyu aliyejitokeza na kusema “hataki urais”, kana kwamba kuna kundi la watu lililomfuata kumbembeleza agombee nafasi hiyo mwaka 2015.

 

Tuliofuatilia “utetezi” wake tulibaini kuwa hakuna mahali popote ambako alifuatwa kuombwa agombee nafasi hiyo, isipokuwa ilikuwa ni janja yake ya kupima upepo kisiasa kujua mwitikio wa umma juu yake.

 

Walio karibu naye wanasema ndoto hiyo ya urais bado inamtokea mara kwa mara. Ndiyo maana haishangazi kumsikia na kumwona akifanya mambo yanayoashiria uchuro wa kushika nafasi kubwa zaidi.

 

Hofu ni kwamba isije ikawa mpango wake wa kupinga “concession fee” na urafiki wake na wenye vitalu ni maandalizi ya kuwa karibu na wafadhili wake wa baadaye katika kutimiza ndoto ya urais.

 

Tunapokuwa tukiwakosoa viongozi kama kina Nyalandu, ni kwa sababu tunaipenda Tanzania, hasa tunapokumbuka beti hizi ambazo hututoa machozi:

 

“Tazama ramani utaona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka

Nasema kwa kinywa halafu kwa kufikiri, nchi hiyo mashuhuri huitwa Tanzania

Majira yetu haya yangekuwaje sasa? Utumwa wa nchi Nyerere ameukomesha.

“Chemchem ya furaha ama nipe tumaini, kila mara kwako niwe nikiburudika.

Nakupenda hasa hata nikakufasiri, nitalalamika kukuacha Tanzania.

Majira yetu haya yangekuwaje sasa? Utumwa wa nchi Nyerere ameukomesha.

“Nchi yenye azimio lenye tumaini, ndiwe peke yako mwanga wa Watanzania

Ninakuthamini hadharani na moyoni, unilinde nami nikulinde hata kufa.

Majira yetu haya yangekuwaje sasa? Utumwa wa nchi Nyerere ameukomesha.”